UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa
unaovuma kuelekea kambi ya upinzani, sasa unaonekana kuwaamsha viongozi wa
vyama hivyo baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa wanafikiria kusimamisha mgombea
mmoja wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
kabla ya kuthibitishwa na mmoja wa viongozi hao, zilieleza kuwa hatua ya vyama
hivyo imekuja baada ya ushirika wao waliouunda kupinga upungufu uliokuwemo
kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuzaa matunda.
Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa
maamuzi hayo magumu ya wapinzani yametiwa chachu na kauli aliyoitoa Rais Jakaya
Kikwete ya hivi karibuni ya kukitabiria anguko Chama Cha Mapinduzi (CCM),
katika uchaguzi wa mwaka 2015 au ule wa 2020, kutokana na kile alichodai kuwa
viongozi wa chama hicho kuendekeza rushwa.
Mmoja wa viongozi wanaounda ushirika
huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alithibitisha taarifa hizo huku akisisitiza kuwa nia ya kufanya hivyo ni
kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mbatia, walichokifanya
kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si nguvu ya
soda na badala yake wataendeleza hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbatia alisema kuwa uongozi wa vyama
vya upinzani unatarajia kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja, ili kuhakikisha
wanaiondoa madarakani CCM.
Mbatia ambaye alikuwa akizungumza
katika mahojiano maalumu na RAI Jumatano, alisema hatua hiyo pamoja na ushirika
wao unalenga kudumisha amani na uzalendo kwa kuweka utaifa mbele.
Alisema umoja wanaoendelea kuuonyesha
kwenye mchakato wa Katiba Mpya, ambao unalenga kuweka mbele maslahi ya Taifa
ili kuhakikisha inapatikana Katiba bora yenye kushirikisha Watanzania wote,
wataufanya pia kwenye chaguzi mbalimbali.
"Ili jambo lolote litokee lazima
kuwepo na chanzo, mwanzo wetu wa ushirikiano ulioanza Septemba mwaka huu ndani
ya ukumbi wa Bunge, tutauendeleza.
"Tupo kwenye maridhiano zaidi,
hata muungano wetu wa Tanzania bara na Zanzibar si wa kisheria, viongozi wetu
Nyerere na Mzee Karume walikaa na kuzungumza, hata sisi tunafanya hivyo,
tunatakiwa kuzungumza kwa maslahi ya nchi," alisisitiza Mbatia.
Alisema vyama vyao viliamua kuwa na
ushirikiano wa pamoja kutokana na kubaini kwamba, bila umoja hakuna
kitakachofanikiwa.
"Tumeshaanza kuzungumza kwa
mapana juu ya ushirikiano wetu, ukweli ni kwamba kuna mwelekeo mzuri,"
alisema.
Alisema hatua ya vyama kujadili kwa
pamoja mchakato wa Katiba ni dalili njema za kuelekea kwenye mafanikio na ndio
maana wanaona ipo haja ya kuuendeleza ushirika huo hadi kwenye chaguzi
mbalimbali nchini.
"Tunapaswa kuvifanya vyama vyetu
viwe vya maslahi mapana kwa taifa, ili visionekane vipo kwa ajili ya maslahi ya
viongozi.
"Kwa kuwa tumeweka maslahi ya
taifa mbele kwenye suala la Katiba, tumeona tuwe na mfumo ambao utalisaidia
taifa, ndio maana hata tulipotoka Ikulu tumekubaliana kuwa Tanzania kwanza
vyama baadaye, naamini kwa nia njema hata ule ushirikiano wetu utaendelea mbele
zaidi kwa maslahi mapana ya taifa letu, tunategemea hivyo... tuna mategemeo
mazuri, lazima tufikirie chanya," alisema Mbatia.
Kauli ya Mbatia imeungwa mkono na
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro ambaye ameeleza kuwa chama chao
hakina tatizo kwenye suala la kumsimamisha mgombea mmoja na wako tayari kwa
sababu ushirikiano ni suala la msingi na lenye maana.
"Kulingana na upepo wa kisiasa
ulivyo sasa, ni dhahiri tunahitaji kushirikiana ili kukiondoa chama tawala
madarakani, kwa sababu mahali tulipo sasa ni pagumu.
"Tunachosubiri sasa ili
kukamilisha muungano wetu ni tamko la pamoja kutoka kwa viongozi wa juu wa
vyama vyote, lakini naamini nia ya kusimamisha mgombea mmoja itakubalika bila
kupingwa," alisema Mtatiro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara
ya Habari kutoka Chadema, John Mnyika, alisema ushirikiano kwa sasa umejikita
kwenye suala la kunusuru mchakato wa Katiba na kuwezesha nchi kupata Katiba
bora.
Alisema ushirikiano katika masuala
mengine ikiwamo pendekezo la kushirikiana katika uchaguzi, litatafakariwa kwa
kuzingatia mafanikio katika ushirikiano kwenye suala la mchakato wa Katiba Mpya
ambao tunaendelea nao kwa sasa.
"Huu ndio msimamo ambao naamini
pia viongozi wote wanao.
"Kwa kuzingatia kauli
zilizotolewa na wenyeviti wote watatu Septemba 15 mwaka huu kwenye mkutano na waandishi
wa habari, wakati wa kutoa tamko la pamoja la ushirikiano," alisema.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya
siasa nchini, Dk. Benson Bana ameukosoa uamuzi huo kwa kudai kuwa hawawezi
kuungana kwa sababu hawana kiwango cha kuing'oa CCM madarakani.
Dk. Bana aliweka wazi kwamba, hadhani
kama vyama hivyo vitafaulu kuitoa CCM madarakani, kwa sababu havina mtaji wa
kutosha wa wanachama.
Alieleza kuwa vyama vyote vitatu
vinavyojiona vinaisumbua CCM, ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi,
havijafanya utafiti wa kutosha kubaini mtaji wa wapiga kura walio nao.
Alisema Chadema ina nguvu ndogo Bara
hasa kwenye maeneo ya mijini, CUF ina nguvu Zanzibar na NCCR-Mageuzi haina
nguvu ya aina yoyote jambo linaloashiria udhaifu wa vyama hivyo, ambapo
alivitaka kujipa muda wa kujipanga kabla ya kufikiria kuing'oa CCM.
Wenye mtazamo tofauti na huo wanasema
kuwa endapo hatua hiyo ya vyama vya upinzani itafanikiwa, ni wazi itathibitisha
kauli ya Mwenyekiti wa CCM kwamba chama hicho kijiandae kung'oka mwaka 2015 au
2020.
Hata hivyo bado kuna shaka juu ya
maamuzi hayo ya vyama vya upinzani, kutokana na yale ambayo yamepata
kushuhudiwa katika chaguzi nyingine zilizotangulia hususani zile za viti vya
ubunge.
Imeshuhudiwa katika chaguzi kadhaa
vyama hivyo vikisigana kufikia maamuzi ya kuachiana maeneo ya kusimamisha
wagombea wenye nguvu.
Mwaka 2010 kwenye uchaguzi Mkuu, CUF
kilikitaka Chadema kutosimamisha mgombea kwenye Jimbo la Tunduru kutokana chama
chao kuwa na nguvu, hata hivyo wenzao walikataa.
Hali hiyo pia ilijitokeza kwenye
Jimbo la Kiteto, Chadema iliitaka CUF kutosimamisha mgombea jambo ambalo
halikutekelezwa.
Chanzo: mtanzania
No comments:
Post a Comment