Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi
Communications limited (MCL)Tido Mhando akizungumza na waandishi wa habari
jijini kuhusu kuanza uchapishaji leo wa gazeti la Mwananchi lililokuwa
limefungiwa kwa wiki mbili. Kulia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo Denis Msacky. PICHA
| FIDELIS FELIX
Kwa ufupi
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za
kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa
wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia.
Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini
wameumia pamoja na familia zao.
Habari kamili
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa
kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya
kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe ya
mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa
nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu mazito
ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo
iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika
wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali
yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti
hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya
ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka yoyote
kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika mamlaka za juu
serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa watumishi wa
Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya Serikali kutaka wananchi
wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla
ya gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari
kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali
uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni hili:
Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na mishahara mipya
kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa
Serikali kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora
hata kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack
Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti
17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha
ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake
kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo wangeandamana
kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania,
Sheikh Ponda Issa Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na
kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari;
‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’ ilichapishwa ikiwa na mmoja
wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu
baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16.
Habari hiyo ilisema Waislamu
hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao waliokuwa
na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria walitanda katika mitaa
mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi.
Lakini kwa mshangao wetu, Serikali
katika kujaribu kuhalalisha kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo
kwamba habari tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya
ibada, wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama
hicho.
Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo
lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo
vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo
iliudhalilisha Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo
kuacha shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa
sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors)
waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea
wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma
gazetini wameumia pamoja na familia zao.
Hivyo hivyo, watoa matangazo na
wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika nao pia
wameumia. Hasara ambayo MCL imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali
haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa
kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya
taaluma yao.
Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.
Hata hivyo, inapotokea tukafanya
makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka kwa lengo la kupunguza maumivu kwa
yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama
kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu
anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni kujitakia kiama.
MCL imeweka miongozo ya sera na
malengo ya uhariri kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari zinazochapishwa
ni sahihi, zinatenda haki na haziegemei upande wowote. Kwa maana hiyo, vyombo
vyake vya habari vinasimamia ukweli na haki na waandishi wake wana jukumu la
kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu cha weledi na maadili ili kuwawezesha
kutoa habari kwa umma.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo
muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya
Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu
wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta.
Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika
kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya
pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga
hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi
za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii
kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa
kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini
tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza
wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment