Naibu waziri wa fedha, Saada Salum
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitajwa kuwa ni miongoni
mwa nchi zenye amani na utulivu, imebainika kuwa Watanzania ni miongoni mwa
watu wasio na furaha na waliokata tamaa hapa duniani.
Ripoti inayoonyesha orodha ya nchi
zenye furaha duniani ya mwaka 2013 (World Happiness Report 2013), imeitaja Tanzania kuwa
ni miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya nchi 156 zilizofanyiwa
utafiti huo.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kundi la
wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mwaka 2010 na 2012, inaonyesha
kuwa Tanzania imeshika
nafasi ya 151 ikiburuta mkia pamoja na nchi za Rwanda,
Burundi, Jamhuri ya Afrika
ya Kati, Benin
na Togo.
Upatikanaji wa huduma za jamii,
mtazamo wa watu kuhusu rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la taifa
na ukarimu wa watu katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo vilivyoangaliwa
wakati wa kuandaa taarifa hiyo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka alieleza kushtushwa na ripoti hiyo kwa maelezo kwamba ni asilimia 11.7
tu ya Watanzania wasio na ajira na kwamba wale wanaofanya kazi, wanapata huduma
zote za msingi, ikiwa ni pamoja na kwenda likizo na mishahara inayolingana na
taaluma zao.
“Watanzania wana furaha, kwa upande
wa wafanyakazi wanapata haki zao zote wanazostahili, sijui ni vigezo vipi
wametumia…kwa mujibu wa takwimu za 2006 ni asilimia 11.7 ya Watanzania ndio
waliokuwa hawana kazi, lakini wakati huo idadi ya watu ilikuwa ndogo, hivi sasa
imeongezeka,” alisema Kabaka na kuongeza:“Usafiri ndiyo tatizo linalowasumbua
wafanyakazi wengi kwa kuwa wanachelewa kwenda kazini.”
Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Saada
Salum alisema pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kutambua furaha ya
Watanzania, umaskini ndiyo unaoweza kuwa chanzo cha Tanzania kushika nafasi za mwisho.
“Inategemea na vigezo vingine
walivyovitumia, nakubali kuwa Tanzania
ni maskini pengine hali hiyo imeifanya nchi kushika nafasi ya mwisho,” alisema
Salum.
Nchi zilizoongoza
Taarifa hiyo imezitaja nchi tano;
Denmark, Norway, Uswisi, Netherlands na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza kwa watu
wake kuwa na furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi ya kwanza Afrika
na ya 61 duniani ikifuatiwa na Algeria (73), Libya (78), Ghana (86), Zambia
(91), Lesotho (98), Morocco (99) na Swaziland (100).
Kwa upande wa Afrika Mashariki,
wananchi wa Uganda ndio
walionekana kuwa na furaha zaidi kwani nchi hiyo imeshika nafasi ya 120
wakifuatiwa na Kenya (123), Tanzania (151), Rwanda
(152) na Burundi
(153).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya
mwaka 2005 na 2012, nchi 60 duniani ziliongeza viwango vya furaha kwa watu
wake, kati ya hizo 16 zikiwa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Nchi 29 zilibaki katika viwango vya
awali, huku watu kutoka nchi 41 wakipunguza viwango vyao vya furaha.
Ikilinganishwa na ripoti ilifanywa
kati ya 2005 – 2007, Tanzania
imeshuka kutoka asilimia 40 hadi 37. Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 10 ya
watu duniani wanasumbuliwa na matatizo ya akili ambayo yamewasababisha kukosa
furaha.
Hata hivyo, imebainika kuwa mtu mmoja
anaweza kukosa furaha kutokana na sababu zaidi ya moja.
“Mtu mmoja anaweza kukosa furaha
kutokana na sababu mbalimbali kama umaskini,
ukosefu wa kazi, kuvunjika kwa ndoa na kusumbuliwa na ugonjwa. Lakini sehemu
kubwa, matatizo sugu ya akili yamesababisha kukosekana kwa furaha,” inasema
sehemu ya ripoti hiyo.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema bado hajaiona na
kwamba atakapoisoma atakuwa tayari kuizungumzia.
“Sijaiona ripoti hiyo kwa hivyo
siwezi kusema chochote hadi niione, wewe si umeiona ndiyo maana ukatupa
maswali?” alihoji Dk Mwinyi.
Wataalamu wanena
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga, alisema
Watanzania wengi wanakuwa na hasira kila wakati kutokana na kukosa matumaini,
baada ya mambo yao
kushindwa kufanikiwa.
Alisema hali hiyo inatokana na watu
wengi kushindwa kudhibiti magonjwa na matatizo mengine yanayowakabili.
“Watanzania wengi wanasumbuliwa na
mood disorder, wanakuwa wakali, wenye hasira kila wakati. Mambo yao hayaendi wamekosa
tumaini. Hali hiyo inawakumbwa hata watoto ambao wanakosa mahitaji yao ya msingi,” alisema
Kimonga.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa
zipo sababu mbalimbali zinazowafanya watu kuwa na furaha: “Wanauchumi wanasema
furaha inaletwa na kipato kikubwa, wanasaikolojia wanaamini furaha inakuja
baada ya mtu kuwa na afya njema na viongozi wa dini wanaamini furaha huletwa na
maadili mema,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kuna uhusiano wa karibu kati ya umaskini na
furaha, kwa kuwa mtu asiye na kipato cha kununua mahitaji yake ya msingi hawezi
kuwa na furaha.
“Gharama za bidhaa zipo juu, mtu
masikini hawezi kuwa na furaha, hata hivyo haimaanishi kuwa nchi tajiri ndizo
zenye furaha. Nchi kama Norway
pamoja na kuwa na uchumi mzuri, lakini ina idadi kubwa ya watu wanaojinyonga,”
alisema Ngowi.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwenyekiti
wa Chama cha Kijamii, Costantine Akitanda, alisema taarifa hiyo iko sahihi na
kwamba karibu kila Mtanzania analalamika.
“Ukichunguza utagundua kuwa karibu
kila Mtanzania analalamika. Hata sera zilizopo hazina mfumo unaowawezesha watu
kunufaika na maliasili za taifa,” alisema Akitanda.
Pamoja na msukosuko wa uchumi
ulioitikisa dunia kuanzia mwaka 2008, dunia imeshuhudia watu wakiongeza viwango
vyao vya furaha kutokana na sababu mbalimbali kulingana na mahali nchi ilipo.
Mkazi wa Mabibo, Kinondoni jijini Dar
es Salaam, Vick Manonge, alisema ripoti hiyo inaonyesha hali halisi ilivyo hivi
sasa hapa nchini, kwa kuwa watu wengi wanaonekana kuwa na hasira.
“Kama kuna mtu hakubaliani na hilo (ripoti hiyo)
aangalie kwenye daladala watu walivyo na hasira bila sababu ya msingi, mwingine
hataki aulizwe hata nauli, “ alisema Manonge.
Katika siku za hivi karibuni baadhi
ya viongozi wakubwa duniani wamekuwa wakizitaka Serikali kutunga sera za
maendeleo zitakazoendana na hali halisi ya maisha ya watu wa eneo husika, ili
kuweka mazingira yatakayowaletea wananchi furaha.
Baadhi ya huduma zinazotolewa na
serikali ni afya, kutengeneza ajira, elimu na kuweka mazingira bora ya
kujiwezesha kichumi kwa kila Mtanzania.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment