Kiongozi wa ngazi ya juu anayeongoza mashambulizi ya kujitoa
mhanga ya kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda ameuawa katika
shambulizi la ndege isiyoruka na rubani Kusini mwa Somalia
Waziri wa Mambo ya Ndani, Abdikarin
Hussein Guled, ameiambia redio ya serikali kuwa idara ya ujasusi ilikuwa
ikimfuatilia Ibrahim Ali Abdi, maarufu kama Anta-Anta, kwa muda sasa kabla ya
shambulizi hilo kufanywa jana Jumatatu 28.10.2013
Waziri huyo hajasema ni nani
aliyefanya shambulizi hilo, lakini afisa mmoja mjini Washington amesema jeshi
la Marekani lilifanya shambulizi la ndege isiyoruka na rubani likililenga kundi
la al-Shabaab nchini Somalia jana Jumatatu.
"Operesheni hiyo ambayo mtu huyu
aliuawa ilikuwa muhimu kwa serikali. Mtu huyu alikuwa na jukumu kubwa kwa raia
wengi wasio na hatia na kifo chake kitasaidia kurejesha amani," alisema
waziri huyo kupitia Radio Mogadishu.
Maafisa kutoka serikali ya Somalia
inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa wamemtaja mwanamgambo aliyeuawa kuwa
anayefahamika vyema kwa kutengeneza mabomu ya kuvaa mwilini pamoja na ya
kutengwa ndani ya gari ambayo hutumiwa mara kwa mara na waasi kuyashambulia
maeneo ya serikali. Hapajakuwa na kauli yoyote kutoka kwa wapiganaji hao.
Shambulizi hilo linakuja wiki chache
baada ya shambulizi kali kufanywa katika jumba la maduka ya Westgate jijini
Nairobi, Kenya, lililodaiwa kufanywa na al-Shabaab ambapo watu 67 waliuawa.
Kisha kikosi maalumu cha jeshi la
wanamaji la Marekani kikafanya shambulizi katika bandari ya kusini ya Barawe
mapema mwezi huu (Oktoba) na kushindwa kufikia lengo lake: ambalo lilikuwa ni
kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa al-Shabaab na Mkenya mwenye asili ya kisomali
kwa jina Abdulkadir Mohammed Abdulkadir, pia anayefahamika kama Ikrima.
Afisa mmoja wa Marekani ambaye
hakutaka kutajwa jina lake, hajasema sehemu ambayo ndege hiyo isiyoruka na
rubani ilianzia safari yake, lakini jeshi la Marekani huendesha shughuli zake
za ndege hizo kutoka kambi za nchini Djibouti na Arba Minch kusini mwa
Ethiopia.
Wapiganaji wa al-Shabaab wametimuliwa
kutoka miji mikuu ya Somalia, ikiwa ni pamoja na Mogadishu na bandari ya kusini
mwa nchi hiyo Kismayo, kufuatia operesheni ya jeshi la Umoja wa Afrika
linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa na ambalo sasa lina wanajeshi 17,700.
Kundi hilo hata hivyo linayadhibiti
maeneo makubwa ya kusini mwa Somalia na katika kipindi cha miezi kadhaa
iliyopita, limekiongeza kiwango cha mashambulizi yake ya kujitoa mhanga.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment