Na Sharon
Sauwa na Habel Chidawali,Mwananchi
Dodoma. Wabunge jana walichachamaa na
kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo wanaojihusisha na ujangili wakati wa
kikao cha kwanza cha mkutano wa 13 wa Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa
majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara
hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha
maswali na majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo,
akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua viongozi wake na
wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao wanatajwa kuhusika na vitendo
vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu
Spika baada ya kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza
Bunge kuwa Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini
bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa wamebainika
kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali
kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa
majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,”
alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa
zimewataja watu wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini,
mawaziri pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna
yeyote miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa
kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa
ikiendeshwa kwa unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi
unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale
wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani,
zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya
Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao
wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya
mwongozo ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa
vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa
msaidizi wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya
kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa
tukio hilo anao kwenye simu yake.
“Lakini sisemi haya kwa kutaka
kuitetea Serikali kuwa isilete ripoti hapa bungeni. Nadhani kuwa kuleta ripoti
hivi sasa haitakuwa vizuri. Ni vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina
uhakika kuwa Wizara itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika,”
alisema na kuongeza:
“Nadhani kuwa `entry point’ (mahali
pa kuanzia) yetu iwe ni kwenye ripoti hii itakayowasilishwa kwenye Kamati,”
Suala la ujangili limeingizwa bungeni
wakati kukiwa na usiri mkubwa wa nani anahusika na vitendo hivyo, huku majina
ya vigogo wanaotajwa kuhusika nayo wakiwa hawafahamiki.
Polisi watajwa vinara
Awali akijibu swali la msingi
lililoulizwa na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile, Nyalandu
alisema Jeshi la Polisi ni vinara miongoni mwa makundi manne ya majeshi ambayo
watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili.
Katika matukio saba ya ujangili
yaliyowahusisha watumishi tisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, Nyalandu
alisema kati ya hao sita ni polisi wakati kwa kupande wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza alikamatwa mtu mmoja
mmoja.
“Katika matukio hayo, jumla ya meno
ya tembo 686 na vipande 447 vikiwa na uzito wa kilogramu 4,253.9 vilikamatwa,
jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa tatizo hilo kwa vyombo vya ulinzi,” alisema
Nyalandu.
Katika swali la msingi, Dk Ndugulile
alitaka kufahamu idadi ya matukio ya upatikanaji wa pembe za ndovu
yaliyohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika swali la nyongeza, Lembeli
ambaye ndiye aliyeuliza swali hilo kwa niaba ya Dk Ndugulile, aliitaka Serikali
kuacha kigugumizi na kueleza ukweli kuwa wapo baadhi ya viongozi, wakiwamo
wabunge ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
“Katika biashara ile kuna hali ya
kulindana sana, hebu Serikali itueleze taarifa za kuwa wahusika wengine ni
wanasiasa na baadhi ya wabunge, ukweli uko wapi, na kuna taarifa kuwa viongozi
wa Polisi wanaoishi kuzunguka hifadhi zetu ndio ambao wanatumiwa kusafirisha
nyara hizo, Serikali inasemaje?” alihoji Lembeli.
Nyalandu alisema Tanzania iko katika
hali mbaya katika kiwango cha mauaji ya tembo ambapo wastani unaonyesha kuwa
kila siku tembo 30 huuawa na majangili.
“Hata hivyo, suala la ulinzi bado
tuko nyuma sana kwani wastani wa ulinzi wa kimataifa ni askari mmoja kwa
kilomita za mraba 25, lakini sisi askari wetu mmoja analinda kilomita za mraba
150 ndani ya hifadhi,” alisema Nyalandu.
Serikali yakiri tatizo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu,
alikiri kuwapo fununu za wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara
hiyo na kusema Serikali italifanyia kazi jambo hilo.
Nahodha aliwataka Watanzania kuwa
watulivu wakati vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaposhughulika na kusafisha
tatizo hili na kuonya wanasiasa kuacha kutoa shinikizo kwa kutumia nguvu zao za
kisiasa.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment