Katika dunia ya leo, watu hususan
wafanyabiashara kuwa na wavuti (website) sio jambo la anasa wala la hiari. Kwa
walio makini wavuti ni jambo la lazima.
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama
za kutengeneza na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake wakiwa
karibu na wateja.
Kila kona katika miji yetu wapo
wataalamu wanaoweza kutengeneza wavuti, achilia mbali kampuni za Tehama kama
vile Wordpress na Blogspot zinazowawezesha watumiaji wake kuwa na wavuti bila
ya kulipia gharama yoyote.
Hata hivyo, kumiliki wavuti sio
mwisho wa safari. Wamiliki wengi wana wavuti, lakini hazifanyi kazi kwa kuwa
zimelala usingizi mnono. Kwa wenye biashara wavuti ni sehemu ya kujitangaza na
pia njia mojawapo ya kuwasiliana na wateja.
Makala haya yanakusudia kuainisha
makosa kadhaa yafanywayo na wamiliki wa wavuti na namna ya kuyaepuka kwa
minajili ya kuupa mafanikio wavuti wako.
Kukosa mwelekeo
Japo wavuti katika dunia ya sasa, ni
sehemu ya biashara, wamiliki wengi hapa nchini hawajui nini kifuate baada ya
kuwa na wavuti. Wengi huishia kwenye hatua ya kuwa na wavuti pekee.
Hivi umejiuliza kwa nini uliamua kuwa
na wavuti? Haingii akilini kama jibu lako litakuwa ulifanya hivyo ili tu nawe
uonekane.
Ili uweze kuona matunda ya wavuti,
lazima ujue lengo na mwelekeo wako. Kwa wenye biashara, mwelekeo huo lazima
uende sambamba na biashara husika. Kwa mtazamo wangu sioni tija ya kuwa na
wavuti kama mtu hatojali maslahi hasa yale ya kibiashara.
Kutokutumia takwimu
Takwimu ni mojawapo ya vitu muhimu
kwenye wavuti wowote. Hata hivyo, wengi hawajui umuhimu wake achilia mbali
namna ya kuzitumia.
Swali muhimu, kama hujui idadi ya
watembeleaji wa wavuti wako, wanafanya nini wakiwa huko au wanapendelea kurasa zipi
za wavuti; utawezaje kupima uwezo wa wavuti uliouanzisha?
Kimsingi, takwimu hutoa picha halisi
ya matumizi ya watembeleaji wa wavuti wako. Aidha takwimu zitakujulisha tabia
za wateja wako, kurasa wanazopendelea, mahala walipo na hata muda wanaopenda kufungua
wavuti wako.
Angalia mfano huu. Unamiliki wavuti
kuhusu mgahawa uliopo Arusha, lakini kwa kutumia takwimu unabaini asilimia
kubwa ya watembeleaji wanapatikana mkoani Dar es Salaam. Kwa mfanyabishara
makini hii ni taarifa ya kuifanyia kazi kwa maendeleo ya mgahawa.
Ili kutatua tatizo hili, unashauriwa
kutumia programu za takwimu, huku ukitafuta wataalamu wanaoweza kukutafsiria
maana ya takwimu hizo kwenye lugha ya kibiashara zaidi.
Katika wavuti nyingi hivi
leo,wahusika wameweka takwimu kuhusu watembeleaji pekee. Idadi pekee haitoshi
kwani kuna mengi yanayopaswa kujulikana ili hatimaye yaweze kufungamanishwa na
bishara na hata uwekezaji kwenye Tehama.
Kukosekana sehemu ya kutafuta taarifa
Kwa wavuti kubwa zilizo na vitu vingi
au kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara, sehemu ya kutafuta taarifa (search
button) ni lazima.
Sehemu hii sio tu itasaidia kuokoa
muda wa watembeleaji wa wavuti ambao hawana muda wa kuanza kujaribu kurasa moja
hadi nyingine, lakini pia utasaidia kuongeza muingiliano kati ya wavuti na
watembeleaji.
Cha muhimu hakikisha unakuwa na
sehemu ya kutafuta taarifa kwenye wavuti wako. Pia hakikisha unaunganisa
kitafuto hiki na mitambo ya takwimu, ili kukupa picha halisi ya vitu gani
ambavyo watu wanavitafuta kwa kiasi kikubwa kwenye wavuti.
Zingatia mfano ufuatao; Una wavuti
kuhusu saluni ya kinamama, ukiwa na sehemu ya kutafuta taarifa na kisha takwimu
zikaonyesha watu wengi wanatafuta bidhaa X, taarifa hiyo itakuwezesha kuboresha
mpango wa biashara yako.
Kurasa zisizoweza kutambazika
Kimsingi watu wengi wanapotafuta
taarifa kwenye wavuti, hawasomi bali wanatambaza (scan) na huondoka mara
wanapokosa taarifa husika. Hapa kuna kosa linalofanywa na wamiliki wa wavuti
hasa Tanzania.
Wamiliki wengi wanashindwa kutoa
picha ya website yao kwa jicho la kwanza. Wavuti na blogu nyingi za Tanzania
zimejaa vitu vingi kiasi msomaji anashindwa aanzie wapi.
Ilivyo hutakiwi kuandika maneno
milioni moja ili kumfanya mtu atumie wavuti wako. Watembeleaji hawana muda wa
kuanza kudokoa kitu kimoja kimoja. Wengi wanadhani, kuwa na makala nyingi ndio
kufanikiwa. Andaa taarifa inayojitosheleza katika njia nyepesi na rafiki zaidi.
Kukipa kisogo Kiswahili
Inasikitisha kuona wamiliki wengi
wakitumia lugha ya Kiingereza kwenye wavuti zao ambazo kimsingi wateja wao
wakubwa ni watumiaji wa lugha adhimu ya Kiswahili.
Inawezekana matumizi ya Kiingereza
yakawa mujarabu zaidi ikiwa biashara husika ni ya kimataifa, lakini kama
biashara ama taarifa inahusu zaidi Watanzania ambao wengi wanatumia Kiswahili,
hakuna haja ya kutumia lugha ngeni.
Matumizi ya lugha ipi inafaa kwenye
wavuti yategemee vitu kama vile lengo na mwelekeo wa wavuti na nani unawalenga.
Ukijiuliza haya utakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua lugha ya kutumia katika
wavuti wako.
Wapo wanaotumia lugha zaidi ya moja
kufikisha taarifa kwenye wavuti zao. Ni jambo la kupongeza na la kuigwa.
Mkata Nyoni ni mtaalamu wa
Menejimenti ya Teknolojia ya Habari na Mshauri wa Biashara. Anapatikana
kupitia barua pepe: mnyoni@dudumizi.com
Pia
Wasiliana na Mmiliki wa Blog hii: ausichiwambor@hotmail.com
No comments:
Post a Comment