Kwa ufupi
Hata hivyo, kazi yangu naikubali pamoja na
ugumu wake. Siku nyingine huwa napokea maswali ya “Nifanyeje ili anirudie”,
“Natafuta mchumba” na kadhalika. Watu wakishasikia wewe ni Mwenyekiti wa Mtaa
basi wanakuletea hadi matatizo ya ndoa zao.
“We mama lete kinywaji! Nusu saa
nzima? Au bia ndiyo inapikwa?” Nilibwata kwa hasira maana subira
ilishanichosha. Sijui kwa nini Wabongo hatujali muda. Hapa hapa niliwahi
kuagiza kuku nikasubiri saa nzima. Kana kwamba mchinjaji ndiyo alikuwa
akimfukuza huyo kuku.
Yule mama (ukweli alikuwa binti,
lakini watu wabaya walikwisha kumchosha) akainuka bila neno, akaenda
kunichukulia kinywaji. Sikuacha kumpa maneno yake: “Ukitaka kufanikiwa kazini
ni lazima uipende kazi yako…”
“Ongea mengine bwana we! Niwe na kazi
mie (akataja kabila)?” Nikaufyata.
Kabla sijapiga funda, mgeni alisimama
mbele ya meza yangu: “Habari gani Mheshimiwa!”
“Nilitua chupa mezani: “Nzuri ndugu,
karibu.”
Alivuta kiti pasi na kujibu. “Mimi
sitaki lawama, bali nimekuja kukuambia ukweli…”
He! Yameshakuwa hayo tena? Mwenyewe
nimekuja mahala tulivu nikate kiu na kupoza machungu ya kazi za mchana kutwa,
mara nimegeuzwa kuwa Pilato?
Hata hivyo, kazi yangu naikubali
pamoja na ugumu wake. Siku nyingine huwa napokea maswali ya “Nifanyeje ili
anirudie”, “Natafuta mchumba” na kadhalika. Watu wakishasikia wewe ni
Mwenyekiti wa Mtaa basi wanakuletea hadi matatizo ya ndoa zao.
Anyway, nilimuuliza kulikoni? Kwa hasira
alianza kubwata hadi nilifunika uso kwa mate yalivyomruka: “Wewe ni mwizi! Tena
huna haya hata kidogo! Mimi ndiye mlevi orijino, lakini huko mtaani watu wote
wanakuita wewe mlevi. Umeniibia jina langu!”
Nilishangaa sana.
Ghafla nikawa na hamu ya kumwangalia
vizuri. Ni kweli alikuwa na ndevu za ovyo ovyo, ngeu mbili tatu usoni na
ukosefu wa meno ya barazani. Koti lake
jeusi lililobadilika na
kuwa la rangi ya udongo lilimwongezea CV ya wadhifa huo.
“Unaitwa nani?” Niliuliza ili nipate
uhakika kwamba naongea na mtu timamu. Usije kushangaa meza inasambaratishwa na
unaachiwa deni la chupa zilizovunjwa.
“Yahaya ei kei ei Mlevi. Uliza Kwa
Mfuga Mbwa wote wananijua.” Alijibu kwa kujiamini.
“Unaitwa Yahaya au unajiita Yahaya?”
Niliuliza tena.
“Nimekambia naitwa Yasini. Babaangu
mwenyewe ndo kanigea jina hilo.”
“Mpo Yahaya wangapi hapa duniani?”
Nikaendelea kuhoji maana niligundua kuwa pamoja na baadhi ya skurubu kukosekana
ubongoni mwake, bado alimaanisha alichokisema.
“Hizo dharau sasa…” Aling’aka. “We
unaweza kuniambia mko walevi wangapi hapa mjini?” Unaona sasa, hata yeye
kaniita Mlevi.
“Kwa hiyo unakasirika mwenzio akiitwa
Yahaya?” Nilimuuliza badala ya kumjibu.
“Nshakuambia hizo dharau… Ni lazima
tuelewane la sivyo patachimbika hapa!”
“Unataka kuniambia hilo koti ni wewe ndiye uliyelianzisha?”
“Ohoooooooo…”
Alileta mzozo hadi baunsa wa baa ile
alipokuja kumtoa. Kweli siku mbaya huonekana kungali mapema. Hata hivyo
niligundua kitu. Watu wengi hufikiri kuwa kila wanachokiona ni kitu kipya,
kumbe ni kipya kwao.
Mwenyezi Mungu alipouumba ulimwengu,
tunaambiwa kuwa alitumia siku sita. Kuanzia Jumangapi hilo usiniulize, ila ndani ya siku hizo kila
kitu kiliumbwa. Kinachoonekana kama udongo na hata kisichoonekana kama upepo. Hakuna kitu kipya hata kimoja kilichozuka
baadaye.
Kinachofanyika sasa ni uharibifu tu.
Mtu anaponda udongo na chokaa kisha anaita sementi. Mwingine anasaga mahindi na
kuita unga: uwe wa chapa hii au ile, bado ni kitu kilekile; unga. Pamba
ikageuzwa nguo, ngozi ikawa kiatu, shayiri ikawa bia, zabibu ikawa mvinyo,
papai likawa gongo… aaaah! Huku tunakowenda sasa siko.
Lakini hakuna jipya chini ya jua. Ebu
tuangalie mfano hai, au nikuulize swali hai: Ni nyimbo ngapi ambazo umewahi
kuzisikia zinazoitwa “Nakupenda”. Iwe “Nakupenda Salima”. “Mariam Nakupenda” au
vyovyote vile. Jibu ni kwamba hujui idadi yake.
Hata muda huu tunapoongea
yupo kijana na rundo la makaratasi, anarekodi wimbo wake utakaokwenda kwa jina
la “Nakupenda” sijui nani. Hapa inategemea: Juu ya makaratasi kumeandikwa
“Nakupenda Halima”. Lakini kesho Halima akileta pozi kichwa cha habari
kitageuka kuwa “Nakupenda Monika” ili mradi Monika aonyeshe “ushirikiano” wa
kutosha. Alamsiki.
No comments:
Post a Comment