Kwa wiki kadhaa hapa nchini
inaendeshwa operesheni ya kupambana na ujangili wa tembo na wanyama wengine
chini ya kikosi maalumu kinachoundwa na maofisa kutoka katika vyombo vya dola,
maarufu kwa jina la Operesheni Tokomeza.
Taarifa mbalimbali zimekuwa
zikiripotiwa kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya kikosi hiki, ikiwamo watu
mbalimbali kukamatwa wakidaiwa kuhusika na ujangili, hasa wa meno ya tembo,
uhalifu ambao kwa siku za karibuni umeichafua sana nchi yetu kimataifa.
Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa
umma na wa kisiasa wamekamatwa katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro, Arusha,
Ruaha, Iringa, Mahenge, Maswa, Meatu na kwingineko ambako pia, ushahidi wa aina
tofauti umepatikana kuhusiana na vitendo vya ujangili.
Kukamatwa kwa watuhumiwa katika
maeneo yote hayo ni ushahidi kwamba majangili wana mtandao mpana unaotumia
nguvu za kifedha, kisiasa au za ulinzi wa dola kujiimarisha katika maeneo mengi
ya nchi, na kuendelea kuhujumu maliasili za taifa.
Hata hivyo, pamoja na lengo zuri la
operesheni hiyo, yapo madai ya kikosi hicho kutumia mabavu na ukiukwaji wa haki
za binadamu, ikiwamo kupiga watu ovyo, kujeruhi na hata kuua watu kadhaa
wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili.
Pamoja na kwamba malalamiko dhidi ya
operesheni hiyo yanatakiwa kushughulikiwa na ukiukwaji huo wa haki za binadamu
kukomeshwa, madai hayo yanatakiwa kutazamwa kwa umakini kulingana na unyeti wa
tukio na mazingira yake.
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa
isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali
inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja
anatendewa kadri ya matendo yake.
Tunatambua kuwa operesheni yoyote
inayowahusisha watu wazito inakuwa na changamoto na vikwazo vingi, hali
inayowasukuma hata wabunge kuanza kushinikiza Serikali kutoa orodha ya vigogo
wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Kwa mujibu wa madai ya wabunge hao na
taarifa za vyombo vya habari, biashara hiyo haramu inawahusisha baadhi ya
wabunge, mawaziri, watumishi wa Serikali na maofisa katika vyombo vya dola.
Jeshi la Polisi limetajwa kuongoza
miongoni mwa makundi manne ya majeshi, ambayo watumishi wake wamekamatwa
wakijihusisha na ujangili katika matukio saba ya ujangili. Wengine ni kutoka
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na
Magereza.
Mathalan, kwa jinsi tatizo hilo
lilivyo kubwa, katika matukio ya karibuni yaliyohusisha maofisa wa vyombo vya
dola, jumla ya meno ya tembo 686 yaliyotokana na kuuawa kwa tembo 343
yalikamatwa, na vipande vingine 447 vilipatikana.
Kwenye operesheni ya namna hii ambayo
Serikali imekiri kuwapo fununu za wanasiasa kuwa miongoni mwa majangili, ni
lazima kuwepo vikwazo na shinikizo la kuizuia au kukwamisha, kwa vitisho au
malalamiko ya umma kutoka kila kona ili kuhakikisha operesheni husika
haifanikiwi.
Kutokana
na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliyoitia juzi bungeni akiwataka wanasiasa kuacha
kushikiza kwa kutumia nguvu zao za kisiasa, kusitishwa kwa operesheni hiyo kwa
sababu yoyote, kwa kuwa tunaamini shughuli kama hii haiwezi kufanikiwa iwapo
itaendeshwa kama lelemama.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment