na Waandishi wetu
MBIO
za urais wa mwaka 2015 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinazidi kuchukua
sura mpya baada ya kundi linalodaiwa kumuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu,
Edward Lowassa, kumeguka huku baadhi ya washirika wake wa Kanda ya Ziwa
wakimwibua William Ngeleja.
Ngeleja
ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ni mmoja wa wanasiasa vijana wanaotajwa
kuwa wafuasi wa kundi la Lowassa, jambo ambalo linazua hofu kuwa huenda kambi
hiyo ikatikisika ikiwa juhudi hizo zitafanikiwa.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa vigogo kadhaa waandamizi wa CCM wakiwemo wabunge na
mawaziri kutoka Kanda ya Ziwa ambao ni wafuasi wa kundi la Lowassa, wameingia
kwenye msuguano wakitaka mgombea urais 2015 atoke kanda hiyo.
Chanzo
chetu, kinaeleza kuwa msigano huo ulizua mtafaruku huku baadhi ya wajumbe
wakidai kanda hiyo tayari ilikwishampata Rais Julius Nyerere ambaye aliongoza
Serikali ya Awamu ya Kwanza na wengine wakisisitiza kuwa ni lazima rais ajaye
atoke kanda hiyo.
“Ni
katika mikakati mizito hiyo, wajumbe walimpendekeza Ngeleja kuwa mpeperusha
bendera hiyo, ingawa yuko na waziri mmoja ambaye anaonekana anatamani nafasi
hiyo,” kilisema chanzo chetu.
Ngeleja
ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, anatajwa kuhudhuria kikao cha siri
kilichofanyika eneo la Nyegezi jijini Mwanza hivi karibuni, ambako mjadala
mkubwa uliongozwa na wazee maarufu wa Kanda ya Ziwa ukimtaka akubali kuomba
kuwa mgombea wa CCM.
Mikakati
ya kumwandaa mbunge huyo, inaelezwa kuwa imeanza kwa kumwandalia hafla
mbalimbali za kushiriki harambee kwenye nyumba za ibada kama wanavyofanya
baadhi ya makada maarufu wa CCM wanaotajwa kuutaka urais, akiwemo Lowassa
mwenyewe.
Hata
hivyo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, Ngeleja alisema huu sio muda muafaka
kwake kuzungumzia kama atagombea urais au hapana.
Akijibu
swali hilo muda mfupi baada ya kumaliza kuhutubia mahafali ya tatu ya kidato
cha nne katika Shule ya Sekondari Lilian, jijini Dar es Salaam juzi ambako
alikuwa mgeni rasmi, Ngeleja alisema: “Kuhusu suala la urais bado ni mapema
sana kulisemea, kuna taratibu, maadili na kanuni za chama. Tusubiri muda
ukifika tutajua nini cha kusema, sijaanza mbio zozote za kuwania nafasi hiyo
kubwa.
“Mimi
bado nina wajibu wa kuwatumikia wananchi wangu wa Sengerema kama mwakilishi
wao, bado nina wajibu wa kutekeleza kazi za kibunge, hivyo kwa sasa kuzungumzia
suala la urais bado ni mapema sana.
“Ni
kinyume cha kanuni na maadili ya CCM, wakati ukifika kanuni zipo wazi, na
maadili yanajulikana kwa wanachama wote, tutajua wakati huo, ndiyo tutasema
kama tunagombea au la, ila kuanza kulisemea sasa ni kujiongezea majukumu ambayo
hayana tija kwa sasa,” alisema Ngeleja.
Wachambuzi
wa siasa wanasema kuwa endapo kundi hilo litashikilia msimamo wake wa kumpigia
debe Ngeleja, litakuwa limedhohofisha nguvu ya Lowassa Kanda ya Ziwa, kwani
eneo hilo ni muhimu kutokana na wingi wa kura.
Majina
mengi ya vigogo wa CCM yanatajwa kugombea nafasi hiyo nyeti, huku msukumo
mkubwa ukiwa upande wa Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Benard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya
na Spika aliyepita, Samuel Sitta.
Duru
za siasa zinadokeza kuwa kundi la Membe linafanya kila jahudi ili kumshawishi
Sitta asigombee waweze kuunda nguvu ya pamoja kwa kuwashirikisha pia Prof.
Mwandosya, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi, Dk.
John Magufuli.
Mei
26 mwaka huu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa,
alisisitiza kwamba chama kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote
anayejipitisha katika maeneo mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais
kabla ya wakati.
Makundi
hayo, yameleta hofu ya rushwa ndani ya chama, hatua ambayo Mwenyekiti wake,
Rais Jakaya Kikwete ameikemea vikali akisema inaweza kuikosesha CCM ushindi
mwaka 2015.
Akifunga
mafunzo ya makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma juzi, Rais
Kikwete alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza
kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe
ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama ubunge.
Alisema
kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi
kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo
linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.
“Kama
hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu
sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020
hatutarudi tena madarakani.
“Najua
rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh laki mbili za ‘airtime’ (muda wa
mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,”
alisema.
Alisema
tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali
ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi
wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu, nawaombeni
tubadilike. Kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi
mbalimbali, nawaambieni,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment