Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Maisha ya wahudumu wengi wa baa ni ya kubahatisha, ingawa
baadhi yao wana
majukumu mengi nyumbani. Kumekuwa na ahadi nyingi za kuwasaidia watu hawa bila
mafanikio. Nini hatma ya wafanyakazi wa baa hususan wahudumu wa baa, ni swali
lisilo na jibu, wengi wanaifanya siyo kwa kupenda bali kwa sababu tu ya hali
ngumu ya maisha.
Umeshawahi kujiuliza unaweza
kuufanyia nini mshahara wa shilingi elfu 60 kwa mwezi? Basi usishangae pale
unapozidishiwa bili, unapoombwa ofa au kutegwa kwa namna yoyote ili utoe fedha
zaidi, hii yote huja ili kuongezea kipato.
Piga hesabu hizi, kodi ya chumba
shilingi 15,000, nauli ya daladala kwa siku tufanye shilingi 800 kwa siku
(inaweza kuwa zaidi kwa wanaopanda mabasi manne kwa siku) , kilo moja ya unga
900, sukari shilingi 2,000 ukipiga na mahitaji mengine muhimu unaweza kuona hii
shilingi elfu 60 inaisha ndani ya siku mbili tu.
Sasa je wanamudu vipi gharama za
maisha ambazo zinapanda kila kukicha? Salma Chitenga (Sio jina lake halisi)
anasema kila kazi ina mbinu zake; kwani kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba
yake.
Anasema yeye na wenzake sita wanaishi
katika chumba walichopewa na mmiliki wa baa anayoifanyia kazi iliyopo maeneo ya
External jijini Dar es Salaam.
“Ninaishi katika chumba
tulichopewa na mmiliki wa baa ninayoifanyia kazi ( mwenyewe analiita ‘ghetto’)
akisema kuwa fedha anazolipwa zinamsaidia kujikimu na kusaidia ndugu zake
waliopo kijijini.
“Ninalipwa shilingi 60,000 kwa mwezi,
lakini kila siku ninapewa shilingi 1,500 kwa ajili ya chakula, pia tajiri
ametupa chumba tunaishi hapa, fedha ninayopata ninanunua nguo na pia kiasi
kidogo huwa ninamtumia mama yangu kijijini,” anasema Salma.
Aisha Suleiman ni mfanyakazi wa baa
na ni mama wa mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Yeye
anasema changamoto yake kubwa iliyo mbele yake ni jinsi ya kuibana fedha ndogo
anayoipata.
“Nina mtoto mdogo ambaye anahitaji
matunzo na mshahara wenyewe ni duni, inabidi nitumie mbinu mbalimbali
kujiongezea kipato,” anasema Aisha.
Aisha anasema zipo njia nyingi za
kujiongezea kipato ambazo wafanyakazi wa baa huzitumia huku akisisitiza kuwa
zipo mbaya na nzuri.
Anakiri kuwa mshahara wa shilingi
60,000 ni mdogo hasa kwa mtu mwenye familia kama
yeye kwani lazima apange chumba na aache hela ya chakula kila siku.
“Kwa kuwa kazi zangu ninafanya usiku,
inabidi katika hiyo fedha ninunue na maziwa ya mtoto pia nimuachie fedha kidogo
mtu anayenitunzia mtoto wangu wakati sipo, nimeshindwa kuajiri mfanyakazi wa
ndani kwa kuwa kipato changu ni kidogo,” anasema Aisha.
Waswahili wanasema njaa huleta akili
na hivi ndivyo anavyosimulia Aisha akisema kuwa msukumo wa kutafuta fedha zaidi
umetokana na majukumu aliyonayo kwa familia yake.
“Kuna njia nyingi za kujiongezea
kipato, mfano ukipata wateja na kuwapa huduma nzuri hawawezi kuondoka bila
kukupa chochote au hata ofa ya kinywaji,” anasema na kuongeza.
“Ukiwa mkarimu kwa mteja, hasa
wanaume, anaweza kukupa ofa ya bia, hapo ni ujanja wako sasa ‘kucheza’ ili ile
ofa usiinywe na badala yake uchukue fedha kwasababu wateja wengine akikupa bia
anakulazimisha uinywe,” anasema Aisha.
Aidha anasema hategemei ofa za bia
peke yake, anapohudumia wateja vizuri pia humpa kitu kidogo maarufu kwa jina la
‘tip’ akisema hizo pekee kwa siku kama mambo yakienda vizuri anaweza kupata
hata Sh 5,000.
Hii ni sehemu tu ya maisha ya
wafanyakazi wa baa, wapo ambao hulipwa kutokana na huduma waliyotoa kwa siku,
wapo ambao hulipwa kwa kuongeza bei ya kawaida ya vinywaji ya baa husika,
lakini wapo ambao hujilipa wanavyojua wenyewe.
Usikose kusoma shuhuda za wafanyakazi
wa baa jumatatu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment