Waandisi wa habari wa kituo cha rediao cha Shabelle wanajulikana kwa kukosoa serikali
Polisi nchini Somalia walivamia makao
makuu ya kituo cha redio cha Shabelle, na kukilazimisha kufunga matangazo yake
mnamo siku Jumamosi.
Maafisa wakuu wanasema kuwa
wanadhibiti jengo hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na serikali miaka ya nyuma.
Kituo hicho kinasifika kwa kukosoa
sana maafisa wakuu wa serikali.
Hatua ya kudhibiti jengo la kituo
hicho, ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya waandishi
huru wa habari ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali sawa na kundi la kigaidi
la al-Shabaab.
Kituo hicho hata hivyo kiliwahi
kutakiwa kuondoka katika jumba hilo.
Maafisa wa usalama wanasema kuwa
notisi ya siku tano waliyotoa kwa wakuu wa kituo hicho kuwataka kuondoka katika
jumba hilo imefika mwisho lakini wakuu wa kituo hicho wanasema kuwa wanakodisha
jumba hilo kihalali kwa mujibu wa mkataba waliokuwa nao na serikali
iliyotangulia.
Serikali ya Somalia iko katika
harakati ya kumiliki majengo na taasisi zilizokuwa zinamilikiwa na serikali ya
awali.
Wanaharakati wanasema kwua hatua hii
itahatarisha maisha ya waandishi wa habari, wengi wanaoishi katika jengo hilo.
Radio Shabelle iliripoti kwenye
mtandao wake kuwa polisi waliingia katika jengo hilo kwa lazima na hata
kuwachapa baadhi ya waandishi waliokuwa kazini.
Walioshuhudia tukio hilo
walifahamisha shirika la habari la AFP kuwa wafanyakazi wa rediao hiyo
walionekana wakiwekwa ndani ya lori za polisi kwa nguvu.
Hata hivyo polisi walikana kuwa
operesheni yao ilikuwa inalenga shughuli za kituo hicho kwani kinasifika sana
kwa kuwa wakosoaji wakuu wa serikali.
Waziri wa mambo ya ndani anasema kuwa
jengo hilo lilikuwa ofisi za shirika la ndege la Somalia na kwa hivyo basi
linapaswa kurejeshwa kwa serikali.
Aidha wakuu wa kituo hicho wanasema
kuwa walikuwa wanatumia jengo hilo lililokaribu na uwanja wa ndege kihalali
baada ya makubaliano kati yao na serikali ya awali.
Waandishi wa habari nchini Somalia ni
baadhi ya wanaokabiliwa na tisho kubwa la usama dhidi ya maisha yao kama
waandishi, hii ni kwa mujibu wa shirika la waandishi wasio na mipaka.
Waandishi habari 18 waliuawa nchini
Somalia mwaka 2012 huku shirika hilo likisema kuwa waandishi 10 wa Redio
Shabelle wameuawa tangu mwaka 2007.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment