Mawaziri wa mambo ya nje Afrika
wanakutana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia
kujadili uhusiano wa bara la Afrika na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia
Tedros Adhanom Ghebreyesus ameilaani mahakama ya ICC kwa kusema ina mapendeleo sana na hicho sio kitu
kinachokubalika na kuwa ina uonevu kwa nchi za Afrika.
Waziri huyo ameyasema hayo wakati wa
ufunguzi wa kikao maalum cha AU kuhusu mahakama ya ICC.
Kikao hicho kinafuatia ombi la
serikali ya kenya.
Umoja wa Afrika unaishtumu mahakama
ya ICC kwa kuwalenga viongozi wa bara hilo
huku ikipuuzilia mbali uhalifu mwengine dhidi ya binadamu unaotekelezwa katika
maeneo mengine ulimwenguni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
kikao hicho waziri wa maswala ya kigeni kutoka Ethiopia Tedros Adhanom
ameishtumu mahakama hiyo kwa kukataa kuheshimu uwezo wa marais wa bara Afrika
na kukitaka kikao hicho kushutumu mahakama hiyo.
Aidha amekitaka kikao hicho kuwasilisha ombi la kuahirisha kesi zinazowakabili Rais wa kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake Wiliam Ruto kusikizwa katika mahakama hiyo.
Mkutano huu maalum umeitishwa baada
ya ICC kukataa ombi la wanachama 34 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za
Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani.
Miongoni mwa yatakayozungumziwa ni
hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana
kati ya ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU
katika kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya
ICC imekosa kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za Kenya. AU
inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu
wake William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu katika
mahakama hiyo.
Kesi yao
inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi
ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha
madai hayo.
Bunge la Kenya
ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari
lieanzisha hoja ya kuondoa Kenya
kutoka katika mahakama ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza nchi za Afrika
kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na majirani zake kama Uganda na Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus
Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo
sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa
huenda AU isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na Botswana tayari zimepinga hatua ya
kujiondoa ICC.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment