Gari
yenye namba STK 3665 likiwa ndani ya kiwanda kimoja kilichopo Mbagala, Dar es Salaam (jina
linahifadhiwa) ambapo dereva wake alikamatwa akidaiwa kutaka kumtapeli mmiliki
wa kiwanda hicho ambaye ni mteja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) juzi
jioni.
Na Mwandishi Wetu
Jeshi la
Polisi mkoani Temeke, linamshikilia dereva wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, aliyefahamika kwa jina la Bw. Samwel Mulagalazi, ambaye
anadaiwa kushirikiana na watu wawili waliotaka kumtapeli mteja wa Shirika la
Umeme nchini (TANESCO), sh. milioni 60
Tukio hilo limetokea juzi saa 11
jioni katika kiwanda kilichopo Mbagala, Dar
es Salaam (jina tunalo), ambapo matapeli (vishoka),
waliojifanya wafanyakazi wa TANESCO, Makao Makuu, Ubungo, walitaka kufanya
utapeli huo kwa mmiliki wa kiwanda hicho.
Matapeli hao walimpigia simu mmiliki wa kiwanda hicho (jina
tunalo), wakidai kiwanda chake kinaiba umeme hivyo walimtaka atoe sh. milioni
60 asiweze kukatiwa umeme.
Mmiliki huyo akitambua kuwa mita zake hazikuwa na tatizo
lolote na hahusiki na wizi huo, aliwasiliana na Meneja wa TANESCO wilayani
Temeke, Mhandisi Richard Mallamia na kumweleza vitisho alivyopewa na matapeli
hao na pesa waliyotaka kupewa.
Mhandisi
Mallamia alimtaka mteja huyo wa TANESCO, kutowakatisha tamaa matapeli hao
badala yake awapigie simu ili waende kuchukua pesa hizo.
Baada
ya kumpa ushauri huo, Mhandisi Mallamia alifanya mawasiliano na ofisi ya
shirika hilo
Idara ya Usalama na Jeshi la Polisi mkoani Temeke ili wakaweke mtego.
Akizungumza
na Majira, Mhandisi Mallamia alisema baada ya matapeli hao kupigiwa simu ili
waende kuchukua pesa walizotaka, awali walikubali lakini baadaye walimpigia
simu mteja wao na kudai wanamtuma dereva.
Bw.
Mulagalazi alifika kiwandani hapo kama dereva
aliyetumwa na matapeli hao akiwa na gari Land Cruiser Hardtop, yenye namba SKT
3665 na kuingia mtegoni (kukamatwa).
Maofisa
wa TANESCO na polisi walimtaka mmiliki wa kiwanda awapigie simu matapeli hao na
kuwajulisha tayari ametoa pesa hizo kwa dereva wao. Vishoka hao walimpigia simu
dereva na kumtaka wakutane maeneo ya Mbagala.
Polisi
na Maofisa wa TANESCO waliingia ndani ya STK ambalo lilikuwa l ikiendeshwa na
mtuhumiwa ili kwenda kuwakamata matapeli hao ambao walipaki gari lao
barabarani.
Chanzo
chetu cha habari kilidai kuwa, matapeli hao wakiwa na gari aina ya RAV 4,
waliiona STK ikiwafuata taratibu bila kujua ndani ya gari kulikuwa na Maofisa
wa TANESCO na polisi ambao walijificha ili wasionekane.
Dereva
(mtuhumiwa), alisimama, kushuka kwenye gari na kuwafuata matapeli hao
akiwaambia TANESCO wamechukua kitambulisho chake hivyo matapeli waliingia
kwenye gari na kukimbia kwa mwendo wa kasi.
Mtuhumiwa
(dereva), alirudi katika gari na polisi walimtaka warudi Kituo cha Polisi
Mbagala. Hadi jana mchana bado alikuwa akiendelea kuhojiwa.
Inadaiwa
kuwa, katika maelezo yake dereva huyo ambaye inadaiwa anamuendesha Mratibu wa
Mradi wa Kibamba, aliwataja watu waliomtuma kwa majina ya Godfrey Mjakamaarufu
'Makofia' na Modest Kayombo Thomas.
Alidai
Thomas ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambaye amejenga maeneo ya
Vikindu na Mjaka ni fundi umeme ambaye hupata tenda mbalimbali.
Katika
utetezi wake baada ya kukamatwa, inadaiwa mtuhumiwa alidai yeye hakuwa
akifahamu lolote zaidi ya kuambiwa akachukue mzigo ambao hakujua ni mzigo gani.
Taarifa
za uhakika zinasema kuwa, vishoka hao Mjaka na Thomas wana kesi Mahakama ya
Kisutu, Dar es Salaam, ambayo inaendelea kusikilizwa na itatajwa Oktoba 15
mwaka huu, wakidaiwa kujifanya wafanyakazi wa TANESCO na walikamatwa wakiwa
wamevaa sare za shirika hilo.
Chanzo
hicho kilidai watu hao walikamatwa wakifanya utapeli kwa wateja wa TANESCO eneo
la Kigamboni, Dar es Salaam.Kamanda wa Polisi mkoani humo, Engelbert Kiondo,
alisema tukio hilo
atalitolea ufafanuzi leo baada ya kupata taarifa kamili.
Mhandisi
Mallamia alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa ni matokeo ya elimu wanayoendelea
kuitoa kwa wateja wao ambao wanatumia umeme mkubwa wakiwemo wamiliki wa
viwanda, bekari za mikati, hoteli pamoja na wateja wadogo ili wawe makini
kujiepusha na matapeli wa aina hiyo.
Alisema
hivi sasa kuna mtandao mkubwa ambao unalihujumu shirika hilo kupitia wateja wake na kuchafua sifa ya
TANESCO kwenye jamii jambo ambalo haliwezi kuvumilika.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment