JENGO LA MAKTABA TEKU UNIVERSITY
Mbeya. Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji
(Teku) kimewataka wahitimu wa
elimu ya juu nchini kufanya kazi kwa uadilifu,
bidii na kufuata maadili ya nchi ili kuiokoa nchi katika lindi la ufisadi.
Mkuu wa chuo hicho ambaye pia ni
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo alitoa wosia
huo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya sita ya chuo hicho, ambapo wanafunzi
2,855 walihitimu katika masomo ya ngazi mbalimbali.
Askofu Cheyo alisema wahitimu wa
kipindi hiki hawana budi kuacha kufikiria zaidi ufisadi,badala yake waishi na
kufanya kazi kwa bidii na kuacha tabia za wizi wa mali ya umma ili kuiepusha
nchi kutumbukia kwenye dimbwi la wezi.
Awali, Makamu Mkuu wa chuo hicho,
Profesa Tuli Kassimoto aliwaambia wageni waliohudhuria mahafali hayo kwamba
katika programu ya shahada ya wanachuo 1,163 wakiwamo wanaume 717 na wanawake
446 waliohitimu.
Alisema wanafunzi 187 kati ya hao
walipata daraja la kwanza wakati wengine 797 walipata daraja la pili la juu
huku wengine 173 wakipata daraja la pili la chini.
Profesa Kassimoto aliishukuru
Serikali kupitia TCU kwa kukiruhusu chuo chake kufungua matawi katika Mkoa wa
Tabora na Dar es Salaam,ambako wanafunzi wa mwaka wa kwanza wameanza masomo na
kwamba lengo ni kuendelea kutoa wigo kwa vijana wengi kupata elimu iliyo bora.
Hata hivyo alisema chuo chake kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za
ofisi zisizokidhi hadhi ya vyuo vikuu na uchache wa hosteli.
No comments:
Post a Comment