Thursday, October 31, 2013

Saini zakusanywa kumng’oa Makinda



Spika wa Bunge, Anne Makinda (kulia) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka na Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola katika Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI

Na Sharon Sauwa,Mwananchi
Kwa ufupi
“Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo. Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa,”

Dodoma. Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.

Dk Kigwangalla aliibua hoja ya kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge wote cha kuelezea shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13, kilichofanyika juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jana alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge, lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika Makinda.

Chanzo chetu kutoka katika kikao hicho cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji kuhusiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine wenyeviti na makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamati husika.

Pia Dk Kigwangala alisema Spika Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000 kwa siku wajumbe wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000.

“Anachokifanya Spika ni matumizi mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata bila posho lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa siku?” chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.

“Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo. Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa,” alisema Dk Kashililah.

Katibu huyo wa Bunge alieleza kuwa zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa maana ya kutaka posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwa zinakabiliwa na majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu wa kawaida.

“Kimsingi, kamati nyingi zinapewa malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa saba au nane usiku, au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na maelezo ya kazi husika, basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo,” alisema Dk Kashililah.

Kuhusu Serukamba
Aidha, Dk Kigwangalla alinukuliwa akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.

“Hakuna mbunge yeyote aliyepo katika kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu maalumu basi wa kuteuliwa angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka ya Mapato Nchini) ipo chini ya kamati yake,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema Dk Kigwangalla alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki, Mgimwa alipokwenda katika kamati hiyo aliambulia kufukuzwa.
Akizungumzia suala hilo, Dk Kashililah alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa waliteuliwa na Spika kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo wakati wa kipindi cha Bajeti Kuu ya Serikali.

Aliwataja wabunge wengine walioteuliwa kushiriki katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa ni John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi Rashid Mohamed (Wawi - CUF).

Kanuni za Bunge
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge katika toleo la mwaka 2007, kifungu cha 137(1), ili kumwondoa Spika madarakani, mbunge anayetaka kuwasilisha hoja hiyo atatakiwa kuwasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu, akieleza sababu kamili ya kutaka kuleta hoja hiyo.

Kifungu kidogo cha pili kinasema baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumwondoa Spika kwenye madaraka, Katibu atapeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.

Kifungu cha tatu kinabainisha kuwa endapo kamati hiyo itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya ibara husika za Katiba, sheria au kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyo itaidhinisha hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.

Kanuni zinasema Naibu Spika, atakalia Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumwondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala na kwamba ili kumwondoa zinahitajika kura zisizopungua theluthi mbili ya idadi ya wabunge wote.
Chanzo: Mwananchi

No comments: