Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara,
Julius Mtatiro akizungumza jana kukanusha taarifa za PAC kuwa hawajawasilisha
hesabu zao. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge wa
CUF, Shaweji Mketo.Picha na Silvan Kiwale.
Na Joyce Mmasi, Mwananchi
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
kinakusudia kumwandikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda
kikimwomba azielekeze kamati mbalimbali za Bunge jinsi ya kufanya kazi zao.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chake kimesikitishwa na
taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
“Chama chetu kinatafakari hatua za
kuchukua ikiwemo kumwandikia Spika ili azifundishe kamati zake namna bora ya
kufanya kazi zake kama kamati za umma.
Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia
kupitia vyombo vya habari kuwa, chama chetu ni miongoni mwa vyama kadhaa
ambavyo havijawasilisha hesabu kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha
miaka minne sasa. Tunaomba Watanzania wazipuuze taarifa hizo kutuhusu kwa
sababu hazina ukweli wowote,” alisema Mtatiro.
Wiki iliyopita, Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe
alisema licha ya kuwa vimepokea ruzuku ya jumla ya Sh67.7 bilioni kwa vyama
tisa vya siasa tangu mwaka 2009, vyama vyote vinavyopata ruzuku ya Serikali
havijawahi kupeleka ripoti yoyote ya ukaguzi wa fedha kwa CAG.
Kamati hiyo vilevile ilitangaza
kusitishwa mara moja utoaji wa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa nchini mpaka
hapo hesabu zake zitakapokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali
(CAG).
Mtatiro alisema CUF kimesikitishwa na
kufadhaishwa na hatua ya kamati kuvihukumu vyama vyote vya siasa wakati jambo
hili ni la chama kimoja kimoja.
“Mbaya zaidi ni pale ambapo
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto amekuwa akishinda kwenye mitandao ya
kijamii akishupalia kuvichukulia hatua vyama – kikiwemo chama chetu, huku akiwa
hana taarifa za kina za namna tulivyotekeleza wajibu wetu,” alisema.
Alisema ni jambo la kufedhehesha kwa
kamati ya Bunge kushinda kwenye mitandao ya kijamii ikihukumu na kutoa taarifa
za uongo kwa umma bila hata kuwasiliana na vyama vya siasa na kumwomba Spika
azipe mwongozo kamati hizo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment