Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa gumzo
kwa wapenzi wa filamu mwishoni mwa mwezi uliopita ni kufanyika tamasha la
kihistoria kwa mara ya kwanza linalohusisha kazi za waigizaji mbalimbali,
lililopewa jina la Dar Film Festival.
Tamasha hilo lilifanyika katika
Viwanja vya Posta Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, kuanzia Septemba 24-26
likiwa na mambo matamu hata machungu.
Tamu zake
Mwandaaji wa tamasha hilo, Myovela
Mfawisa, analizungumzia tamasha hilo kuwa lenye mafanikio kwa kuwa halikulenga
wingi wa watu bali kufikisha ujumbe kwa wanaouhitaji na ndiyo sababu halikuwa
na kiingilio.
Alisema kuwa mbali na kuonyesha
filamu tamasha hilo pia lilikuwa na vitu
mbalimbali vilivyolibeba zikiwamo semina na mikutano, mmoja ukiwa kati ya
wasanii, Baraza la Sanaa Tanzania,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na wadau wengine kama Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, ambao kwa pamoja
walifika, lakini waigizaji wenyewe ambao ndiyo walengwa wakuu hawakufika.
Anasema kuwa pamoja na kuangalia kazi
lakini pia kulikuwa na filamu zilizokusudiwa kuuzwa kwenye viwanja hivyo na
ziliuzwa kwa bei nafuu, tofauti na zinavyouzwa na walanguzi mitaani.
Kumbi mpya za sinema Dar
Anaitaja faida nyingine iliyojitokeza
kwenye tamasha hilo kuwa ni pamoja na mafunzo kwa ajili ya kuandaa filamu za
kuonyeshwa kwenye kumbi badala ya Cd. Anabainisha kuwa mafunzo hayo yalifanyika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata mahudhurio makubwa kutoka kwa wadau,
ambapo darasa moja la wanafunzi 20 lililazimika kupokea wanafunzi 40 kwa siku
zote yaani Septemba 24-26 na kwamba hilo ndilo kilikuwa lengo kuu.
“Mafanikio yalikuwa makubwa kwenye
hizi semina kwani ilikuwa ni wazi kila aliyetaka kushiriki. Wengi wa
waliohudhuria semina hizo ni wasomi, ambao wao ni rahisi kusambaza au
kukifanyia kazi walichojifunza hayo ni mafanikio tosha,”anasema Myovela.
Anafafanua kuwa kupitia tamasha hilo walipata wazo jipya
la kuzungumza na mmiliki wa majengo makubwa eneo la Kariakoo ambaye amekubali
kutoa kumbi nne kwa ajili ya kuyafanya majumba ya sinema. “Filamu zitakuwa
zikionyeshwa mara nne kwa wiki na mhusika kulipwa fedha yake papo hapo kwa
lengo la kukuza kipato cha wasanii.
Pia kukuza uwezo wao wa kufanya
kazi tofauti na kuingia katika soko la Kimataifa na kuachana na dhana kuwa
filamu zinazotakiwa kuonyeshwa kwenye majumba ya sinema ni za kizungu pekee na
siyo za Kiswahili,”anasema Myovela.
Wasomi wanena kuhusu Tamasha
Baadhi ya wasomi kutoka wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam waliohudhuria tamasha hilo
walitoa maoni yao ambapo Abdula Mohamed,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
anasema kuwa lengo la tamasha hilo
lilikuwa zuri na kwamba amejifunza mengi na kuona baadhi ya filamu ambazo kabla
hakuwahi kuziona.
“Nimejifunza katika semina na kweli
nimeona umuhimu wa kuwataka waigizaji wa nyumbani wabadilike na kwenda na kasi
ya dunia kuhusu masuala ya maigizo,”anasema Mohamed.
Naye Teacher Issa ambaye pia ni
Mhahiri katika chuo hicho anasema kuwa akiwa mmoja wa wawezeshaji katika
tamasha hilo
amebaini kuwa waigizaji bado hawajitambui na kutambua mchango wao kwenye jamii.
Anasema kuwa lengo lilikuwa zuri na
mwandaaji alifanya kile alichotakiwa kukifanya, lakini wahusika ambao ni
waigizaji walimwangusha kwa kuwa hawakutambua maana ya semina hiyo.
“Kuna umuhimu wa wadau kuhakikisha
wanawapa semina waigizaji wetu kuhusu tasnia ya filamu inapoelekea sasa.
Wanaweza kualikwa kwenye baadhi ya nchi, hakuna kuvaa kama
waigizaji bali ni kuhudhuria mafunzo na kurudi, wanahitaji elimu kwa kweli
watoke huko waliko na kuangalia mbele,”anasema Issa.
Waigizaji wazungumzia tamasha
Chungu
Hata hivyo Myovela anaonyesha
wasiwasi wake kwa waigizaji na wasanii kwa jumla akisema wanajitia kitanzi
wenyewe kwa kuogopa mikataba ya wazi.
Anabainisha kuwa hali hiyo
ilidhihirishwa na waigizaji wakubwa kutohudhuria tamasha hilo kwa kile alichoeleza wengi wao
wanawaogopa watu waliongia nao mkataba, ingawa mikataba hiyo haikuwafunga au
kuwazuia kuhudhuria matamasha yanayowahusu.
Hidaya Njaidi anasema kuwa
hakufurahishwa na kitendo cha wao wasanii kulipotezea tamasaha hilo
lakini akapendekeza wakati mwingine kuwepo na matangazo mengi kujua uwepo wa
tamasha kama hilo.
Jackob Steven, anasema kuwa
ilikuwa lazima ahudhurie kwenye tamasha hilo
lakini hakuhudhuria kutokana na kufanyika wakati ambao yeye alitakiwa kupiga
picha za filamu ndani na nje ya Jiji la Dar
es Salaam akiwa tayari ameshatumia fedha za kufanya
kazi hiyo.
Elizabeth Michael (Lulu), anasema
kuwa tamasha hilo lilikuwa zuri ingawa
linahitaji maboresho madogo kama ya matangzo
zaidi ili liweze kufana zaidi mwakani.
“Maboresho ni madogo yanahitajika,
cha msingi ni kulitangaza siyo kwa blogi pekee, bali hata kwenye redio na
kuweka mabango makubwa pembezoni mwa barabara ambayo yatamfanya kila mmoja ajue
nini kunaendelea wapi na lini,”anasema Lulu.
Filamu zilizoonyeshwa ni pamoja na
Network, Mdundiko, Shoe Shine, CPU na Foolish Age
No comments:
Post a Comment