Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo amewataka wapiganaji wa makundi yote ya waasi mashariki
mwa nchi yake kuweka silaha zao chini, baada ya kile kinachoaminika kuwa ni
kusambaratika kwa kundi la M23.
Akihutibia taifa hapo jana (tarehe 30
Oktoba) kwa njia ya redio na televisheni, mara tu baada ya jeshi la serikali
kuuteka mji wa Bunagana, Rais Kabila alilipongeza jeshi hilo na wale Umoja wa
Mataifa kwa kulirejesha eneo la Rutshuru mikononi mwa serikali.
Hata hivyo, Rais Kabila akasema
pamoja na ushindi huo wa kijeshi, diplomasia na mazungumzo baina ya Wakongomani
yataendelea.
“Ninasisitiza wito wangu kwa wapiganaji
wa kundi lililofurushwa kwenye mitaa ya Nyiragongo na Rutshuru kutua silaha zao
chini kwa ikhari yao wenyewe kulingana na pendekezo la Nchi za Maziwa Makuu.
Kinyume cha kufanya hivyo tutalazimika kuwapokonya silaha kwa nguvu. Wito wa
aina hiyo hiyo unatolewa pia kwa makundi mengine ya wapiganaji ya kitaifa,
kusitisha hatua zote za kijeshi kutasababisha wao na wengine kufaidika na
mpango wa kuingizwa katika maisha ya kawaida.” Amesema Rais Kabila.
Kabila azionya nchi jirani, makundi
ya kigeni
Katika hotuba hiyo ya kwanza tangu
taarifa za kusambaratika kwa kundi la waasi wa M23 mashariki kwa nchi hiyo,
Rais Kabila aliyatahadharisha pia makundi ya wapiganaji ya kigeni yalioko
nchini huko Kivu.
“Kuhusu makundi yaliosalia ya kigeni
yakiwemo FDLR, LRA, ADF/Nalu na FNL yanayoendelea kutaabisha wakaazi wa Kivu ya
Kusini na Kivu ya Kaskazini, ninayatahadharisha kutua chini silaha haraka sana.
Vyenginevyo, makundi hayo yatapokonywa silaha kwa nguvu na yatachukuliwa hatua
kama tunayoendesha hivi sasa.”
Katika hatua nyengine, Rais Kabila
ametumia hotuba hiyo kuzionya nchi jirani,ambayo hakuzitaja jina, kwamba amani
ya kudumu ya Kanda la Maziwa Makuu itatokana na utekelezwaji wa Mkataba wa
amani wa Addis Ababa.
“Kwan nchi jirani, ninaziambia mara
nyingine kwamba njia muafaka ya kuleta amani na ustawi wa ukanda huu, ni
utekelezwaji wa dhati na kwa nia nzuri kwa Mkataba wa Amani wa Addis Ababa na
vile vile Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ninawahimiza kutekeleza wajibu wao kulingana na mkataba huo.”
Anyoosha mkono wa diplomasia
Rais Kabila amesema ijapokuwa ushindi
wa kijeshi umepatikana, lakini juhudi za kidiplomasia na kisiasa zitaendelea.
“Mtizamo wetu ni ule wa kutafuta
suluhisho la mzozo wa Kongo kwa njia tatu: ya kijeshi, ya kisiasa na
kidiplomasia. Na ndilo tunalofanya sasa. Ushindi wa kijeshi huko Kivu hauwezi
kuvunja juhudi zingine za kisiasa na kidiplomasia.”
Kufuatia ushindi wa jeshi la Kongo
dhidi ya waasi wa M23, Rais Kabila aliwapongeza wanajeshi na kusema wameungwa
mkono na taifa nzima.
Vile vile, aliwapongeza wanajeshi wa
Tanzania katika kazi wanayoifanya kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa na kutoa
heshima zake na rambirambi za pole kwa familia ya wanajeshi wa Kongo na wale wa
Tanzania waliopoteza maisha yao kwenye uwanja wa mapambano.
Rais Kabila alitoa wito wa kutokueko
na ulipizaji kisasi baina ya Wakongomani.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW
Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Khelef
No comments:
Post a Comment