Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu
Chiku Gallawa, amesema watu waliomuua askari mgambo Salum Mgonje na kumpiga
risasi Mkuu wa Kituo cha Polisi Songe, wilayani Kilindi Edward Lusekolo ni
kikundi kilichokuwa kinaishi msituni.
Alisema kikundi hicho kinaipinga
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kudai ni ya kikafiri kikiwa na mipango ya
kutaka Tanzania isitawalike.
Akizungumza na waandishi wa habari
Mjini Handeni, Bi. Gallawa alisema kikundi hicho kiliweka kambi tatu wilayani
humo kikifanya mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kijeshi.
“Pia kikundi hiki ndicho kilichokuwa
kikipinga mchakato wa sensa mwaka 2012, kambi zao tatu zilikuwa katika Kata ya
Lwande na Negero kwenye Kijiji cha Madina.
“Katika kambi ya Madina, wafuasi wao
wawili wameuawa baada ya kupinga kitendo cha kukamatwa na askari Oktoba 26
mwaka huu wakijiita wafuasi wa Sunni,” alisema.
Aliwataja wafuasi waliouawa kuwa ni
Ramadhan Hamis, ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mwingine jina lake
halikufahamika mara moja lakini inasemekana ni mwalimu wa dini ya Kiislamu
(ustaadh) Kijiji cha Lwande.
Aliongeza kuwa, kikundi hicho
kimekutwa na bunduki tatu aina ya gobore, shortgun moja, bastola mbili
zilizotengenezwa kienyeji, mapanga 18 na visu 10.
Bi. Gallawa alisema wafuasi 46 wa
kikundi hicho tayari wamekamatwa lakini jambo la kushangaza wamo watumishi wa
Serikali ambao ni walimu wa shule za msingi na watafikishwa mahakamani wakati
wowote.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa,
ambayo inaongozwa na Bi. Gallawa, imeamua kuweka kambi Kilindi kwani hivi sasa
hali ya usalama si nzuri hadi itakapotulia.
Akizungumza na Majira hivi karibuni,
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constantine Masawe, alisema askari mgambo Salum
Mgonje aliuawa Oktoba 22 mwaka huu ambapo Edward alipigwa risasi za mbavu na
mkononi Oktoba 23, saa mbili usiku.
Kikundi hicho kinajumuisha wakazi wa
vijiji mbalimbali wilayani humo ambao wamefukuzwa na wenzao kutokana na tabia
zao za kupinga mambo mbalimbali ya maendeleo.
Chanzo cha kuanzishwa kikundi hicho
ni baada ya mwenzao mmoja ambaye ni mfanyabiashara kutakiwa kulipa ushuru
katika Kijiji cha Lwande na kukataa hivyo mgambo waliingilia kati ndipo wafuasi
wao walichukua uamuzi wa kwenda kuwakata mapanga mgambo ambao mmoja alijeruhiwa
na mwingine kuuawa.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment