Na. Aron Msigwa, Iringa
Wakati maadhimisho ya Wiki ya Vijana
kitaifa yakiingia siku ya tatu mkoani Iringa Serikali imewahakikishia vijana
kuwa itaendelea na mkakati wake wa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia
mikopo ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha na kuondokana
na umasikini.
Akizungumza na Vijana wanaoshiriki
maadhimisho hayo mkoani Iringa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Mh. Amos Makala amesema kuwa serikali katika kuhakikisha inatimiza
lengo hilo kwa kuanzia imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.1 katika bajeti ya
mwaka 2013/2014 ili kuwawezesha vijana kote nchini.
"Jambo hili la kuwawezesha
vijana tunalipa uzito mkubwa na kwa kuanzia katika bajeti ya mwaka huu
tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.1 kuwawezesha vijana, ni mwanzo mzuri
pamoja na kuwa tunahitaji kufanya zaidi" amesema
Amefafanua kuwa kiasi hicho cha fedha
kitatolewa kwa vijana walioamua kujishughulisha na wenye mawazo ya kujikwamua
kiuchumi na kuwataka vijana kote nchini kutumia fursa ya mikopo wanayopata
kuitumia katika kufanya shughuli za maendeleo.
"Nawaomba vijana muepuke kutumia
fedha hizo katika anasa na mambo mengine yasiyokusudiwa yanayowafanya mjikute
mmeingia katika matatizo ya madeni na kuendelea kuwa maskini" amefafanua
Hata hivyo amesema serikali kwa kuliona
jambo hilo imeandaa mpango wa kuwapatia elimu vijana ili waweze kuzitumia
ipasavyo fursa za maendeleo zilizopo na waweze kujiandaa kunufaika na kiasi
hicho cha fedha zilizotengwa pia inafanya jitihada za kuboresha vyuo vya vijana
pamoja na kuongeza idadi ya walimu wa vyuo hivyo.
"Nataka niwahakikishie kuwa
serikali inaendelea kuviboresha vyuo vyetu vya ndani ikiwa ni pamoja na
kushirikiana na nchi marafiki ambapo kwa kushirikiana na Afrika ya Kusini
tunaandaa utaratibu wa kupeleka walimu wetu ili waweze kusoma huko na kuja
kufundisha vijana katika vyuo vyetu" amesema.
Mh. Makala ameongeza kuwa tayari
serikali katika kushughulikia tatizo la ajira hasa kwa vijana wanaohitimu
masomo ya elimu ya juu kwa kuzungumza na baadhi ya taasisi za fedha zikiwemo
benki za NMB, EXIM Bank na CRDB ili ziweze kutoa mikopo kwa vijana hao kwa
dhamana ya vyeti vyao na kubainisha kuwa tayari baadhi ya benki zimekwisha anza
zoezi la kuwakopesha vijana kwa kutumia dhamana ya vyeti vyao.
Aidha kuhusu maadhimisho ya Wiki ya
Vijana kitaifa amesema kuwa inatokana na uamuzi waserikali uliofanyika mwaka
1999 mjini Dodoma wa kuhakikisha kuwa kila mwaka vijana wanapata fursa ya
kujumuika pamoja katika maadhimisho hayo.
Aidha amewashukuru viongozi wa mkoa
wa Iringa kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya ya kwa kushirikiana na viongozi
wa Wizara ya Habari Vijana , Utamaduni na Michezo kuhakikisha kuwa shughuli za
Wiki ya Vijana na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru tarehe 14/10/2013
zinafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
"Sisi kama viongozi wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo tunawashukuru sana viongozi wa Iringa kwa
ushirikiano mlioutoa katika kufanikisha shughuli hizi za Wiki ya Vijana
kitaifa, na ni matumaini yetu kuwa tarehe 14 mwezi huu wananchi wengi zaidi watajitokeza
katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2013" amesema Mh. Makala.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu
yanalenga kuwafanya vijana kujitambua na kuwakumbusha kuzitumia fursa za
kimaendeleo zilizo katika maeneo yao kujiletea maendeleo.
Amesema katika maadhimisho ya mwaka
huu licha ya kuwepo kwa maonyesho ya bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na
vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini vijana watapata fursa ya kujadili mada
mbalimbali katika midahalo ikiwemo mada ya kuujua mkoa wa Iringa na fursa za
kimaendeleo na ajira zilizopo katika mkoa wa Iringa, pia huduma za hifadhi ya
jamiii na maendeleo ya vijana,nafasi ya vijana wa Tanzania katika kutunza amani
na upimaji wa hiari wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt.
Christine Ishengoma amesema kuwa mkoa wa Iringa utaendelea kutoa msukumo kwa
vijana ili waweze kujiletea maendeleo kutokana na fursa zilizopo ndani ya mkoa
huo.
Ameongeza kuwa mkoa huo kwa muda mrefu
umekuwa na jukumu la kuwaandaa vijana kuwa watu wanaojitegemea, kuwa viongozi
na watoa maamuzi sahihi, wajasiriamali na wazazi wanaowajibika na kuongeza kuwa
serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kutoa elimu
kwa vijana kuhusu uzazi salama, ujasiriamali na kujikinga dhidi ya maambukizi
ya Ukimwi.
Dkt. Ishengoma ameeleza kuwa mkoa wa
Iringa umeanzisha mfuko wa kuwawezesha vijana kwa kuwapatia mikopo na mitaji ya
kuendesha miradi midogo midogo ya kiuchumi na kuondoa tatizo za utegemezi na
tayari vikundi vipatavyo 70 katika halimashauri za mkoa wa Iringa katika mwaka
2012/2013 vimepatiwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 116.
No comments:
Post a Comment