Saturday, October 12, 2013

Muhimbili na rekodi pekee ya kutenganisha watoto pacha



Madaktari wakiendelea na upasuaji wa watoto walioungana  katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha  watoto. 

Na Emmanuel Rubagumya, Mwananchi


Upasuaji wa kuwaokoa pacha pengine unadhaniwa kuwa ni jambo linalowezekana nchi za nje pekee. Lakini hata hapa nchini, inawezekana. 

Agosti 30, 2013 ulifanyika upasuaji wa kihistoria kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo mtoto aliyezaliwa ameungana na mwenzake kwa sehemu ya chini ya uti wa mgongo alitenganishwa na mwenzake ambaye hata hivyo hakuwa amekamilika viungo vyake.

Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Watoto, MNH Dk Zaitun Bokhary anaeleza mengi kuhusu tukio hilo na masuala mengine yanayohusu umahiri wa MNH katika kukabiliana na aina hiyo ya tatizo katika jamii pamoja na pia kutoa ushauri.
Anasema tukio hilo  limeandika historia nyingine kwenye  tasnia ya kitabibu nchini na kuonyesha kuwa Watanzania wanaweza.

Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wakishirikiana na wenzao ( MNH) walifanikisha upasuaji huo wa mtoto aliyezaliwa akiwa ameungana na mwenzake sehemu ya chini ya uti wa mgongo.
Licha ya kuwa na uhai, kiwiliwili cha mtoto huyo mwingine  hakikuwa na viungo muhimu kama kichwa na macho.  Pia, hakikuwa pia na moyo, figo, tumbo na maini, ila kilikuwa na uti wa mgongo.

Mtoto  huyo ambaye amepewa jina la Kudra alifikishwa MNH akitokea Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alikozaliwa na  mama yake, Pili Hija (24), Agosti 18, 2013.
Kwa kuona uwezo wao, madaktari wa Mnazi Mmoja waliamua kumhamishia MNH mtoto na mama yake kwa  upasuaji mkubwa zaidi ili kumwokoa.

Ushuhuda wa Dk Bokhary
Upasuaji kama huo wa kutenganisha  watoto pacha walioungana si wa kwanza kufanyika katika hospitali hiyo na hapa nchini.

Anasema mwaka 1994, Profesa Joseph Shija, gwiji wa kwanza Mtanzania mtaalamu wa upasuaji wa watoto aliwahi kufanya upasuaji kama huo.  Hata hivyo, tofauti na Kudra, watoto wale waliofanyiwa upasuaji na Prof Shija walikuwa wamekamilika, waliungana tumboni (omphalopagus), kila mmoja akiwa mtu kamili.  Mmoja wao alipona, mwingine  alikufa.

Upasuaji mwingine wa kutenganisha  pacha ni ule uliofanywa na bingwa  mwingine, Dk Petronila Ngiloi mwaka 2009 kwa pacha waliokuwa wameungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo (ischiopagus).

Kwa bahati mbaya, hao  walifariki  muda mfupi baada ya upasuaji wao.
Profesa Shija na Dk Ngiloi, wote kwa sasa ni wastaafu, ingawa wanaendelea na shughuli za tiba.

Dk Bokhary anasema kwamba baada ya kufanya vipimo mbalimbali na uchunguzi wa kina, Kudra na kitegemezi chake, timu ya wataalamu waliona kuwa ni kazi wanayoweza kuifanya.

“Tuliona kuwa ni ‘case’ (suala) tunayoweza kuifanya kama pakiwa na matayarisho mazuri na kujituma,” anasema Dk Bokhary.

Pamoja naye (Dk Bokhary), mabingwa wengine waliohusika na upasuaji huo ni Dk Ngiloi (aliyekaribishwa), Dk Robert Mhina (mifupa), Profesa Karim Manji (bingwa wa watoto), Dk Karim Khalid (dawa ya usingizi), Dk Hamis Shaaban (mishipa ya fahamu na uti wa mgongo) na Dk Bashir Nyangasa (moyo na mishipa ya damu).

Ingekuwa vipi kuwatenganisha watoto pacha wawili ambao wamekamilika?
Swali hilo analijibu Dk Bokhary akisema kuwa  mara nyingi huwa ni changamoto kubwa zaidi.  Ugumu huo hutokana na jinsi pacha hao walivyoungana.Anaongeza kuwa huhitajika wataalamu wengi zaidi na wa aina tofauti, teknolojia na vyombo vya kisasa.

Kwa mfano anaeleza tukio la watoto pacha, Eliud na Elikana Erick Mwakyusa waliopokelewa katika hospitali hiyo ya rufaa wakitokea mkoani Mbeya mapema mwaka huu. Hao anasema walikuwa wameungana kwenye njia ya haja kubwa na wakiwa na sehemu moja ya kiume.

Kwao, haikuwezekana kutenganishwa nchini na ililazimu kupata ufadhili  wa kuwapeleka India kwa sababu ilihitaji vipimo vya kisasa na utaalamu mkubwa ambao bado haupatikani nchini.

Kwa mfano, anasema pacha hao wanaoendelea na matibabu  India ikiwa ni matayarisho ya upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha, watahitaji wataalamu bingwa wa upasuaji wa watoto waliobobea na wale wa njia ya mkojo,  ambao bado hawapo nchini.
Pia, kama moja ya matayarisho, watoto hawa wanafanyiwa utaalamu unaojulikana kitaalamu kama ‘tissue expansion.’

Huduma hii, Dk Bokhary anaeleza kuwa  bado haipo hapa nchini na wataalamu wake wajulikanao kama ‘pediatric plastic surgeons’ bado hawapo.   Kitu kingine kinacholeta changamoto hadi kufikia kupeleka watoto kama hawa nje ni kukosekana kwa huduma maalumu baada ya upasuaji. Dk Bokhary anafafanua kuwa uangalizi baada ya upasuaji wa aina hiyo huhitaji chumba maalumu cha uangalizi wa hali ya juu na wataalamu/wauguzi waliofunzwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Chumba hicho  kinajulikana kama ‘Neonatal Intensive Care Unit’ (NICU), ambacho hakipo katika hospitali hiyo na nyingine nchini.

“Huwezi kupeleka watoto wachanga kwenye ICU ya watu wazima baada ya upasuaji kwa ajili ya uangalizi ni hatari na haikubaliki kitaalamu,” anasema mtaalamu huyo na kuongeza kuwa bado hii ni changamoto kubwa inayotakiwa kufanyiwa kazi.

Anasema wakati mwingine huwa anapata homa pale ambapo anatakiwa kufanya upasuaji mkubwa huku akijua kabisa kuwa hakuna Neonatal ICU katika hospitali hiyo, chumba ambacho husaidia sana kufuatilia maendeleo kwa karibu na kwa kitaalamu huduma baada ya upasuaji kufanyika.

Anasema Kudra amekuwa akiendelea vizuri kwa ushirikiano mkubwa wa timu ya wataalamu waliomshughulikia kila mmoja akimfuatilia kwa karibu kuhakikisha kila kitu kinakwenda vyema.
“Kusema kweli palikuwa na ushirikiano wa hali ya juu baina yetu,” anasema.

Sababu za  kuzaliwa wakiwa wameungana
Anasema kuwa hadi sasa hakuna sababu maalumu inayojulikana kisayansi.
Dk Bokhary anasema pacha walioungana huwa ni matokeo ya kushindwa kukamilika kwa mchakato wa yai kugawanyika na hatimaye kila upande uanze kujenga viungo vyake ili wapatikane pacha wanaofanana.

Mchakato huu hutakiwa kufanyika kati ya wiki ya tano na wiki ya nane ya ujauzito.  Hata hivyo, kwa sababu ambazo bado hazijajulikana,  mchakato huo hugoma kukamilika katika kipindi hicho na kusababisha  kuzaliwa  kwa pacha walioungana.

Anasema kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna vihatarishi vinavyoweza kusababisha yai lishindwe kutengana sehemu mbili kama inavyotakiwa. Anazitaja sababu hizo hatarishi kwa wazazi wote wawili kunywa pombe kupindukia, kuvuta sigara kupita kiasi, mtindo wa vyakula visivyofaa kama mafuta mengi, unene kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

“Tunadhani vihatarishi hivi vinaweza kusababisha mtu kuzaa mtoto asiye na afya au pacha walioungana,” anasema.
Pia, anashauri mama kuanza kutumia madini ya folic acid pale ambapo anajitayarisha kubeba mimba.

“Kinamama waanze kutumia madini haya pale wanapojitayarisha kubeba mimba, maana haya yanasaida katika kujenga viungo vya mtoto tumboni,” anaeleza.
Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, tafiti zinaonyesha kuwa tatizo la watoto pacha kuzaliwa wakiwa wameungana ni mara chache kutokea duniani ambapo kati ya kila watoto 100,000 wanaozaliwa, ni tukio moja  huwa ni la pacha walioungana.

Pia, wingi wa kuungana huku hutofautiana ambapo pacha walioungana tumboni ndio wanaoongoza kuzaliwa kwa asilimia 47; uti wa mgongo (asilimia 26); na pacha wanaozaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kichwa ni asilimia 2.
Mapacha wanazaliwa huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyake au Conjoined  Tetrapus Parasyticus Twins ni nadra zaidi kutokea.
Chanzo: Mwananchi


No comments: