Shadrack Willced Mongi maarufu
‘Sheddy Clever’ ndiye prodyuza wa studio hii iliyotengeneza wimbo wa ‘My Number
One’ unaomilikiwa na mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’, wimbo uliofanya vizuri
katika levo za kimataifa.
Na Herieth
Makwetta, Mwananchi
Ukiingia ndani ya studio ya Burn
Records iliyopo Tabata, jijini Dar es Salaam, huwezi kuamini kama ndiyo sehemu
‘zinakopikwa’ kazi za baadhi ya wasanii zinazowafanya kuwa maarufu na
kuwaingizia kipato, kupitia shoo na mialiko ya ndani na nje ya nchi.
Studio hii iliyopo maeneo ya
‘uswahili’ imezingirwa na nyumba nyingi kiasi cha kushindwa kuijua njia kwa
uharaka zaidi pale mtu anapotaka kufika kwa prodyuza huyo. Studio hii ni ndogo
yenye vifaa vichache tu vya kimuziki lakini yenye prodyuza makini na mwenye kipaji.
Shadrack Willced Mongi maarufu
‘Sheddy Clever’ ndiye prodyuza wa studio hii iliyotengeneza wimbo wa ‘My Number
One’ unaomilikiwa na mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’, wimbo uliofanya vizuri
katika levo za kimataifa.
Hata hivyo sehemu ya mahojiano na
mwandishi wa Starehe ni kama ifuatavyo;
Swali: Mbona Studio yako ipo uchochoroni
hivi?
Jibu: Unasema uchochoroni! Wasanii
wengi wamekuja hapa na wanatumia muda mwingi kuwepo ndani ya studio hii huku
wakitumia vyakula vya hukuhuku kwetu uswahili, si jambo la ajabu. Lakini ni
mazoea tu kwetu tunaona sawa na kwa upande wangu inanipa hamasa kwani najisikia
huru kufanya kazi nikiwa maeneo haya.
Swali: Ndiyo kusema Diamond alikuja
kurekodi kwenye studio hii?
Jibu: Ndiyo alikuja kurekodi katika studio
hii na alikuwa akikaa hapa kutwa nzima. Yule jamaa anafanya kazi sijawahi ona
kutoka kwa wasanii wengine akija hapa anatumia muda mwingi kujenga mashairi,
hata hivyo anatumia akili kubwa sana katika kufanya kazi si sawa na vile watu
wanamwona. Korasi ya wimbo wa My Number One tulitumia zaidi ya saa 12
kuitengeneza na saa nyingine 12 kuirekebisha, yupo makini sana. Ilichukua miezi
sita kukamilika.
Swali: Ilikuwaje akapajua hapa?
Jibu: Diamond alinitafuta yeye mwenyewe,
ilikuwa saa mbili asubuhi akanipigia na kunifahamisha jina lake akasema
anakuja, kwa kuwa namba niliyokuwa nayo alishaacha kuitumia nilidhani si yeye
lakini baada ya muda nikashangaa amefika. Alinitaka nimsikilizishe midundo nami
nilifanya hivyo hatimaye akapenda mmoja wapo, basi tulipeana mikakati kazi
ikafanyika.
Swali: Kazi uliyoifanya imeweza kumwingizia
kitita kikubwa cha pesa mwanamuziki huyo vipi kwa upande wako inakuneemesha
vipi?
Jibu: Hapana nilimfanyia kazi akanilipa
ujira wangu mzuri tu, hivyo huko mbele ni kazi yake. Lakini katika upande wa
hatimiliki hivi sasa tupo mbioni kuhakikisha chama chetu cha maprodyuza
cha Tanzania TSPA kinasajiliwa ili kuweza kutetea kazi zetu na hatimiliki.
Swali: Umechukua hatua gani kwa prodyuza
aliyechukua biti ya wimbo wako na kuichakachua kwa kutengeneza kazi feki?
Jibu: Huyo mtu namtafuta sana tena sana,
sijapata tu mahala anapofanyia kazi.
Swali: Tuambie uhalisia wa kazi zako
ulianzia wapi?
Jibu: Nilianza mwaka 2005, nikiwa mkoani
Tabora katika studio za rafiki zangu. Lakini studio yangu ya kwanza ilikuwa ni
pale Student Center kulikuwa na mzungu mmoja aliitwa Father Clombi ndiye
aliyekuwa mmiliki. Nikiwa huko nimepata kutengeneza vibao kadhaa vilivyofanya
vizuri katika redio mbalimbali mkoani hapo. Niliamua kuondoka huko mwaka 2008 wakati
huo nilikuwa nimeshapata jina kidogo. Nilifika jijini na kuanzisha studio pale
Liwiti. Mtu aliyenisaidia sana ni Mbishi Real na kunipa uzoefu mkubwa katika
kazi hii baadaye nikahama na kufika hapa Da West.
Swali: Kazi yako ya kwanza kabisa kuitoa na
ikafanya vizuri ilikuwa ipi?
Jibu: Nivute Kwako wa Dayna
aliyomshirikisha Barnabas. Wimbo huu ulinitambulisha katika ramani ya muziki wa
kizazi kipya, tangu hapo walianza kumiminika wasanii maarufu wakitaka
niwatengenezee kazi.
Swali: Ni kazi zipi maarufu ulishawahi
kuzifanya?
Jibu: My Number One wa Diamond, Marry Me
wa Rich Mavoko, Zilipendwa wa Matonya, Yatakwisha wa Ben Pol ft Linah, Mtoto
Amekuwa wa Pasha, Swaga wa PNC na Ney wa Mitego na nyingine nyingi tu.
Swali: Una mikakati ya kuhama eneo hili na
vipi kuhusu vifaa vya kisasa?
Jibu: Ninamalizia kujenga nyumba yangu
huko Kinyerezi, hivyo nikimaliza tu studio yangu itakuwa nyumbani kwangu na
huko ndiko nitafunga vifaa vya kisasa tofauti na hapa.
Swali: Unafanya shughuli gani tofauti na
kazi yako ya utayarishaji wa muziki? Umepata faida gani kutokana na kazi yako?
Jibu: Mimi ni mjasiriamali nina duka
linalouza CD, nina banda linaloendesha shughuli za michezo ya tv kwa watoto,
bodaboda na vinginevyo. Nimeweza kujenga nyumba yangu mwenyewe, namiliki gari
langu binafsi, nimekuwa na marafiki wengi na kujuana na watu mashuhuri kupitia
kazi yangu.
Swali: Umeoa au una mchumba?
Jibu: Sijaoa bado ila nipo njiani
kuelekea huko. Kifupi naogopa sana wasichana kwani nina rafiki wa kike ambaye
hata hivyo kutokana na kutendwa na wengi bado naendelea kumchunguza.
Amakweli
ukifanya kazi vizuri watu watakujua tu.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment