Friday, October 11, 2013

UCHAMBUZI WA HOTUBA YA JK NA MGONGANO WA MASWALI





Hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete na kuzungumzia kwa undani mchakato wa Katiba Mpya, imeacha maswali mengi huku ikiashiria kutokuwapo kwa mawasiliano madhubuti ndani ya Serikali kuhusu suala hilo.

Kadhalika, hotuba hiyo imeibua mambo mawili ambayo ni hofu ya kuahirishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba na kuzidi kwa lawama dhidi ya wabunge wa CCM pamoja na uongozi wa Bunge, hususan Naibu Spika, Job Ndugai.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya muswada wa awali kupitishwa, baadhi ya mawaziri walinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakisema kusingekuwapo na mwanya kwa Rais Kikwete kukutana na wapinzani kwani upitishwaji wa sheria hiyo ulifuata taratibu zote za kibunge.

Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake ya Septemba mwaka huu kwa taifa, alitangaza kuwapo fursa ya majadiliano baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya upinzani; Chadema, CUF na NCCR Mageuzi ambavyo tayari vilikuwa vimeungana kupinga mchakato huo.

Viongozi wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi) walichukua hatua ya kuhamasisha umma kutokubaliana na mchakato huo, wakirejea kutoridhika na jinsi Bunge lilivyoshughulikia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kauli ya Rais Kikwete kuwaalika wapinzani kwenye meza ya mazungumzo, inatafsiriwa na baadhi ya wasomi kuwa ni aibu kwa Bunge na wabunge waliopitisha sheria hiyo na kwamba ni dhahiri kwamba itarejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Mwanza, Steven Dasu alisema Rais Kikwete ameridhia kuzungumza na wapinzani baada ya kubaini kuwapo udhaifu katika mchakato wa kupitisha sheria husika bungeni na kwamba hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa Katiba yenye tija kwa nchi.

Hata hivyo, Ndugai jana alitetea uongozi wake bungeni huku akisema: “Bunge limefanya kazi yake, inawezekana liliamua vibaya au liliamua vizuri lakini uamuzi ulifanyika. Sasa kama sheria iliyopitishwa ina kasoro inaweza kurekebishwa tu kulingana na taratibu zilizopo”.

Pia aliwaponda wapinzani kwa kile alichokiita kuwa ni kukimbilia kwa Rais, badala ya kujenga hoja zao ndani ya Bunge na kwamba lazima watambue kuwa tabia hiyo haitawapeleka mbali.

Lawama kwa wabunge
Wakili wa kujitegemea, Dk Rugemeleza Nshala alisema wabunge hawakuwa makini na kwamba miswada inayotungwa na Bunge kurudishwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuanza kutumika “ni aibu kwa mhimili huo”.

Pia Dk Nshala alisema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwani wabunge wanapokaa na kufanya kazi bila umakini inalazimu warudi tena kufanya kazi ileile huku wakilipwa.

Naye mwanasheria wa siku nyingi wa Moshi Mjini, Peter Shayo alisema: “Tafsiri ya uamuzi huu wa Rais ni kuwapo kwa incompetence (upungufu) kwenye system (mfumo) ya Bunge. Wabunge waliopitisha sheria hiyo hawakutimiza wajibu wao vizuri.
“Wenzao wa upinzani waliuona upungufu huo mapema na kuusema lakini wakazidiwa na self interest (masilahi binafsi) ya CCM.Sasa unarudishwa bungeni kwa agizo la Rais, waliopitisha wanajisikiaje?”

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Amir Manento aliungana na Rais Kikwete akisema: “Katiba ni suala la wananchi wote, halipaswi kuwa la kikundi cha watu au chama cha siasa.

“Ninachoona, ndicho Rais alichoona na sasa anataka kuweka mambo sawa. Ukipeleka suala la Katiba kwa kuegemea upande fulani unaweza usipate matunda uliyotegemea. Suala hili ni nyeti kidogo na busara inatakiwa zaidi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Eugenia Kafanabo alisema hashangazwi na muswada huo kurejeshwa bungeni kwa sababu ulipitishwa huku baadhi ya wabunge wakiupinga baada ya kuona makosa na kwamba Rais Kikwete ameona upungufu huo.

“Ulipitishwa kwa kulazimishwa, baadhi ya wabunge walisema uko sahihi, wengine wakitaka ufanyiwe marekebisho. Katiba ni sheria mama lazima upatikanaji wake uwe wa maridhiano, lazima wanaotengeneza Katiba husika waridhiane na kusiwe na malalamiko,” alisema Kafanabo.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema suala la Rais kusaini muswada huo, kisha kurudishwa bungeni ni utaratibu wa kawaida.

Alikanusha taarifa kwamba hakuna mawasiliano baina ya Rais na mawaziri wake na kwamba suala la sheria kurejeshwa bungeni ni la kawaida. “Ni utaratibu wa kawaida tu kurekebisha sheria ambayo imeshasainiwa, hakuna kitu kipya hapo unaweza kufanyiwa marekebisho mpaka mara tatu.”

Kuhusu kile ambacho Rais Kikwete alikizungumza kwenye hotuba yake ya Septemba, waziri huyo alisema wanasubiri maelekezo yake ambayo ni dhahiri yatatokana na mwafaka utakaopatikana kwenye mazungumzo baina yake na viongozi wa upinzani.

Bunge la Katiba
Uamuzi wa Rais Kikwete kukutana na wapinzani kujadili suala hilo, pia umezua hofu ya kuchelewa kwa Bunge la Katiba ambalo linapaswa kufanyika mwezi ujao.
Hofu hiyo inatokana na suala la marekebisho ya sheria ambayo ilipitishwa na Bunge kutokuwamo katika ratiba ya sasa ya vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inakutana kwa siku ya tano leo. Kamati hiyo ndiyo yenye dhamana ya kupitia na kuifanyia uchambuzi miswada ya sheria kabla ya kufikishwa Bungeni.

Juzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwasilisha mbele ya kamati hiyo miswada ya sheria ambayo inapaswa kupelekwa katika Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza Oktoba 29, mwaka huu lakini marekebisho ya sheria iliyozua mvutano si sehemu ya miswada hiyo. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema ikiwa marekebisho yanayokusudiwa kufanywa hayatapelekwa katika mkutano ujao wa Bunge, basi ni ishara kwamba Bunge la Katiba litachelewa.

“Bunge la Katiba haliwezi kufanyika bila sheria husika kukamilika. Kwa hiyo kama Serikali itaamua kuurejesha muswada huo bungeni lazima liwe ni Bunge hili linalofuata, tofauti na hapo utaathiri Ratiba ya Bunge la Katiba,” alisema Mdee.

Kwa upande wake, Chikawe alisema hata kama Rais ataamua kurejesha sheria hiyo Bungeni, hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu muda wa Bunge la Katiba kwani kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa... “Tusubiri maelekezo kwanza hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Kama kutakuwa na maelekezo kuna uwezekano wa kurekebisha na kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.

Miongoni mwa mambo ambayo yanalalamikiwa na wapinzani ni pamoja na madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni na utaratibu wa kufikia uamuzi katika Bunge la Katiba.

Rais Kikwete katika hotuba yake alionekana kukubaliana na baadhi ya hoja za wapinzani huku akitaka suala la Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutofanya vikao na wadau wa Zanzibar lirejeshwe bungeni kwa lengo la kupata mwafaka wa pamoja.

Kuhusu kura katika Bunge la Katiba, Rais Kikwete alisema wingi wa wabunge wanaotoka pande za muungano siyo hoja, kwani Katiba ya sasa iko wazi kwamba masuala yote ya muungano yatapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka kila upande. 

Hata hivyo, msimamo huo wa Rais unapingana na kile kilichopitishwa na Bunge ambacho ni nyongeza ya kipengele kinachoeleza kwamba, ikiwa kura zitapigwa mara mbili na jambo linalobishaniwa likakosa kuungwa mkono kwa theluthi mbili ya kura, basi suala hilo litapitishwa kwa kuangalia idadi ya kura kwa maana ya wingi pekee (simple majority).

Wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa anapinga wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuteuliwa na Rais, kupendekeza ufanyike uchaguzi... “Wanatakiwa wawepo wajumbe ambao hawafungamani na upande wowote, akiwamo Rais.

CCM wabadili msimamo
Msimamo wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, unaonekana kuwagawa wanachama wa chama hicho wakiwamo wabunge ambao wanalaumiwa kwamba walipitisha muswada wa sheria husika kwa kuweka mbele masilahi ya chama badala ya mustakabali wa Taifa.

Msingi wa lawama hizo ni vurugu zilizotokea bungeni Septemba 6, mwaka huu na kusababisha wabunge wa Chadema, NCCR Mageuzi na CUF kususia mjadala wa sheria husika, hivyo kuwapa mwanya wenzao wa CCM.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya alisema kitendo cha mawaziri na wabunge kupitisha muswada huo, kinaonyesha jinsi wanavyothamini masilahi ya chama chao kuliko ya taifa.

“Walipitisha muswada ule kwa kutazama zaidi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wao nia yao ni kuendelea kukaa madarakani. Katika suala hili, Rais lazima asimame kidete maana yeye hana cha kupoteza, ” alisema Mallya.

Wakili wa Kujitegemea, Karoli Muluge alisema mvutano uliopo sasa unatokana na muswada huo kuandaliwa na watu wa CCM, hivyo kuweka vipengele ambavyo vitakibeba chama hicho.

“Viongozi wanatakiwa kuwasikiliza wananchi na kujua kitu gani kinatakiwa kufanyiwa marekebisho katika muswada husika. Watu wasikilizwe kwa sababu wameeleza wazi upungufu uliopo,” alisema Muluge.

Katika vikao vyake vya juu, CCM kilifikia uamuzi wa kupinga mapendekezo ya Serikali tatu yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi ambao ulifuatiwa na baadhi ya makada wake kuwakejeli wajumbe wa tume hiyo, akiwamo Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Joseph Warioba.

Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake alizipa kisogo kejeli hizo, pale aliposema kuwa tume hiyo ilifanya kazi nzuri, kwani ilizingatia masilahi mapana ya nchi kwa kuwasemea watu wote bila ya kubagua.

“Natambua kuwapo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu nao waige mfano huu mzuri. Wajali masilahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao,” alisema Kikwete.

Kauli hii inatafsiriwa kuwa ndiyo msingi wa msimamo wa CCM uliotangazwa na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye alisema licha ya baadhi ya wanachama wake kuonekana kuilaumu na kuiponda Tume ya Warioba, chama chenyewe “kinaikubali na kuiunga mkono.

“CCM ina wanachama zaidi ya milioni sita, huwezi kuchukua maoni ya mmoja wa wanachama wake ukayachukulia kama msimamo wa chama. CCM kama taasisi kina msimamo wake unaotolewa na msemaji wake ambao ndiyo huu. Nakuambia sisi tunaiunga mkono Tume ya Jaji Warioba na tunaikubali.”

Wabunge wa CCM
Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rweikiza alimshauri Rais asaini muswada huo mara moja ili mchakato wa Katiba uendelee kama kawaida.
“Hawa wenzetu, wao waliamua kutoka nje ya ukumbi badala ya kukaa wakawasilisha hoja zao. Sisi tulijadili na kufuata taratibu zote, kwa hivyo Rais ana haki kabisa ya kusaini na kama kuna marekebisho atarejesha tena bungeni.

Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema anaunga mkono hoja ya Rais Kikwete ya kufanyiwa marekebisho katika sheria hiyo kwani nia ni kupatikana kwa Katiba itakayosaidia nchi.

“Kama zipo hoja tuungane tuzizungumze na kuja na kitu kimoja kitakachokuwa na masilahi ya taifa. Tusivutane bila sababu za msingi, kwa sababu tunajenga nyumba moja.” Alisema wapinzani walipaswa kujenga hoja zao ndani ya Bunge badala ya kutoka nje na kususia vikao.“Sasa marekebisho yanategemea na uhitaji, sioni shida, kama Rais ameusoma na kuona kama kuna marekebisho hakuna tabu…

Sheria hizi zinatarajia utashi, kitu ambacho sisi tumetunga na kukipitisha kinaweza kuwa sahihi lakini mtu mwingine anaweza kuangalia akaona siyo sahihi,” alisema Mpina.
Imeandikwa na Tausi Mbowe, Joyce Mmasi, Fidelis Butahe na Fredy Azzah (Dar), Daniel Mjema (Moshi) na Sheilla Sezzy (Mwanza).
                                         Chanzo: Mwananchi

No comments: