Mapigano ya siku tatu mfululizo baina
ya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 katika
miji ya Kiwanja, Rutshuru na Kibumba sasa yanaonekana kutulia, baada ya jeshi
kuidhibiti miji hiyo.
Mapigano hayo yaliyoanza Ijumaa
iliyopita yaliendelea hadi jana Jumapili (tarehe 27 Oktoba) na kupelekea
kuanguka kwa miji ya Kiwanja na Rutshuru katika mikono ya jeshi la serikali,
likiungwa mkono na vikosi vya Umoja wa Mataigf nchini humo, MONUSCO.
Katika mapigano hayo, mwanajeshi
mmoja wa Umoja wa Mataifa kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alipoteza
maisha. Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Martin Kobler,
amelaani vikali kuuawa kwa mwanajeshi
huyo, ambaye amepoteza maisha yake wakati akitekeleza jukumu lake la kuwakinga
raia wa kawaida.
Nao wakaazi wa mji wa Kiwanja, ambao
kwa takribani mwaka moja sasa walikuwa chini ya uongozi wa M23, wamewakaribisha
wanajeshi wa serikali kwa mayowe na nderemo, wakiomba kwamba wanajeshi hao
wabaki kuwalinda daima.
Makaburi ya Halaiki
Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini,
Julien Paluku, aliutembelea mji mdogo wa Kibumba hivi karibuni na ametangaza
kugunduliwa makaburi ya pamoja mawili katika mji mdogo wa Kibumba. Gavana huyo
ameomba jumuia ya kimataifa pamoja na Monusco kuendesha uchunguzi wa kina ili
waliohusika na uhalifu huo waadhibiwe.
"Ni uhalifu wa vita na uhalifu
dhidi ya binadamu. Na ikiwa itabainika kuwa wahanga walifanyiwa unyama huo
kutokana na kabila lao, ni mauwaji ya kimbari. Kwa hiyo nadhani kwamba MONUSCO
pamoja na jumuia yote ya kimataifa, pamoja na mashirika ya kutetea haki za
binaadamu, wanaalikwa kwa haraka kwenda huko iliwaliohusika wajulikane na hasa
kwani eneo hilo lilikuwa chini ya uongozi wa M23 na kama ni M23 waliohusika
wapelekwe mahakamani, na pia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC
ijulishwe."
Umoja wa Mataifa wawaalika M23
kujisalimisha
Na wakati vita vikiendelea, Kikosi
cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo kimewafungulia milango
wapiganaji wa M23 wajisalimishe. Hayo yalitangazwa na ofisa wa Tawi la Siasa
katika MONUSCO Goma, Josuas Obate.
Waasi wa M23,baada ya kupoteza miji
ya Kiwanja na Rutshuru, kilomita 80 kaskazini ya mji wa Goma, wanaliomba jeshi
la serikali kushimamisha vita ili kuendelea na mazungumzo ya mjini Kampala.
Msemaji wa chama hicho, Amani
Kabasha, alisema ikiwa serikali haitashimamisha mapigano, watalazimika
"kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya ngome za jeshi la serikali,
FARDC."
Mwandishi: John Kanyunyu/DW Goma
Mhariri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo:
DWSwahili
No comments:
Post a Comment