Wanajeshi wawili nchini Kenya
wamefutwa kazi na kufungwa jela kwa kitendo cha uporaji waliofanya wakati wa
shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Westgate mwezi jana. Hii ni kwa mujibu
wa mkuu wa jeshi Julius Karangi.
Karangi alisema kuwa mwanajeshi wa
tatu aliyeshukiwa kwa uporaji anachunguzwa.
Awali Karangi alikanusha kuwa wanjeshi
walifanya uporaji baada ya kutokea picha za CCT zikionyesha wanajeshi wakibeba
mifuko ya plastiki ya moja ya maduka makubwa yaliyokuwa ndani ya jengo la
Westgate.
Wanamgambo wa Somalia, al-Shabaab
walikiri kufanya shambulizi hilo ambapo waliteka nyara wakenya kadhaa waliokuwa
ndani ya jengo hilo kwa siku nne.
Watu 67 walifariki na mamia ya
wengine kujeruhiwa.
Wakati huohuo, mkuu wa kitengo cha
uchunguzi wa uhalifu katika idara ya polisi,Ndegwa Muhoro alisema kuwa mmoja wa
magaidi waliokuwa ndani ya jengo hilo walipiga simu nchini Norway wakati
walipovamia jengo hilo.
Mmoja wa washukiwa wa shambulizi hilo
ametajwa kuwa Hassan Abdi Dhuhulow mzaliwa wa Somalia ingawa raia wa Norway.
Jeshi limesema kuwa magaidi wote
wanne waliofanya shambulizi hilo waliuawa.
Lakini katika ripoti za awali,
iliarifiwa kuwa washambuliaji walikuwa kati ya kumi na kumi na watano.
Bwana Muhoro alisema kuwa watu
wengine watano wamezuiliwa kwa uchunguzi zaidi na kuwa watafikishwa mahakamani
hivi karibuni.
Chanzo: BBCSwahili
No comments:
Post a Comment