“Mipango ya tume ni kukamilisha kazi hii
ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Sura ya 83.”
Jaji Joseph Warioba
Na Editha Majura, Mwananchi
Ikiwa maombi hayo ya Tume
yatakubaliwa ina maana watatakiwa kukabidhi ripoti yake Desemba 1, mwaka huu.
Dar es Salaam. Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba
kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni
yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph
Warioba ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18 kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba.
Maana yake ni kuwa Tume hiyo
iliyoanza kazi Mei 1, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba
1, mwaka huu.
Ikiwa maombi hayo ya Tume
yatakubaliwa ina maana watatakiwa kukabidhi ripoti yake Desemba 1, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Augustine Ramadhan aliliambia gazeti hili kwa simu jana kuwa wamepeleka
serikalini maombi ya kuongezewa muda wa kufanya kazi.
Hata hivyo, Jaji Ramadhan alisema
kuwa wameomba muda zaidi kutokana na kukabiliwa na kazi kubwa ya kuchambua
maoni hayo.
Alisema hakuwa na taarifa ya majibu
ya kama ombi lao limekubaliwa au la.
“Hatukuomba miezi miwili kama sheria
inavyotuelekeza, tumeomba mwezi mmoja na mpaka Ijumaa nilipotoka ofisini sikuwa
na taarifa kama kibali kilikuwa kimetolewa, labda kesho (leo) nikienda ofisini
nitafuatilia kufahamu kama kimetoka,” alisema Jaji Ramadhan.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo,
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alikiri kuwa tume hiyo imeomba
kuongezewa muda.
“Ni kweli barua ya Tume imeletwa,
tumeipokea na inafanyiwa kazi,” alisema Rweyemamu kwa kifupi.
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias
Chikawe akizungumza kwa njia ya simu; baada ya kuulizwa ikiwa Serikali imetoa
kibali hicho au la alisema, “Sizungumzi na waandishi leo.” Simu ikakatika.
Ahadi ya Warioba yashindwa
kutekelezeka
Hatua hiyo inatofautiana na ahadi ya
Jaji Warioba, ambaye mara nyingi amekuwa akisisitiza kuwa tume yake itamaliza
kazi yake katika muda uliopangwa.
Jaji Warioba alitoa ahadi hiyo kwa
mara ya mwisho wakati akizungumza na vyombo vya habari Septemba 26, mwaka huu.
“Mipango ya tume ni kukamilisha
kazi hii ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Sura
ya 83,” alieleza Jaji Warioba wakati huo.
Tume imefuata sheria
Tume imeomba kuongezewa muda kama
inavyoelekezwa kwenye kifungu cha kidogo cha (4) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
“Endapo Tume itashindwa kukamilisha
kazi yake ndani ya kipindi kilichoelezwa katika kifungu kidogo cha (3), Rais
kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar, anaweza kuongeza muda usiozidi miezi
miwili ili kuiwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti,” kinaeleza
kifungu kidogo hicho.
Bunge la Katiba na Kura ya Maoni sasa
kuchelewa
Kutokana na ombi hilo la tume, maana
yake sasa mkutano wa Bunge la Katiba utasogezwa mbele.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ilitakiwa kukabidhi kazi yake Novemba 1, lakini kwa kuomba muda ina maana
wataathiri ratiba ya mkutano wa Bunge la Katiba.
Bunge la Katiba lilitakiwa kukutana
katikati ya mwezi Novemba kujadili Rasimu ya pili ya Katiba baada ya
kuwasilishwa na tume.
Maana yake sasa Bunge la Katiba kuna
uwezekano mkubwa likakutana mwakani au Desemba mwishoni.
Pia suala hilo litaathiri mpangilio wa
kura ya maoni, ambayo inatakiwa kuitishwa baada ya Bunge la Katiba kupitisha
rasimu.
Ombi hilo kwa kiasi kikubwa linaweza
kuathiri mchakato wa kupata Katiba ya Tanzania Bara ikiwa Katiba ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Serikali tatu itapitishwa na wananchi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment