HII haijawahi kutokea! Kwa mechi ya
watani wa jadi inaweza kuwa historia. Dakika 45 za mwanzo ungedhani Mnyama
amechinjwa, lakini huwezi kuamini kwani Simba walisema: “Hawatuwezi.”
Yanga iliyocheza kwa mbwembwe dakika
45 za mwanzo iliondoka na kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ikiwa
inaongoza kwa mabao 3-0, lakini hali ilibadilika kipindi cha pili baada ya
Simba aliyejeruhiwa kuingia kwa kasi uwanjani na kusawazisha mabao yote matatu
na kuufanya ubao wa matokeo usomeke 3-3 mpaka dakika ya mwisho ya mchezo.
Kwa matokeo hayo, mashabiki wa Simba
wanaona kama wameshinda mchezo, kwani wanaamini kusawazisha mabao hayo ni
ushujaa mkubwa na hakika wanastahili kujisifu kwa hilo.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara
iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana Jumapili, Yanga ndio
waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 14 mfungaji akiwa, Mrisho Ngassa.
Ngassa alifunga bao hilo kutokana na
juhudi za Mrundi, Didier Kavumbagu aliyeambaa vizuri na mpira na kumpasia Hamis
Kiiza ambaye alimuunganishia Ngassa aliyeujaza wavuni akiwa katikati ya mabeki
wawili wa Simba, Gilbert Kaze na Joseph Owino.
Kiiza afanya kweli
Yanga waliongeza bao la pili dakika
ya 35 mfungaji akiwa ni Kiiza. Mpira ulirushwa na Mbuyu Twite na Kavumbagu
akaupiga kichwa kwa nyuma na kumkuta Kiiza aliyeujaza wavuni.
Awali kipa wa Simba Abel Dhaira
alitaka kuufuata mpira uliorushwa na Twite lakini akasita na ndipo Kavumbagu
alipotumia nafasi hiyo kuupiga kichwa na Kiiza kuujaza wavuni kwa shuti la mguu
wa kulia.
Yanga iliandika bao la tatu dakika ya
45 mfungaji akiwa ni Kiiza tena. Kiiza alifunga bao hilo kutokana na mpira
ulioanzia kwa Haruna Niyonzima ambaye aliukokota vyema na kumuunganishia
Kavumbagu.
Kavumbagu licha ya kuonekana yuko
katika nafasi nzuri ya kufunga, hakuonyesha ubinafsi, alimuunganishia pande
safi Kiiza aliyeujaza wavuni.
Mashabiki Simba wasusa
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko,
Yanga walikuwa mbele kwa mabao yao matatu hali iliyowafanya baadhi ya mashabiki
wa Simba kuanza kuondoka uwanjani na kufanya baadhi ya majukwaa ya upande wa
Simba kuwa tupu.
Wakiwa katika hali ya huzuni
mashabiki hao walionekana wakiinuka vitini mmoja mmoja wakiamini kwamba timu
yao ingefungwa mabao mengi zaidi.
Hatua hiyo ya mashabiki hao pengine
ilichangiwa na kucheza hovyo kwa timu hiyo na kuruhusu mabao ambayo yalitoa
dalili ya mvua kuwa wangefungwa zaidi kipindi cha pili.
Lakini ikawa si hivyo kwani Simba
iliingia kipindi cha pili na nguvu mpya baada ya kupewa maelekezo na kocha wao,
Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ambaye pia aliwatoa, Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’
na Haruni Chanongo wakaingia, Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ dakika ya
46.
Vijana wa maajabu
Kuingia kwa Ndemla na Gallas ambao
wamepandishwa kutoka timu ya vijana kuliifanya Simba ing’are kwani safu ya
kiungo ilitawala zaidi na kuifanya safu ya ushambuliaji, iliyokuwa imesinzia
kipindi cha kwanza kuamka na ikawa urahisi kwa Betram Mwombeki na Mrundi Amis
Tambwe kupata mipira mingi na dakika ya 53 Mwombeki aliwafungia Simba bao la
kwanza.
Mwombeki alifunga bao hilo akiwa yeye
na kipa wa Yanga, Ally Mustaph ‘Barthez’ baada ya mabeki wa Yanga, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani kujichanganya na wote kumkaba Amis Tambwe.
Wakati mabeki hao wakipambana na
Tambwe, mchezaji huyo kutoka Burundi alimsogezea mpira Mwombeki ambaye aliujaza
wavuni kiulaini.
Simba wazidi kucharuka
Dakika tatu baada ya bao hilo, kasi
ya Simba iliongezeka na kulisakama lango la Yanga ambao mabeki wake na safu ya
kiungo walionekana kama wamechanganywa na kasi hiyo ya vijana wa Msimbazi.
Hatimaye mpira wa kona uliopigwa na
Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 56 uliwapita wachezaji wa Yanga na kumkuta
Joseph Owino ambaye aliujaza wavuni kwa kichwa na mpira kumshinda kipa wa
Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’ ambaye licha ya kuurukia lakini akawa kama
anausukumizia wavuni.
Mabao hayo yaliamsha ari zaidi na
kufufua matumaini ya wachezaji wa Simba na kwa mara nyingine juhudi zao zilizaa
matunda dakika ya 83 kwa bao la Gilbert Kaze aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa
adhabu ndogo uliopigwa na Nassor Said Chollo.
Bao hilo lilizidi kuwaweka mashabiki
wa Yanga katika wakati mgumu wasiamini kilichokuwa kikiendelea uwanjani huku
wale wa Simba wakionekana kupagawa kwa furaha.
Kabla ya Simba kufunga bao la tatu,
dakika ya 64, Ngassa aliichambua safu ya ulinzi ya Simba na kufumua shuti kali
akiwa karibu na kipa Dhaira lakini kipa huyo alionyesha umahiri wake kwa kuruka
na kudaka shuti la Ngassa la kimo cha mbuzi ambalo lilielekezwa upande wa
kushoto wa kipa huyo.
Simba nayo ilikuja juu dakika ya 72
baada ya Jonas Mkude kuufumania mpira nje ya eneo la 18 na kufumua shuti ambalo
lilipaa juu ya lango la Yanga.
Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu
mno kwa Simba ambao walionekana kujichanganya kiasi cha kuruhusu mabao hayo
matatu huku wakishindwa kulitia misukosuko lango la Yanga.
Baada ya mechi hiyo, nahodha wa
Simba, Chollo alisema kuwa Yanga walicheza vizuri kipindi cha kwanza na wao
walifanya hivyo kipindi cha pili:
“Kipindi cha pili tulipewa maelekezo
na makocha wetu tukayafuata, tunashukuru tumeweza kusawazisha na tulikuwa
tunatafuta bao la kuongeza lakini muda haukuruhusu.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Cholo,
Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Singano,
Abdulhalim Humoud/William Lucian, Betram Mwombeki/Zahor Pazi, Amis Tambwe na
Haroun Chanongo/Said Ndemla.
Yanga: Ali Mustapha Barthez, Mbuyu
Twite, David Luhende, Nadir Cannavaro, Kelvin Yondani, Athuman Idd Chuji,
Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis
Kiiza/Simon Msuva.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha
pointi 19 katika mechi zake tisa wakati Yanga ambayo pia imecheza mechi tisa
imefikisha pointi 16. Matokeo hayo yanafafanishwa na fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya mwaka 2005 wakati Liverpool walipotoka nyuma ya mabao matatu na
kusawazisha yote mpaka kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chanzo:
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment