• Aponzwa
na ndoa ya mbunge na kinda
na Betty Kangonga
MBUNGE wa Viti Maalumu, Mchungaji
Getrude Rwakatare (CCM) wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),
Mikocheni B, jijini Dar es Salaam, ametengwa katika Ushirikiano wa Makanisa
baada ya kanisa lake kulalamikiwa kufungisha ndoa inayodaiwa kukiuka taratibu
za kikanisa, kisheria na kimaadili, Tanzania Daima Jumatano limejulishwa.
Ndoa inayolalamikiwa kufungishwa na
kanisa hilo ni ile iliyoibuliwa na gazeti hili wiki iliyopita ambayo
inamhusisha Mbunge wa Viti Maalumu, Rosweeter Kasikila (CCM) mwenye umri
wa miaka 60 na kijana Michael Christian wa miaka 26.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika
kanisa hilo Septemba Mosi mwaka 2011, imebaki kuwa gumzo na kuwaacha hoi baadhi
ya mawaziri, wabunge pamoja na majirani wanaoishi jirani na mbunge huyo mjini
Bagamoyo, Pwani.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Jamii ya makanisa hayo, Mchungaji
William Mwamalanga, alisema uamuzi wa kulitenga kanisa la Mama Rwakatare
umetokana na kikao cha Kamati ya Maadili iliyokutana jana jijiji Dar es Salaam.
Alisema Kanisa la Mchungaji Rwakatare
halifai kuendelea kuwa katika ushirika huo kutokana na kubariki ndoa hiyo
aliyodai kuwa ni batili.
Mchungaji Mwamalanga alisema
utaratibu wa ndoa katika makanisa unafahamika, ikiwa ni pamoja na wafungaji wa
ndoa kutakiwa kutangaza ndoa hiyo hadharani kwa kipindi cha wiki tatu.
“Ndoa hii haikutangazwa hadharani,
kibaya zaidi inasemekana imefungwa ndani ya ofisi na sio kanisani. Hiyo haiwezi
kuitwaa ndoa maana haijakidhi vigezo na taratibu za kikanisa, ni lazima
Mchungaji Rwakatare awajibike,” alisema.
Alisema lazima nyumba za ibada
zikubali kutogeuzwa kichaka cha kusaidia uovu kama ilivyofanywa na kanisa hilo
la Mikocheni B kwa kukubali kufanikisha ndoa hiyo kinyume cha taratibu.
“Tunalaani ndoa hiyo kuanzia mawio
hadi machweo kwa kuwa hata maandiko ya kitabu kitakatifu cha Biblia
kinawathamini yatima kama alivyo huyo kijana Michael anayeonekana kutoafiki
ndoa hiyo kwa matakwa yake,” alisema mchungaji huyo.
Alisisitiza kuwa wanamtenga Mchungaji
Rwakatare na kanisa lake kwani amewachafua na kuyatia aibu makanisa
mengine yote nchini.
Mchungaji huyo pia alimtaka
Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete kuwaengua kwenye chama hicho
Mchungaji Rwakatare na Kasikila kuhusiana na ndoa hiyo.
“Rwakatare ni mtunga sheria, anajua
wazi kuwa ndoa inatakiwa pia kubandikwa katika ubao wa matangazo. Ni wazi kuwa
wameamua kuvunja sheria na kutenda kosa la jinai,” alidai.
Mwamalanga alisema kuwa kwa hatua
hiyo ndoa hiyo ni batili na haramu kwa kuwa ni aibu pia kwa mtoto kumuoa
mwanamke mwenye umri wa mama yake.
Katika hatua nyingine, mchungaji huyo
alisema umoja wao unafanya kila iwezalo kuhakikisha kijana Michael anarudishiwa
vyeti vyake ambavyo kwa sasa vimezuiliwa na Mbunge Kasikila.
Pia aliitaka Kamati ya Maadili ya
Bunge kuwaita na kuwahoji wabunge hao kwa kitendo chao cha kuhalalisha ndoa
hiyo kwani kimeutia doa muhimili huo.
Alisema Bunge ni sehemu tukufu, hivyo
Rwakatare na Kasikila hawana hadhi ya kukaa huko, hivyo alishauri waenguliwe.
Alipopigiwa simu kueleza msimamo wake
juu ya uamuzi wa umoja wa makanisa hayo kumtenga kwa kuhalalisha ndoa hiyo,
Mchungaji Rwakatare aling’aka na kukata simu.
Alipopigiwa tena simu yake ilizimwa
na hakuweza kupatikana tena hadi tunaenda mitamboni.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment