Njombe. Wananchi wa Kijiji cha Makoga Wilaya
ya Wanging’ombe mkoani Njombe jana walisimamisha msafara wa Rais Jakaya Kikwete
na kumweleza kero zao mbalimbali ikiwamo ya kutaka gari la kubebea wagonjwa
(ambulance) kwa ajili ya zahanati ya kijiji hicho.
Wananchi hao walifurika saa nne
asubuhi kandokando ya barabara na kuomba msafara wa Rais Kikwete usimame.
Msafara wa Rais Kikwete ulikuwa
unatokea Makete kuelekea Njombe na ndiyo ukakutana na wananchi hao waliokuwa na
shauku ya kueleza matatizo hayo kwa Rais.
Rais Kikwete alikubali kushuka na
ndipo baadhi ya wananchi mmoja mmoja wakaanza kutaja kero zinazowakabili katika
Kijiji cha Makoga.
Wananchi waliomba kuboreshwa kwa
huduma ya maji pamoja na kuwahishiwa pembejeo za kilimo.
“Mheshimiwa Rais pia tunaomba gari la
wagonjwa kwani tunapata shida sana kuwapeleka wagonjwa wetu hospitali,”
alisikika mmoja wa wananchi hao akisema.
Majibu ya Rais Kikwete
Akijibu kero hizo za wananchi, Rais
Kikwete aliwaahidi kuwa Serikali yake itatafuta fedha kwa ajili ya kuwaletea
gari la wagonjwa.
Kuhusu pembejeo za kilimo, alisema Serikali
itaangalia uwezekano wa kuongeza pembejeo za kilimo mwakani. Kuhusu maji
alisema kijiji hicho kipo kwenye mpango wa vijiji 10 vitakavyopatiwa huduma ya
maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe katika bajeti ya mwaka
2013/14.
Pia Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, George Simbachawene alisema kijiji kipo kwenye mpango wa kuletewa umeme
hivi karibuni.
Ahimiza tohara
Pia Rais Kikwete aliwataka wanaume
nchini kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata tohara kama moja ya njia za
kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi.
Akisalimia wananchi katika Kijiji cha
Kipengele kilichoko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, ambako
anaendelea na ziara yake kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, Rais pia
amewapongeza wanaume ambao mpaka sasa wamejitokeza kupata tohara ili
kukabiliana na ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete
alizindua Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) katika Wilaya ya Makete ikiwa ni
chuo cha kwanza katika mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na
chuo cha ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanapata fursa
kujifunza ujuzi mbalimbali.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo
hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Zebedayo Mushi alisema chuo hicho kimejengwa
kwa ushirikiano kati ya Veta na Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment