Na
Mwandishi Wetu
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe , leo anatarajiwa kuwa
miongoni mwa washiriki wa mjadala mpana kuhusu njia za kumaliza tatizo la ndoa
za utotoni , ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mtoto wa kike Duniani.
Mjadala huo umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), Kikundi cha Mashirika ya Umoja wa
Mataifa Tanzania
yanayoshughulikia jinsia, kwa kushirikiana na Jukwaa la Graca Machel linalopigania
hadhi ya mtoto.
Maadhimisho ya pili ya siku ya mtoto wa kike duniani nchini Tanzania yenye
kauli mbiu kuwa; "Kuwawezesha wasichana, kuhakikisha haki zao za binadamu
na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji wao ni muhimu kwa maendeleo ya familia nzima
ya wanadamu."
Tanzania ni
miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni duniani. Kwa
wastani, watoto wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka
18.
Mjadala huu unalenga kuchochea zaidi ushirikiano ulioundwa kwa ajili
ya matokeo bora kwa watoto ikiwa ni pamoja na wasichana na wavulana na hasa
uraghibishi endelevu na wa kina kuhusu suala la ndoa za utotoni na ajenda pana
kuhusu haki za wanawake na watoto.
Washiriki wengine ni pamoja na Shekhe Alhad Musa Salim, Askofu
Jacob ole Paul Mameo, Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka na
Bi.Valerie Msoka , Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake
Tanzania atakayeongoza mjadala huo na Jama Gulaid ambaye ni Mratibu Mkazi wa
Umoja wa Mataifa nchini.
Mama Graca Machel atawasalimia washiriki kwa njia ya video,
washiriki wote watakuwa na nafasi ya kuuliza maswali jopo la wazungumzaji na
pia kushiriki mjadala kwa kuchangia mada kwa kutumia utaalamu na ufahamu.
Wakati huo huo ,Grace Ndossa,anaripoti kuwa Shirika la Kimataifa
la Plan International, leo linaadhimisha siku hiyo kwa kuelimisha jamii na
kutetea haki za mtoto wa kike.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaama jana kuhusu
kampeni hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Jorgen Haldorsen, alisema
kampeni hiyo itafanyika katika viwanja vya Shule ya Benjamini Mkapa.
Alisema lengo ni kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha
maisha ya wasichana milioni nne duniani na zaidi ya wasichana 300,000 nchini
Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha
pamoja na kujikimu.
Alisema pia kuwawezesha wasichana kushiriki katika shughuli mbalimbali katika
jamii na kulindwa kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto wa
kike.
Alisema inanuia kuongeza stadi, maarifa na uelewa wa hatari zinazowakabili
watoto wa kike kutokana na ukatili wa kijinsia katika familia, shuleni na jamii
katika maeneo mbalimbali.
Aliongeza kuwa Plan inatambua kuwa ubaguzi dhidi ya wasichana ni sababu kuu
inayosababisha umaskini miongoni mwa watoto, wasichana kwa wavulana.
Alisema wasichana wana uwezekano mkubwa wa kukosa chakula , wanakabiliwa zaidi
na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na wanategemewa kufanya kazi nyingi za
nyumbani na hivyo kuwafanya wasifikie upeo na uwezo wao wa kiakili.
Alisema kwa hapa Tanzania kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi na shirika hilo
Oktoba mwaka jana kwa kushirikiana na wizara mbalimbali za Serikali, mashirika
ya haki na ustawi wa watoto, mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, mashirika
ya kitaifa na kimataifa, watoto pamoja na wadau wengine.
Alisema kwa mwaka huu
siku hiyo inasherehekewa kupitia shughuli na matukio mbalimbali nchi nzima
ambayo yanajumuisha watoto na jamii zao, vitengo na wizara mbalimbali na
taasisi wabia za kijamii.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment