na Salehe Mohamed, Dodoma
UTARATIBU wa mawaziri kuwa wabunge
jana ulionesha udhaifu wake baada ya kusababisha mvutano mkubwa bungeni kati ya
Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (CHADEMA), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Mvutano huo ulitokea baada ya Abwao
anayetoka Mkoa wa Iringa kuuliza swali la uhaba wa maji katika Jimbo la Isimani
linaloongozwa na Lukuvi.
Abwao alilielekeza swali hilo kwa
Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), akitaka kufahamu ni lini vijiji vilivyomo
katika Jimbo la Isimani vitapata huduma ya maji safi na salama.
Wakati akiuliza swali hilo wabunge
kadhaa walikuwa wakipiga makofi kumshangilia, hali iliyomfanya Spika wa Bunge,
Anne Makinda, kumtaka aliulize tena, kwa madai kuwa hakulisikia.
Mbunge huyo alilazimika kulirudia
swali hilo ambalo lilijibiwa na Waziri Stephen Wassira, ambaye alisema tatizo
hilo si la Isimani pekee bali ni la nchi nzima na kwamba serikali itahakikisha
vijiji vyote vinapata maji.
Baada ya Wassira kutoa jibu hilo,
Lukuvi alisimama kushibisha majibu ya waziri mwenzake, lakini baadhi ya wabunge
walikuwa wakipiga kelele kupinga uamuzi wake huo.
Licha ya kelele hizo, Spika alimpa
nafasi ya kuzungumza, akimtaka azungumze kama mbunge lakini Lukuvi alisema
angelizungumza kwa kofia ya uwaziri.
“Mimi ni waziri, ninaweza kuzungumzia
jambo la wizara yoyote ile, hivyo hawa wenzangu wanaona nimekiuka kanuni,
wanakosea, nataka waelewe vizuri mambo haya,” alisema.
Lukuvi alisema serikali inafahamu tatizo
la maji la jimbo hilo na inatekeleza mradi wa sh bilioni tatu huku mbunge wake
(yeye) akishiriki kikamilifu kutafutia ufumbuzi.
Alibainisha kuwa tayari vimekwisha
kuchimbwa visima 25 vya maji kwa jitihada zake binasfi na mpango mwingine wa
kuchimba visima vingine 10 unaendelea.
“Mipango hii yote ikikamilika kila
kijiji kitakuwa na uhakika wa maji pamoja na kuwa na kisima kimoja cha akiba,”
alisema.
Majibu hayo ya Lukuvi yalizusha
vifijo na kuzomeana ndani ya Bunge kulikokwenda sambamba na kurushiana maneno
baina ya wanaomuunga mkono na wale wa Abwao, ambao walidai kuwa ana masilahi na
Jimbo la Isimani.
Mara baada ya Lukuvi kumaliza kutoa
ufafanuzi wake huo, Makinda alisema kuwa kila mbunge ana haki ya kutoa maelezo
juu ya jimbo lake anapoona kuna mwenzake kalizungumzia.
Hata hivyo, Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika (CHADEMA), alisimama na kuomba mwongozo kuhusiana na hatua hiyo ya
Lukuvi kutumia kofia mbili kujibu swali ambalo hakuulizwa.
Akitumia kanuni ya 68 (7), Mnyika
alihoji sababu ya Lukuvi kusimama na kutumia mamlaka ya ubunge kujibu hoja hiyo
wakati yupo kwa ajili ya nafasi ya uwaziri.
“Nimesimama kwa kanuni ya 68 (7),
wakati wa kipindi cha maswali alisimama Mheshimiwa Lukuvi kujibu swali la
Mheshimiwa Abwao, lakini alijibu akitumia cheo chake cha ubunge, wakati kanuni
ya 39 (1) inatoa ruhusa kwa waziri kujibu maswali na hoja za wabunge na si
wabunge.
“Kanuni ya wabunge kujibu maswali
inahusu wabunge walioulizwa na walioteuliwa kwa kazi maalumu, kilichotokea leo
inaonyesha wazi kuwa mchanganyiko wa vyeo unaleta madhara, waziri atakiwe
kuepuka kutumia nafasi; nilikuwa naomba mwongozo wako,” alisema Mnyika.
Katika mwongozo wake, Makinda alisema
Lukuvi yuko sahihi mpaka hapo Katiba itakapotenganisha kofia ya ubunge na
uwaziri.
Utoro wa mawaziri
Katika hatua nyingine, kumejitokeza
tukio la kushangaza la mawaziri wengi kutokuonekana bungeni wakati wa mjadala
wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015, hatua iliyowafanya
wabunge wakiongozwa na Spika Anne Makinda kuwashambulia kwa utoro.
Juzi jioni wakati akiahirisha mjadala
huo, Makinda aliwaonya baadhi ya mawaziri kuwa kutokuwapo kwao bungeni
kutaiathiri serikali katika kujibu hoja za wabunge.
“Nyinyi mawaziri msidhani huu mjadala
na mpango huu unamhusu Waziri Wassira peke yake…hapana, huu unahusu wizara
zote, maana litaulizwa swali ambalo Wassira hana jibu lake, lazima muwepo,”
alisema.
Licha ya onyo hilo, jana hali ilikuwa
mbaya zaidi ambapo mawaziri na manaibu waliokuwapo ndani ya ukumbi idadi yao
ilikuwa haizidi saba wakati baraza zima wako zaidi ya 50.
Kutokana na utoro huo, wabunge wengi
waliochangia mjadala walisema utoro huo umesababisha kutowajibika ipasavyo,
hivyo maendeleo kusuasua.
Waliongeza kuwa utoro huo
unadhihirisha dharau walizonazo na kwamba hao ndio kikwazo cha mipango mizuri
inayoandaliwa na serikali.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), alisema serikali inaonesha ina mchoko mkubwa ndiyo maana
mawaziri waliomo ndani ya Bunge wakifuatilia mjadala huo hawazidi wanne.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa,
alisema haoni kama mpango huo utafanikiwa kwa kuwa wasimamizi na watekelezaji
wa mpango huo hawapo bungeni.
Kombo Hamis Kombo (CUF), alisema
mawaziri na manaibu wao wanafanya mchezo wa kuigiza katika mambo muhimu kwa
taifa, badala ya kuweka mkazo kwenye kusikiliza mapendekezo ya wabunge kuhusu
Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Kutokana na mashambulizi hayo, Waziri
asiye na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliwakingia kifua mawaziri na
manaibu wao akisema wanafuatilia mijadala hiyo kupitia runinga.
Aliongeza kuwa kutokuwapo kwao na
watendaji wengine bungeni si kikwazo cha utekelezaji wa mpango huo, kwa kuwa
serikali inafanya kazi kwa njia mbalimbali, ikiwamo hiyo ya runinga.
Waziri huyo alisema kila kinachosemwa
bungeni kinaandikwa na maofisa wa serikali ambao hukifikisha katika ngazi
husika kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment