Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana
amefuta agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli la kuwataka
wamiliki wa magari makubwa ya mizigo, kutozwa asilimia tano kwa kila gari
litakalozidisha uzito na kuagiza kurudiwa kwa utaratibu wa zamani wa msamaha wa
asilimia tano ya tozo hiyo.
Pinda pia ametoa muda wa mwezi mmoja
kwa Wizara ya Ujenzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Viwanda na
Biashara, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Waziri Mkuu
kukutana na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa),Chama cha Wamiliki
wa Malori (Tatoa) ili kukubaliana kwa pamoja kuhusu tozo hiyo. Agizo hilo la Magufuli alilolitoa takribani siku nne zilizopita,
liliathiri kasi ya upakuaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na mgomo huo wa
malori.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Pinda alisema, katika mazingira yaliyopo sasa, ushirikiano kati ya
Serikali na wadau unahitajika. "Ni lazima wadau washirikishwe ili kusiwe
na malalamiko na mambo yaende vizuri," alishauri Pinda.
Alisema, awali utaratibu uliokuwa
unatumika ulipewa baraka na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu (sasa Ujenzi),
Basil Mramba ambaye baada ya wadau wa usafirishaji kulalamika kuhusu ubovu wa
barabara na mizani, alitoa unafuu wa kupunguza asilimia tano ya uzito
utakaosomwa katika mizani (utakaozidi).
"Lengo lake ilikuwa
ni kufidia matatizo ya upungufu wa mizani kutoweza kupima kwa usahihi uzito wa
magari yanayopimwa katika vituo mbalimbali vya mizani nchini, lakini hivi sasa
mizani yetu ni mizuri na ya kisasa," alisema na kuongeza:
"Lakini ikumbukwe kuwa agizo hilo lilikuwa kinyume na
Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 toleo la 2002 na kanuni zake za mwaka
2001, ambayo inazuia malori kuzidisha uzito. Mramba aliamua vile ili kumaliza
hali iliyokuwa imejitokeza wakati akiwa Wizara ya Miundombinu," aliongeza
Pinda.
Alisema kati ya kanuni hizo, kanuni ya 7(3) inatoa sharti la kama lori likibainika kuzidisha mzigo,sharti ni ama
kupanga upya mzigo ili kupunguza uzito,kuushusha mzigo uliozidi au kupigwa
faini mara nne ya faini ya kawaida. Pinda alisema baada ya kuibuka kwa mgomo
huo alikutana na wadau wa usafirishaji na mawaziri wa wizara zenye dhamana na
ujenzi na usafirishaji, kubaini kuwa kulikuwa na ulazima wa wizara hizo
kukutana na wadau ili wakubaliane.
Bandari walia na mgomo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
(TPA),imeeleza kuwa wananchi ndiyo wataumia kwa kulazimika kulipa hasara
iliyotokana na mgomo huo.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa Bandari
hiyo, Janeth Ruzangi alisema hali hiyo itatokana na wafanyabiashara kulazimika
kupandisha bei ya bidhaa mbalimbali zilizokwama kwa siku kadhaa bandarini hapo
ili kufidia gharama walizotozwa na wamiliki wa meli.
Chanzo: Mjengwablog
No comments:
Post a Comment