Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, jana alitoa taarifa kwa umma akieleza
bayana kwamba yeye ndiye aliyeliruhusu gazeti hili kuendelea kutolewa kwa njia
ya mtandao (online) na Gazeti la Rai kutolewa kila siku.
Makalla alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya Idara ya
Habari-Maelezo kutoa taarifa kwamba Serikali imesikitishwa na Gazeti la
Mwananchi na gazeti dada la Rai, Mtanzania kukiuka masharti ya adhabu
walizopewa.
Septemba 27, mwaka huu Serikali iliyafungia Mwananchi kwa
siku 14 na Mtanzania siku 90.
Wakati likianza kutumikia adhabu yake, Mwananchi ambalo tayari
limemaliza kuitumikia, liliendelea kutoa taarifa kwenye tovuti yake wakati
Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ambayo inamiliki Mtanzania ilianza kuchapisha
kila siku gazeti la Rai ambalo awali lilikuwa likichapishwa kila wiki.
Katika ufafanuzi wake alioutoa
jana Makalla alisema: “Nimelazimika kueleza haya baada ya
taarifa mpya ya Idara ya Habari-Maelezo iliyohoji uhalali wa gazeti la
Mwananchi kuwa online (mtandaoni) na gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya
mara moja kwa wiki (Alhamisi).”
Katika ufafanuzi wake Makalla alisema kuwa Oktoba 4 mwaka
huu, alifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL) na New Habari Corporation (2006) Limited na Msajili wa Magazeti
na kwamba katika kikao hicho yaliwasilishwa maombi matatu.
“Waziri aliombwa kupitia upya adhabu iliyotolewa kwa magazeti
hayo. Katika hili majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye
dhamana na masuala ya habari pekee,” alisema.
Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwekwa katika mtandao, Makalla
alisema naibu msajili wa magazeti alisema kuwa hakuna sheria yoyote inayoweza
kuzuia gazeti hilo kuwa mtandaoni, lakini
aliwataka lisionekane gazeti zima kama
lilivyo, pia wabadili nembo ya gazeti na kuweka ya MCL.
“Baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo
lililotolewa na naibu msajili wa magazeti,” alisema Makalla.
Kuhusu Rai kutoka kila siku, alisema kuwa awali Kampuni ya
New Habari iliwahi kuomba kwa maandishi kwamba gazeti la Rai litoke kila siku
ambapo naibu msajili wa magazeti licha ya kukiri kulikuwa na tatizo la kiufundi
katika kurejea maombi hayo, alisisitiza kuwa hakuna kinachozuia gazeti hilo kutoka kila siku.
“Niliruhusu Mwananchi na Rai kuendelea na mambo yote
niliyoyaeleza baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote
uliofanywa na waombaji,” alisisitiza.
Alisema ameamua kuweka sawa jambo hilo kutokana na taarifa ya Idara ya Habari
Maelezo kutolewa bila kuwepo kwa mawasiliano kati yake na waziri, naibu waziri
wa wizara hiyo pamoja na naibu msajili wa magazeti.
“Ndiyo maana kuanzia Oktoba 10 mwaka huu, gazeti la Rai
lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, gazeti la Mwananchi likaanza kuwa
mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya naibu msajili wa magazeti,” alisema.
Ziafutazo ni taarifa mbili zinazokinzana za serikali;-
TAARIFA YA NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI
NA MICHEZO, MH. AMOS MAKALLA KWA VYOMBO VYA HABARI
Napenda kuufahamisha umma kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU
Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake,
pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.
Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana
na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la
Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Ndg xxxxxxxxx kuhoji uhalali wa Gazeti la
Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja
kwa wiki (Alhamisi).
Tarehe 4/10/2013 nilifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni
ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa
upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya
Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;
1. Ombi la kumuomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa
mageazeti hayo. Katika hili Majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu
ya suala hilo
ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.
2. Ombi la Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai
kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.
2.1 New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba
kwa maandishi (barua) kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu
Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la
kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti
la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe
kutoka kila siku.
2.2 Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili
alisema hakuna sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online
ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama
lilivyo pia wabadili nembo (Master Head) kwamba waweke nembo ya MCL na siyo ya
gazeti husika ambalo limefungiwa. Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa
kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti.
3. Hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya
Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka
misuguano isiyo ya lazima.
3.1 Pendekezo hili nililipokea na niliwasilisha kwa Mhe
Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na
ushauri wa kujenga uhisiano na vyombo vya habari.
3.2 Masuala ya Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka
kila siku, NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo hiyo, na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu
baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na
waombaji.
Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya
Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni
kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa upande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu
waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.
Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni
mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa
kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa
kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.
Imetolewa na:
Amos G. Makalla
Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na
Michezo
11 Oktoba 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Idara ya Habari – MAELEZO, inapenda kuufahamisha umma wa
Watanzania kwamba Mheshimiwa xxxxxxxx Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo amepokea maombi kutoka kwa wamiliki wa Magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania wakiomba kupunguziwa adhabu au kusamehewa adhabu wanazozitumikia
kuanzia 27 Septemba, 2013.
Wakati Mheshiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo anatafakari maombi hayo, amesikitishwa kuona kwamba magazeti haya
mawili yamekiuka masharti ya adhabu walizopewa.
Wamiliki wa Gazeti la Mtanzania baada ya kufungiwa wameamua
kuligeuza gazeti la kila wiki la RAI kuwa la kila siku bila ya kibali cha
Msajili wa Magazeti. Kwa mujibu wa ratiba ,gazeti la RAI linapaswa kutoka kila
siku ya Alhamisi.
Wamiliki wa gazeti la Mwananchi nao wameendelea kuchapisha
gazeti hilo
katika mtandao kinyume na agizo la kufungiwa.
Serikali inawataka wamiliki wa vyombo habari nchini kuwa na
utamaduni wa kutii sheria za vyombo vya habari zinazotumika wakati huu. Hivyo
serikali kwa mara nyingine tena inawataka wamiliki wa Gazeti la MTANZANIA,
kuzingatia ratiba yao
ya kutoa gazeti lao kila siku ya ALHAMISI.
Aidha, serikali inawataka wamiliki wa Gazeti la Mwananchi
kuacha mara moja kuchapisha gazeti lao katika mtandao kama
amri ya kufungiwa ilivyoanisha.
Imetolewa na,
Idara ya Habari – MAELEZO
10 Oktoba, 2013
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment