Ni saa
9.00 alfajiri katika Kijiji cha Sintale, wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Maumivu ya uchungu wa kujifungua yamemuanza binti aitwaye Naomi John.
Amewahishwa
katika zahanati ya kijiji ambayo hata hivyo haina dawa wala vifaa zaidi ya
mkunga wa zamu wa siku hiyo.
Kwa
kuwa hakuna usafiri wa ku mwahisha Naomi katika hospitali ya wilaya, mkunga
anajaribu kumsaidia katika kujifungua, lakini baada tu ya kujifungua, dada huyu
anatokwa na damu kwa wingi, lakini pia, kichanga kilichozaliwa kinashindwa
kupumua na kwa bahati mbaya wote… wanapoteza maisha.
Roho
za kinamama na watoto wengi zinapotea kila kukicha kutokana na ukosefu wa
huduma za afya, jambo ambalo limesababisha idadi ya vifo vya
makundi haya kuwa milioni 6.9 kwa mwaka.
Vifo
vya mama na mtoto vinaepukika na katika kupunguza vifo hivyo wataalamu wa afya
wamebuni teknolojia nyepesi na nafuu itakayowezesha wataalamu wa afya katika
eneo lolote Kusini mwa Jangwa la Sahara kuokoa
maisha ya viumbe hawa muhimu duniani.
Shirika
la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa, uvumbuzi wa teknolojia rahisi
utaweza kuokoa maisha ya wanawake na watoto zaidi ya milioni 7.5 kwa mwaka.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki- Moon amesema, uvumbuzi huo ni sehemu
muhimu kwa kila mwanamke na kila mtoto duniani kwani ni miongoni mwa harakati
za kuokoa maisha ya wanawake na watoto milioni 16 ifikapo mwaka 2015.
Kupunguza
vifo vya wanawake na watoto ni miongoni mwa malengo ya Milenia ya Umoja wa
Mataifa. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa, kati ya watoto 1,000
wanaozaliwa nchini kila siku, 26 hufariki kwa sababu zinazoweza kuzuilika. Wasaidie
watoto kupumua (Helping Baby Breath) ni teknolojia inayotumiwa na wataalamu wa
afya sehemu yeyote ile kuwasaidia watoto wanaozaliwa na kushindwa
kupumua.(birth asphyxia) Teknolojia hii imesaidia kupunguza asilimia 47 ya vifo
vya watoto wanaozaliwa na tatizo la kupumua nchini.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Profesa Cyriel Massawe anasema, iwapo
teknolojia zaidi zingevumbuliwa, basi vifo vya wanawake na watoto vingekwisha
kabisa.
“Tatizo
kubwa ni kuwawezesha wataalamu wa afya. Hata kama teknolojia hizi zitavumbuliwa
bado wataalamu wanahitaji usafiri ili kuzifikisha vijijini ambako kuna vifo
zaidi, ” anasema Profesa Massawe.
Profesa
Massawe anasema ni teknolojia rahisi kutumika kwani inafundisha mbinu za
kumkausha mtoto pindi anapozaliwa na kumvalisha kifaa maalumu kinachomsaidia
kupumua.
Wakunga
nchini walipewa mafunzo hayo na jinsi ya kutumia kifaa aina ya ‘Neonatalie’
ambacho ni kifaa rahisi kutumiwa na mtaalamu yeyote hata mkunga wa jadi ili
kumsaidia mtoto mwenye matatizo ya kupumua pindi tu anapozaliwa. Teknolojia
nyingine inayofanana na HBB ni ‘Bubble CPAP,’ kifaa cha njia ya upumuaji
ambacho huwasaidia watoto waliopata matatizo ya mfumo wa upumuaji ikiwemo
nimonia.
Kifaa
hiki huingiza hewa safi
katika mapafu ya mtoto. Kwa gharama ya Sh640,000 kifaa hiki kinachotumia
pampu na chupa ya maji kinaweza kuokoa maisha. Simu za Oximeter ni
simu za gharama nafuu zenye kifaa kinachosimamiwa kinachopima
kiwango cha oksijeni katika damu na kuwapa taarifa watendaji wengine wa afya
kupima nimonia.
Teknolojia
ya simu kupima saratani ya shingo ya kizazi nayo imo kwenye orodha hii.
Wataalamu wa afya wa Tanzania
na Canada
wameshirikiana katika kupunguza vifo vya wanawake wenye saratani ya shingo ya
kizazi kwa kutumia simu za mkononi katika maeneo ya vijijini.
Timu
ya wataalamu wa afya itakwenda katika maeneo ya pembezoni nchini ili kuwapima
wanawake wanaoishi mbali na huduma za afya. Wauguzi ambao watapewa vifaa vya
kupimia saratani hiyo pamoja na simu zenye teknolojia.
Watatakiwa
kutumia simu kuchukua picha za kizazi cha mama na kuzituma kwa njia ya ujumbe
kwa wataalamu wa afya. Wataalamu walio katika hospitali zenye vifaa
wataichunguza picha ya kizazi. Watarudisha majibu kwa waugu na kuanzishiwa
tiba.
Ipo
pia teknolojia ya Kit Yamoyo. Hiki ni kisanduku kilicho na dawa za kuzuia
kuhara, pamoja na sabuni. Teknolojia hiyo ambayo kwa jina jingine inaitwa Cola
Life inasambazwa katika masanduku ya vinywaji vya Coca Cola ili kuwafikia
watu wengi zaidi hata walio mbali vijijini. Magonjwa ya kuhara kwa watoto
yanasababisha vifo zaidi ya 600,000 kila mwaka.
Anti–shock
garment. Hiki ni kifaa kinachofungwa katika sehemu ya chini ya mwili wa mama
ili kuzuia damu kutoka kwa wingi baada ya kujifungua na vilevile kifaa hiki
husaidia kuhifadhi damu katika ogani ya moyo, mapafu na ubongo hadi mama
atakapopewa huduma zaidi.
Mhadhiri
wa Ukunga katika Chuo cha Ukunga Muhimbili, Dk Selbada Leshabari
anasema mama anapotoka damu kwa wingi ogani ya moyo, mapafu na ubongo
hupata mshtuko kwa sababu damu hujikusanya sehemu za chini na miguuni.
Majaribio
ya uvumbuzi huu yalifanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na
katika kambi mbili za wakimbizi.
Kifaa
hiki huifanya damu itembee katika sehemu nyingine za mwili na hivyo kuzuia
kifo.
Kutoka
damu kwa wingi ni sababu kuu ya vifo vya kinamama na huua wanawake zaidi ya
72,000 kila mwaka.
Chlorhexidine.
Hizi ni dawa zinazotolewa kwa gharama nafuu ili kuzuia maambukizi
katika kitovu cha mtoto mchanga. Maambukizi katika kitovu husababisha vifo kwa
watoto kwa asilimia 12 kila mwaka.
Rotovac,
ni chanjo kwa ajili ya kuzuia virusi vinavyosababisha ugonjwa wa kuhara ambao
ni maarufu katika nchi zinazoendelea. Chanjo hii inayotolewa pamoja na madini
ya zinc na ORS ina uwezo wa kuondoa ugonjwa wa kuhara.
No comments:
Post a Comment