Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM, Kapteni Mstaafu, John Komba amevunja ukimya na kutamka wazi kuwa Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ndiye chaguo lake na atakuwa Rais ajaye
uchaguzi wa 2015.
Komba anakuwa mtu wa pili kumtaja
Lowassa hadharani kuwa anafaa kwa rais 2015.
Itakumbukwa Mbunge wa Viti Maalumu,
Beatrice Shelukindo (CCM) naye alivunja ukimya baada ya kutangaza kumuunga
mkono Lowassa kumrithi Rais Kikwete.
Shelukindo alitoa kauli hiyo wakati
akiwasalimia wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa
Hosteli ya KKKT, kwenye sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika
nyumbani kwa Lowassa na kuhudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.
Akizungumza na Mwananchi katika
mahojiano maalumu jana, Komba ambaye ni Kiongozi wa Kundi la Uhamasishaji cha
CCM Tanzania One Theatre (TOT Plus), alisema mtazamo wake kwa mtu anayefaa
kumrithi Rais Jakaya Kikwete ni Lowassa.
Komba aliyeingia kwenye siasa
kutokana na msukumo wa mama yake aliyekuwa msaidizi wa Bibi Titi Mohamed,
alisema anazo sababu kuu tano za kumkubali Lowassa kuwa Rais na atasimama popote
kumtetea.
"Nakuambia Lowassa ndiye anafaa
kuwa Rais... unafikiri kuna mwingine. Nina sababu zangu tatu," alisema
Komba na kuhoji:
"Wewe unakwenda kwenye harambee,
nani leo hii anaweza kusaidia kuchangia kwa fedha nyingi na zote hizo ni kwa
maendeleo yanayokusudiwa kama siyo Lowassa?"
alisema Komba ambaye ni mahiri katika
kuinadi CCM, katika kampeni mbalimbali za udiwani, ubunge na urais.Juu ya kuwa
atakuwa katika wakati mgumu endapo anayempigia debe hatokuwa, Komba alisema:
"Mimi sikwambii ni nani, lakini wapo Mawaziri waliomkana, lakini leo hii
wapo kwenye Serikali hii hii ya Rais Kikwete.
"Mimi nasema Lowassa, na kama
akipita sawa nitaburudiiika kwelikweli, lakini kama akiteuliwa mwingine, mimi
nitakuwa naye...nitamwimbia hadi mwisho. Kazi yangu si unaijua, nitampigia debe
kwa kuwa si mtu wa mtu mmoja, ni uteuzi wa wanaCCM ule si wa Komba."
alisema.
Mbali na kumnadi Lowassa, Komba
alisifu uimara wa chama chake kuwa kinaimarika siku hadi siku na ndicho
kinachotoa viongozi wa kweli na hata wananchi wanakikubali.
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya
CCM, Komba ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga, alisema kama chama kuna watu wa aina
nyingi, kuna wasafi, kuna wachafu lakini wote wako kwenye mstari mmoja.
Alisema kuwa vita ya rushwa ndani ya
CCM itamalizika endapo kila kiongozi atasimamia kwenye haki na maadili ya
uongozi na pia kutambua wajibu wake ndani ya chama.Komba alijipigia upatu kuwa
ameleta maendeleo katika jimbo lake kwani jimbo linatazamika ikilinganisha na
miaka ya nyuma kuwa wananchi walikuwa wakiishi maisha ya tabu na kimaskini
ilhali wana raslimali za kutosha.
No comments:
Post a Comment