- WAIPINGA PAC,WAJIPANGA KUCHUKUA HATUA
- WATISHA KUSUSIA KIKAO CHAKE OKTOBA 25
Rachel
Balama na Anneth Kagenda
Chama cha Wananchi (CUF),
kinatafakari hatua za kuchukua pamoja na kumuandikia barua Spika wa Bunge, Bi.
Anne Makinda aweze kuzifunda Kamati za Bunge ili zitambue wajibu wake.Tamko la
CUF linatokana na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya
Mwenyekiti wake, Bw. Zitto Kabwe, kuvitangazia kiama vyama tisa vya siasa
vinavyopata ruzuku lakini vimeshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha.
Taarifa za ukaguzi huo zilipaswa
kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa (CUF) Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema chama
hicho kinatekeleza sheria zinazovitaka vyama vya siasa kupeleka hesabu zao ili
zikaguliwe na vyombo maalumu vya Serikali.
Alisema chama hicho hakihusiki na agizo
la Bw. Kabwe aliyedai chama hicho ni miongoni mwa vyama vinavyopewa ruzuku na
kimeshindwa kuwasirisha taarifa za ukaguzi wa fedha kwa CAG katika kipindi cha
miaka minne.
"Pamoja na kumwandikia Spika barua, CUF haitakutana na Kamati
ya PAC, Oktoba 25 mwaka huu kama alivyodai Bw. Kabwe kwa sababu hatujapewa
barua ya wito hivyo hatuwezi kuitwa kihuni kupitia mitandao ya kijamii.
"Hiki ni chama cha siasa ambacho kina utaratibu wake,
hatuwezi kuitwa katika mkutano kupitia facebook, twiter, whasapp, google na
mitandao mingine ya kijamii, Oktoba 25 hatuendi na gerezani hatuwezi
kupelekwa... vielelezo vyote tunavyo na tayari vimehakikiwa na Msajili wa
Vyama," alisema.
Aliongeza kuwa, PAC imeamua kuligeuza jambo hilo kuwa mtaji wa
kisiasa na kusisitiza kuwa, hesabu ambazo chama hicho hakijawasilisha kwa CAG
ni zinazoishia Desemba 31,2012 ambazo wakaguzi wa ndani na nje wamemaliza
kuzikagua Julai mwaka huu.
Bw. Mtatiro alisema, hesabu hizo zitathibitishwa na Kikao cha
Kamati ya Utendaji Taifa mwezi huu na Baraza Kuu la Uongozi Desemba mwaka huu
hivyo hesabu ambazo bado hazijamfikia Msajili ni za mwaka mmoja uliopita.
"Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia kupitia vyombo vya
habari kuwa CUF ni miongoni mwa vyama vilivyoshindwa kuwasilisha hesabu zake
kwa CAG miaka minne mfululizo, tunaomba Watanzania wazipuuze taarifa hizo kwa
sababu hazina ukweli wowote," alisema Bw. Mtatiro.
Alisema Bw. Kabwe hana taarifa za kina jinsi CUF ilivyotekeleza
wajibu wake na kama Kamati ya Bunge inafanya kazi zake katika mitandao ya
kijamii ni jambo la kufedhehesha."Kamati makini ya Bunge ni ile inayopokea
taarifa kutoka pande zote muhimu, inakutana na wadau wote, kujua tatizo liko
wapi na kuujulisha umma nani amesababisha uzembe," alisema. Hivi karibuni
Bw. Zitto alivishutumu vyama vyote vinavyopokea ruzuku na kudai vimeshindwa
kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa hesabu kwa CAG na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Chanzo:
Majira
No comments:
Post a Comment