Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi,
imeelezwa kuwa marubani wa ndege ya kijeshi ya Qatar, walitumika katika
kutorosha twiga wanne kwenda Uarabuni na kwamba washtakiwa walikuwa na hati za
kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia.
Shahidi wa 13, Prisca Sabugo ambaye
ni Ofisa Uhamiaji, aliiambia mahakama juzi kuwa hati hizo hazikugongwa mihuri
wala kupewa viza.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, shahidi huyo alidai kuwa
ndege hiyo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia)
Novemba 24 mwaka 2011.
"Baada ya hiyo ndege ya jeshi
kutua, alikuja wakala wao kutoka Kampuni ya Equity Aviation akaniletea
Diplomatic Passport zao na akaniambia wamekuja kwa shughuli za utalii kwa siku
tatu," alisema.
Huku akiongozwa na mawakili wa
Serikali, Evetha Mushi na Joseph Maugo, shahidi huyo alidai kuwa marubani na
wafanyakazi wa ndege huwa hawapitii utaratibu wa kawaida wa kujaza fomu na
kupewa viza. Alisema, tangu wageni hao waingie nchini kama watalii, hawakuwahi
kuhojiwa na chombo chochote kuhusu kutogongwa mihuri kwenye hati zao.
Shahidi wa 12, Oscar Jullius ambaye
ni Ofisa Wanyamapori, alidai kuwa vibali vilivyotumika kukamata wanyama hao
vilikuwa vya kampuni mbili ambazo ni Ham Market na Luega Birds Traders.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, vibali
hivyo vilikuwa vya kumiliki nyara na si vya kukamata wanyamapori hai na kwamba
yeye ndiye aliyeandika ripoti ya thamani ya wanyama hao.
Alisema thamani ya wanyama wote
waliotoroshwa ilikuwa ni Sh170.5 milioni na kwamba twiga hao wanne kila mmoja
alikuwa na thamani ya Dola 10,000 za Marekani sawa Sh60 milioni za Tanzania.
Alipoulizwa na mmoja wa mawakili
wanaowatetea washtakiwa, Edmund Ngemela, kama vibali walivyokuwa navyo vilikuwa
halali, alikiri kuwa vilikuwa halali na vilikuwa ni vya kumiliki nyara.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea Novemba
29 mwaka huu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja
na raia wa Pakistan, Kamran Ahmed, Hawa Mang'unyuka, Martin Kimath na Michael
Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.
Katika hatua nyingine, madiwani
watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwamo mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, wanashikiliwa na maofisa wa Kikosi cha Maalumu cha Kupambana na ujangili.
Huko Dodoma, watu sita wamekamatwa na
polisi wilayani Kondoa baada ya kupatikana na vipande vinane vya meno ya ndovu
yenye thamani ya Sh 25milioni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma
Suzan Kaganda, aliwambia waandishi wa habari jana kuwa, watuhumiwa hao
walikamatwa katika operesheni maalum ya kupambana na ujangili.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment