Monday, October 21, 2013

Wajumbe wa UN wataka mazungmzo ya amani ya DRC yapige hatua



Umoja wa Mataifa umeshinikiza paweko hatua ya maendeleo katika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya DRC na waasi yanayofanyika mjini Kampala Uganda, huku kukiwa na dalili mazungumzo hayo yanaelekea kushindwa.

Wajumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wanaofuatilia mazungumzo hayo wameelezeawasiwasi wao kuwa katika mazungumzo hayo kunakosekana mpango wa kulisambaratisha kundi la waasi la M23 wanaopigana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wajumbe hao wametoa taarifa ya pamoja inayotaka papigwe hatua katika siku chache zijazo ambapo mazungumzo hayo yanafanyika tena.
Raia wa Congo wanaokimbia mapigano Raia wa Congo wanaokimbia mapigano

Hata hivyo wajumbe hao pia wameonya dhidi ya hatua za kichokozi katika mazungumzo na kutaka kila pande kuhakikisha mazungumzo hayo yanaendelea kwa amani.

Kwa upande wake afisa wa serikali ya DRC amesema mazungumzo yanaendelea kwa upole lakini akakiri huenda yakawa yanaelekea katika mkwamo.

Afisa huyo moja kwa moja amewashutumu waasi wa M23 ambao awali walisema mazungumzo yanapiga hatua kuwa wanatoa maamrisho mapya kila wakati huku serikali ikiendelea kurithia lakini mkwamo mkubwa wa mazungumzo hayo yalioanza tena mwezi Septemba kufuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Afrika ni suala la kutoa kinga kwa waasi na kuwajumuisha katika jeshi la serikali.

Waasi wa M23 watakiwa kuweka silaha zao chini

Huku hayo yakiarifiwa wajumbe wa Umoja wa Mataifa sasa wamewataka waasi wa M23 kuachana na ghasia za aina yoyote na wanachama wote wa kundi hilo kuweka silaha zao chini wakizingazia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 2098 linalowataka kufanya hivyo.

Kwa sasa waasi hao wanadhibiti eneo lililo na ukubwa wa kilomita 700 mashariki mwa nchi hiyo ilio na utajiri wa madini katika eneo hilo la Mashariki linalopakana na Uganda na Rwanda.
Wanajeshi wa kundi la waasi wa M23 Wanajeshi wa kundi la waasi wa M23

M23 ilianzishwa na waasi wa kitutsi waliojumuishwa katika jeshi la jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo chini ya mazungumzo ya amani yaliofanyika mwaka wa 2009.

Waasi hao walidai kuwa matakwa yao hayakuridhiwa katika mazungumzo hayo na kuanza tena uasi mwezi Aprili mwaka wa 2012. Katika uasi wa hivi karibuni Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Uganda na Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi jambo ambalo nchi hizo zimekanusha vikali.

Hata hivyo waasi wanaonekana kuwa na mtazamo tofauti juu ya mazungmzo hayo. Siku ya Jumamosi waasi walisema kwamba mazungumzo yanayofanyika nchini Uganda yanaelekea kupiga hatua kubwa kati yao na serikali ya DRC.

Kwa upande wake waziri wa mawasiliano wa Congo na pia msemaji wa serikali Lambert Mende, amesema kupigwa kwa hatua hiyo kutaonekana tu katika makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo iwapo yatatiwa saini na pande zote mbili.

Mwandishi: Amina Abuakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

No comments: