Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa
akizungumzia kuhusiana na tukio la mtoto wa miaka 11 aliyeolewa na binamu yake.
Mtoto huyo sasa anaishi nyumbani kwake. Picha na Sharon Sauwa.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Imetokea Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa amchukua mtoto
huyo aliyeolewa, aahidi kumsomesha.
Dodoma. Katika hali ya kawaida, binti wa
miaka 11 (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili), mkazi wa kijiji cha
Kongogo, Wilayani Bahi mkoani Dodoma hivi karibuni aliolewa na binamu yake,
kisha ndoa yake kuvunjwa na Serikali.
Hakuna taarifa nyingi za mabinti
kuolewa katika umri mdogo katika wilaya hiyo mbali ya kuwepo kwa watoto wadogo
ambao huondolewa katika masomo na wengine kushindwa kupata elimu kwa
sababu wazazi wao huwapeleka migodini na wengine maeneo ya mijini kutumikishwa
majumbani.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi,
Betty Mkwasa, anasema wilaya yake inaongoza mkoani hapa kwa kuwa na kiwango
kikubwa cha vitendo vya ukeketaji wa wanawake ikiwa nayo ni sehemu ya
ukatili wa kijinsia.
Lakini kwa tukio hilo,
lililojitokeza katika moja ya familia ya wafugaji, kunaweza kukafanya umuhimu
wa kujikita katika utafiti wa kina kuliangalia suala la kuolewa katika umri
mdogo lina ukubwa gani mkoani hapa.
“Hazungumzi na mtu yeyote humu ndani
na unaweza kumsemesha anakuangalia tu, ila anazungumza na mimi (Mkwasa), ama
wasichana wawili tu wa hapa ndani ambao anashinda nao,”anasema Mkwasa ambaye
sasa anamlea mtoto huyo.
Maneno hayo yanathibitishwa na
mwandishi wa makala haya, aliyefika nyumbani kwa Mkwasa kwa nia ya
kuzungumza naye baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa mtoto huyo.
Anapoitwa kwa nia ya kutambulishwa,
anafika mlangoni na kubaki akiangalia tu huku wakati mwingine akiinamisha macho
yake chini na hata anaposalimiwa haitikii, badala yake anaondoka na
kwenda kujificha ndani.
Hali hii iliweka ugumu katika kufanya
mahojiano naye, lakini kwa usiri mkubwa inatubidi kumtumia mmoja wa wasichana
ambaye amekuwa muwazi kwake kusikia nini kilichotokea.
Si kwamba hazungumzi, la hasha binti
huyu ni mzungumzaji mzuri na tunapotoka nje na kuwaacha wawili ndani ya sebule
hiyo tunawasikia wakizungumza na hata kucheka kwa sauti.
Mkwasa anasema siku za mwanzoni
binti huyo alikuwa haongei na mtu yoyote lakini baada ya kuhudumiwa na
mwanasaikolojia ambaye hufika nyumbani kwake kila baada ya siku tatu, alianza
kuongea.
Akisimulia tukio hilo, Mkwasa anasema
mtoto huyo alikutwa akizubaa na akiwa amechoka katika kijiji cha Mindola baada
ya kutoroka kwa mwanamume aliyeolewa naye.
Anasema alipigiwa simu na viongozi wa
kijiji hicho na kuagiza apelekwe katika kituo cha polisi.
“Nilikuwa kwenye kikao mjini,
nikawaambia OCD (Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya), akae naye mtoto huyo
hadi nitakaporejea, nilimwona mtoto. Hakuwa katika hali nzuri sana kwanza
alikuwa mwoga, halafu hakuwa anaongea na mtu yeyote,”anasema.
Anasema polisi walimshauri kumpeleka
mtoto huyo kwa daktari kwa ajili ya vipimo ambapo iligundulika kuwa
ameshaingiliwa sana kimapenzi na kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
“Alipewa dawa na tukarudi nyumbani.
Licha ya kulalamika kuwa anasikia maumivu, hata kaa yake pale nyumbani kwa siku
za awali haikuwa nzuri,”anasema Mkwasa.
Anasema baada ya siku mbili mtoto
huyo alionekana anajisaidia haja ndogo iliyochanganyika na damu, hali
iliyomfanya kumrudisha tena hospitali alifanyiwa vipimo na kupewa dawa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment