Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo amesema ataunda serikali ya umoja wa kitaifa hivi
karibuni kufuatana na mapendekezo yaliyotolewa na mkutano wa kitaifa
ulomalizika Oktoba 5 2013.
Katika hotuba nadra aliyotowa mbele
ya mabaraza mawili ya bunge siku ya Jumatano kiongozi huyo alisema
"serikali hiyo itakuwa na wajumbe wa mungano wa vyama tawala, upinzani na
mashirika ya kiraia kwa lengo la kudumisha amani na utawala wa kitaifa kote
nchini pamoja na kuimarisha umoja, kuikarabati nchi, na kukamilisha utaratibu
wa madaraka mikowani.
Baadhi ya vyama vya upinzani
vinapinga wazo hilo la serikali ya umoja wa kitaifa, vyama hivyo vinaeleza
kwamba havijahusishwa kikamilifu katika mazungumzo ya kitaifa na serikali
haiwezi kufanikiwa bila ya kiongozi hyo kukutana na viongozi wakuu wa upinzani.
Mbunge wa Uvira na kiongozi wa chama
cha upinzani cha UNC Justin Bitakwira, Biwanahai, ameiambia Sauti ya Amerika
kwamba ili upatanishi na maridhiano yaweze kukamilika ni lazima kwa Bw. Kabila
kuzungumza kwanza na Bw. Etienne Tshisekedi na Bw. Vitale Kamerhe, viongozi
wawili aliyewashinda katika uchaguzi mkuu ulopita ulokuwa na utata.
Viongozi hao wawili walisuisia pia
mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais Kabila.
Akizungumzia suala la mazungumzo ya
Kampala kati ya serikali na kundi la M23, Rais Kabila amesema, mazungumzo
yamechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa na kwamba hapatakuwa na msamaha kwa
waasi walotenda uhalifu wa kuchukiza na wapiganaji hawatoandikishwa katika
jeshi la Taifa.
Mwakilishi wa Marekani kwa ajili ya
Mataifa ya Maziwa Makuu Russ Feingold alisema mjini Kinshasa siku ya Jumatano
kamba serikali ya Washington inaunga mkono msimamo wa Kinshasa na kwamba
mazungumzo ya Kampala yanabidi kupelekea kuvunjwa kwa kundi la M23.
Hata hivyo msemaji wa M23 Amani
Kabasha, ameiambia Sauti ya Amerika kwamba kundi lake limeshtushwa na tangazo
hilo la Kabila, na kutowa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia ili mazungumzo
yaweze kumalizika na amani kupatikana huko Kongo. Chanzo: voaswahili
No comments:
Post a Comment