• Asema watawamwaga
Kagame, Museveni, Kenyata
na Salehe Mohamed, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, amesema Tanzania itatoa talaka kwa nchi za Rwanda,
Kenya na Uganda ambazo zimeamua kuanzisha Jumuiya ya hiari nje ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Sitta alisema kutokana na nchi hizo
kuonekana kuitenga Tanzania na Burundi ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo,
wameshaanza mazungumzo ya kushirikiana kiuchumi, kisiasa na nchi za Burundi na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC).
Kauli hiyo ya Sitta inatokana na
mikutano ya mara kwa mara inayofanywa na marais Uhuru Kenyata wa Kenya, Paul
Kagame (Rwanda) na Yoweri Museveni (Uganda) kuzungumzia masuala mbalimbali ya
kushirikiana nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri Sitta alibainisha msimamo wa
Tanzania kutengwa na nchi hizo tatu jana bungeni, alipokuwa akijibu maswali ya
wabunge mbalimbali waliokuwa wakitaka kujua kauli ya serikali juu ya vikao
vinavyofanywa na marais hao watatu.
Mbunge wa Viti Maalumu Rukia Ahmed
(CCM), aliitaka serikali ipeleke pendekezo bungeni la kujitoa katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki kabla haijapewa talaka kutoka kwa Rwanda, Uganda na Kenya
ambazo zimekuwa zikifanya mikutano inayojadili masuala ya jumuiya bila
kuihusisha serikali ya Tanzania.
Akijibu hoja hiyo Sitta, alisema ni
mapema kwa Tanzania kupeleka bungeni hoja ya kujitoa katika jumuiya hiyo kwa
kuwa kinachofanywa na nchi hizo kimeshafikishwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri wa nchi wanachama ambaye atakitolea ufafanuzi katika kikao
kitakachofanyika wiki mbili zijazo.
Sitta alifafanua kauli ya Waziri
mwenzake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, hivi
karibuni ya kwamba Tanzania inasubiri talaka akisema yenyewe ndiyo yenye uwezo
wa kutoa talaka kwa jumuiya hiyo kwa kuwa inamiliki asilimia 52 ya eneo lote
huku nchi zilizobakia zikigawana asilimia 48 iliyobakia.
“Hawa wenzetu wanafanya utoto wa
kutuzunguka, sisi tunatumia hekima za mzee Mwinyi aliyesema ‘mwongo, mwongoze’.
Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi tutazibaini, kama ni ndoa
kwenye jumuiya basi sisi ndio tutakuwa tumeoa…hivyo tutatoa talaka wakati
wowote,” alisema.
Naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne
Kilango Malecela (CCM), aliitaka serikali isiendelee na hatua zozote kwenye
jumuiya hiyo ambayo inaonekana kuelekea kuvunjika.
Akijibu swali hilo, Sitta alisema
serikali haijakaa kimya bali imeamua kutoshiriki vikao vyote ambavyo nchi za
Kenya, Rwanda na Uganda zitakuwa zimeshayazungumzia masuala husika na kuamua
kuwa na msimamo wa pamoja nje ya jumuiya.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed
(CUF), alihoji serikali inangoja utafiti gani juu ya kutengwa kwao kiuchumi na
nchi hizo tatu wakati Kenya wameshaingia makubaliano ya kibiashara na Ethiopia
na Sudan.
Katika jibu lake, Sitta alisema
Tanzania imeshafanya mazungumzo na nchi za DRC na Burundi kushirikiana katika
nyanja mbalimbali.
Alisema kuwa DRC ndiyo yenye manufaa
makubwa kiuchumi kwa Tanzania kuliko Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi kwa
sababu mizigo mingi hutegemea bandari ya Dar es Salaam.
“Burundi nao wanatengwa kama
tunavyofanyiwa sisi, lakini tumeamua kushirikiana kikamilifu na DRC pamoja na
Burundi ambao tuna imani wana manufaa makubwa kwetu,” alisema.
Hivi karibuni Tanzania iliingia
kwenye mgogoro na Rwanda baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ushauri kwa Rais wa
Rwanda, Kagame kuketi chini na waasi wa nchi hiyo ili kuzungumzia masuala ya
amani kwa nchi yao.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment