na Abdallah Khamis, Kaliua
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe juzi alilazimika kuhutubia
mkutano wa hadhara wilayani Kaliua, Tabora kwa njia ya simu akiwa jijini Dar es
Salaam ili kuwanusuru viongozi wa chama hicho.
Viongozi walionusurika kupigwa ni
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa CHADEMA, Msafiri Mtemelwa, wenyeviti wa
chama wa mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi.
Dalili ya viongozi hao kuwa katika
wakati mgumu zilianza kuonekana mapema wakati msafara wao ulipofika katika
Kijiji cha Ibambo, Kata ya Mwongozo bila Zitto kuwepo.
Matangazo ya awali ya mkutano wa
CHADEMA yalisema kuwa Zitto angekuwepo, lakini kiongozi huyo alisitisha
ziara yake ya kuimarisha chama ili kurejea Dar es Salaam kuhudhuria kamati za
Bunge.
Katika Kijiji cha Mwendakulima, umati
wa wananchi uliridhika baada ya viongozi kuwahakikishia kuwa Zitto atakuwepo
katika mkutano wa mwisho uliofanyika Uwanja wa Mnadani wilayani Kaliua.
Hata hivyo, kabla ya msafara wa viongozi
kufika uwanjani hapo, baadhi ya waandishi wa habari waliwasiliana na Zitto
kumuelezea hatari inayowakabili wenzake baada kutoonekana.
Zitto alisema kuwa alikosa ndege na
kuahidi kurejea katika Wilaya ya Kaliua kabla ya kufanya ziara katika Mkoa wa Kigoma.
Baada ya wananchi kubaini kutokuwepo
kwa Zitto, walizuia gari la matangazo lisiondoke na kumtaka Mtemelwa ampigie
simu ili wasikie kauli yake, vinginevyo msafara wao usingetoka salama uwanjani
hapo.
Kutokana na hali hiyo, Mtemelwa
alimpigia simu Zitto na kisha kuunganisha mazungumzo yao katika kipaza sauti
uwanjani hapo.
Zitto aliwaomba radhi wananchi wa
Kaliua kwa hali iliyojitokeza na kuwaahidi kuungana nao wakati mwingine.
“Naomba muendelee na moyo huo huo kwa
ajili ya CHADEMA, niliahidi kuwa nanyi leo ila nimeshindwa kwa sababu ya kukosa
usafiri wa kunifikisha huko, wasikilizeni viongozi mlionao nami nitaungana
nanyi wakati mwingine, nawaomba msamaha kwa hali ilyojitokeza,” alisema.
Katika hotuba yake kwa njia ya simu,
Zitto aliwaeleza wananchi juu ya umuhimu wa kujua haki zao za msingi na namna
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyowasahau wakulima na kuwakumbatia wawekezaji
huku nchi ikiendelea kubaki katika umasikini.
Wananchi waliozungumza na gazeti hili
uwanjani hapo, walimuahidi Zitto kuwa wanaruhusu msafara uendelee katika maeneo
mengine kwa sharti la yeye kurudi katika eneo hilo, vinginevyo waachane na
CHADEMA.
“Tumeahirisha mkutano mara tatu, kila
siku tunaambiwa Zitto amepata dharura, ndiyo maana leo tulitaka kuwashughulikia
hawa viongozi waliokuja bila Zitto,” alisema mmoja wao.
Awali katika Kijiji cha Mwendakulima,
wananchi walieleza namna chama cha msingi kinavyowadhulumu fedha za mauzo ya
tumbaku na kwamba wanaohoji juu ya hilo hufukuzwa uanachama.
Walisema tayari wanachama zaidi ya
180 wameshafukuzwa kutokana na kudai fedha za mauzo ya tumbaku.
Katika Kijiji cha Ibambo, Kata ya
Mwongozo, CCM ililalamikiwa kupora jengo la wananchi na kulifanya mali yake.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibambo,
Erasto Mazinge aliwaeleza hayo baada ya waandishi kutaka ufafanuzi wa ofisi ya
serikali kuwa katika sehemu moja na ofisi za CCM.
Mazinge alisema licha ya wananchi
kujenga jengo la vyumba nane kwa matumizi ya serikali, CCM iliamua
kuwabadilikia na kulifanya ni jengo la chama.
Kauli ya Mazinge inaungwa mkono na John
Kapongo, Katibu wa Tawi la CCM Mwongozo, aliyesema chama chake kilitumia mbinu
ya kuwalaghai wananchi kujitolea kujenga jengo hilo kwa ajili ya matumizi ya
serikali.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment