MATAJIRI wawili wenye hamasa kubwa
kwa mashabiki wa Simba na Yanga, Zacharia Hanspoppe (Simba) na Yusuph Manji
(Yanga) jana Jumapili walionyesha ubabe kwa muda kwa kucheza na akili za
mashabiki wao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea wakati wa kuanza
kwa mchezo, mapumziko na dakika za mwisho lakini kishabiki Hanspoppe alionekana
kumzidi kete Manji kwavile timu yake ilimkomboa kwa kuchomoa mabao na
kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Wakati mpira unaanza Manji ambaye ni
Mwenyekiti wa Yanga aliingia uwanjani hapo akiambatana na makamu wake, Clement
Sanga na kabla hawajakaa, Manji alizunguka akihamasisha mashabiki kuhesabu
vidole vitano akimaanisha Yanga ingeshinda kwa mabao matano kitendo ambacho
kilishangiliwa na mashabiki wa Yanga.
Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa
Usajili wa Simba, alipoona hivyo alisimama na kuwahamasisha mashabiki wa Simba
na kuwaonyesha ishara ya mabao matatu na kuwaambia watulie.
Hata hivyo hadi mapumziko Yanga walikuwa
wanaongoza kwa mabao 3-0 jambo ambalo lilimpa kiburi Manji na wakati wa
mapumziko akahamasisha tena mashabiki wake akimaanisha goli zilezile tano.
Lakini upepo ukambadilikia kipindi
cha pili timu yake iliporuhusu mabao yote matatu yakarudi ndipo Hanspoppe
akainuka na kuanza kutamba tena huku Manji na Yanga wote wakanywea kwa
kutoamini kilichotokea.
Mpaka mchezo unamalizika Yanga
walikuwa wamenywea huku Simba wakiongozwa na Hanspoppe walikuwa wakishangilia
sare hiyo ambayo ni kama ushindi kwa vile walichomoa bao zote na kuwaacha Yanga
midomo wazi.
Baada ya mchezo huo Yanga walinywea
mitaani huku Simba wakizunguka wakipiga kelele kwa mbwembwe nyingi kama
wametwaa ubingwa.
Jijini la Dar es Salaam lilikuwa
limezizima kwa kelele za mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakishangilia kwa
kutumia honi za magari, mavuvuzela na maneno ya kebehi.
Chanzo:
Mwanaspoti.com
No comments:
Post a Comment