Generali Keith Alexander mkurugenzi wa
Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA.
Hasira iliyozuka barani Ulaya
kutokana na upelelezi wa Marekani inatishia makubaliano ya mabilioni ya dola
katika biashara kati ya Marekani na Ulaya na mazungumzo ya mkataba mwengine
wenye thamani ya mabilioni ya dola.
Idadi inayoongezeka ya maafisa wa
Ulaya wanatowa wito wa kusitishwa kwa makubaliano yanayojulikana kama ya
"eneo salama" ambayo yanaruhusu makampuni ya Marekani kufanya mauzo
ya data za kibiashara na kibinafsi, baruwa pepe na picha kutoka kwa wateja
barani Ulaya. Makubaliano hayo ambayo hayajulikani sana lakini muhimu
yanayaruhusu makampuni ya Marekani zaidi ya 4,200 kufanya biashara barani Ulaya
yakiwemo makampuni makubwa ya mtandao kama vile Apple, Google, Facebook na
Amazon.
Kufichuka kwa kiwango cha upelelezi
unaofanywa na Marekani kwa washirika wake wa Ulaya pia kunatishia kutibua
mojawapo ya malengo makuu ya Rais Barack Obama wa Marekani kwa uhusiano kati ya
Marekani na Ulaya: makubaliano makubwa ya kibiashara ambayo yataongezea dola
bilioni 138 sawa na euro bilioni 100 kwa mwaka kwa pato la uchumi ndani ya nchi
kwa pande zote mbili.
Uaminifu umevunjika
Maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya
wanasema uaminifu uliokuwa ukihitajika kwa ajili ya mazungumzo hayo umevunjwa.
Kamishna wa Haki wa Umoja wa Ulaya,
Viviane Reding, amesema katika hotuba yake kwenye Chuo Kikuu cha Yale hapo jana
kwamba ili mazungumzo magumu na makubwa yaweze kufanikiwa inabidi kuwepo
uaminifu miongoni mwa washirika wa mazungumzo.
Maafisa wa Ulaya wanatarajiwa kudai
Marekani iimarishe kwa kiasi kikubwa sheria zake za masuala ya faragha ili
kuwapa wateja wake udhibiti zaidi juu ya namna kampuni zitakavyopaswa kutumia
data zao binafsi na kuzitanuwa haki hizo kuweza kuwafikia raia wa Ulaya na hata
kuwapa haki ya kuzishtaki kampuni za Marekani katika mahakama za Marekani.
Ulaya imekuwa ikishinikiza madai hayo
kwa muda mrefu lakini tokea mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa
la Marekani, NSA, Edward Snowden, alipoanza kufichuwa habari za kushangaza za
upelelezi unaofanywa na Marekani barani Ulaya, madai yao yamezidi kupata hoja.
Google na Yahoo zadukizwa
Kashfa ya upelelezi wa shirika hilo
la usalama wa taifa la Marekani, NSA, inazidi kutapakaa baada ya kubainika
kwamba imekuwa ikidukiza mawasiliano makuu yenye kuunganisha vituo vya data vya
kampuni za mitandao za Yahoo na Google duniani kote.
Gazeti la Washington Post limeripoti
hapo jana kwamba taarifa za siri za tarehe 9 Januari mwaka 2013 zimedokeza
kwamba NSA imekuwa ikituma rekodi za mamilioni ya mawasiliano kila siku kutoka
mitandao ya ndani ya Yahoo na Google kwenda kwenye ghala ya data katika makao
makuu ya shirika hilo yaliyoko Fort Meade, Maryland mjini Washington, Marekani.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la
Washington Post katika kipindi cha siku 30 zilizopita wakusanyaji wa data
wameshughulikia na kutuma zaidi ya rekodi mpya za mawasiliano 180 milioni
kuanzia za "metadata" ambazo zingelidokeza nani aliyetuma baruwa pepe
na wakati gani na maudhui yake yawe katika maandishi, sauti na video.
Kufichuliwa kwa taarifa hizo
kumepokelewa kwa ghadhabu na kampuni ya Google na kuzusha masuala ya kisheria
ikiwa ni pamoja na iwapo shirika hilo la NSA yumkini likawa linakiuka sheria za
nchi taifa kuhusu udukuzi wa mawasiliano.
Mwandishi:Mohamed Dahman/AP
Mhariri:Josephat Charo
No comments:
Post a Comment