Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa
kivita ICC imeamua sharti Naibu Rais wa Kenya William Ruto avihudhurie vikao
vyote wakati wa kesi yake ambapo ameshtakiwa kutekeleza uhalifu wa kivita.
Viongozi wa mashtaka walipinga uwamuzi wa awali ambapo Bw Ruto angekubaliwa
kushiriki vikao vichache tu huku akitumia muda wake mwingi nchini Kenya.
Hata hivyo mahakama imesema licha ya
uwamuzi huo, huenda akakubaliwa ruhusa ya kutokuwepo baadhi ya siku ikiwa
kutatokea sababu maalum. Mawakili wa Ruto waliambia mahakama kwamba kiongozi
huyo alistahili kuwepo nchini Kenya baada ya nchi hiyo kushambuliwa na
wapiganaji wa AlShabaab ambapo walilenga jumba la biashara la Westgate.
Naibu Rais wa Kenya amekanusha
kuhusika na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008 ambapo takriban
watu 1,200 walipoteza maisha na wengine laki sita kukimbia makaazi yao.Uwamuzi
wa mahakama ya ICC huenda ukazidisha mgogoro kati yake na Muungano wa Afrika
ambapo muungano huo umelalamikia ICC kwa kuwalenga viongozi wa Bara Afrika
Pekee.
Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake
William Ruto na mtangazaji Joshua Arap Sang wameshtakiwa kwa kupanga na
kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi ambapo watu wasiokuwa na hatia
wakiwemo akina mama na watoto walipigwa risasi huku wengine wakikatwakatwa hadi
kufa na magenge ya uhalifu.
Kesi dhidi ya Rais Kenyatta
inatarajiwa kuanza mwezi ujao wa Novemba na mahakama ya ICC imemkubalia
kuhudhuria ufunguzi na siku ya mwisho ya kesi dhidi yake pekee. Wachanganuzi
wanasema ICC iko katika njia panda ambapo inakabiliwa na shinikizo za kimataifa
kutoutamausha utawala wa Kenya.
Chanzo:
BBCSwahili
No comments:
Post a Comment