Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro,
wamemlalamikia Mbunge wa Kilombero, Abdallah Mteketa, kwa madai ya kutoshiriki
kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani ya chama hicho jimboni kwake.
Aidha, wajumbe hao wamedai kuwa
mbunge huyo anafanya kazi zake za ubunge kwa chini ya asilimia 40 tu.
Walitoa kauli hiyo juzi baada ya
kukutana na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Morogoro ambapo baadhi yao walidai
mbunge huyo kutoonekana jimboni na kushindwa kushiriki vikao vya baraza la
madiwani.
Walisema kitendo hicho kinawafanya
wananchi kukilalamikia chama hicho kwa kukosa uwakilishi.
Walidai kuwa mbunge huyo amekuwa
akiwaweka viongozi wa wilaya hiyo katika wakati mgumu kutokana na kushindwa
kujibu maswali wanayoulizwa na wananchi wake juu ya kero mbalimbali, wakati
kazi kubwa ya mbunge ni kuchukua kero za wananchi na za kijamii na
kuziwasilisha bungeni zitafutiwe ufumbuzi.
Alipoulizwa kuhusiana na malalamiko
hayo, Mteketa alidai kuwa viongozi wa wilaya hiyo ndiyo wamekuwa chanzo cha
kukwamisha utendaji wa kazi zake kutokana na kutompa ushirikiano pale
anapohitaji kutekeleza masuala ya kisiasa.
Aidha, alidai kuwa hata anapoomba
ushirikiano wao kwenda kwenye shughuli za wananchi, hudai hawana nafasi huku
akitaja sababu nyingine kuwa ni kuuguliwa na mkewe aliyepooza.
Aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa
wilaya hiyo akiwamo Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho wilaya, kwamba
hawakumtaka hata wakati alipokuwa akiwania nafasi hiyo ya ubunge.
Hali kadhalika, alisema bado
wameendeleza makundi yaliyotokana na uchaguzi baada ya kushinda na badala yake
wamekuwa wakitengeneza wabunge wao watarajiwa kinyume na utaratibu wa CCM.
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro,
Rodgers Romuli, alithibitisha kupokea malalamiko hayo, ingawa jukumu lao kama
chama ni kumwita na kumwambia yaliyojitokeza ili ayafanyie kazi kwa manufaa ya
chama hicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment