Shirika
la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo, European Network on
Debt and Development (Eurodad) watafanya
ziara ya kiuchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya
kuanzia tarehe 20 Oktoba mpaka tarehe 5 Novemba mwaka 2013. Uchunguzi huo
utaendeshwa na wataalamu waliobobea wa masuala ya kodi na maendeleo. Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa Bunge la Tanzania Zitto Zuberi
Kabwe ameteuliwa kuongoza Jopo la uchunguzi huo.
Eurodad
ni Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19 za
Ulaya ambayo yanajihusisha na masuala ya kufutia madeni nchi zilizoendelea,
misaada yenye maana na kodi za haki. Mashirika haya yamekuwa kwenye kampeni ya
kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya
kimataifa kwa nchi zinazoendelea. Zitto amekuwa mmoja wa wabunge wanaosimamia
hoja ya kutaka Watanzania waliotorosha fedha kwenda nje warejeshe na
kufunguliwa mashtaka.
Mwaka 2012 aliwasilisha hoja binafsi Bungeni na
kupitishwa kuwa Azimio la Bunge ya kutaka uchunguzi kuhusu utoroshwaji wa fedha
na kufichwa nje kama Uswiss. Kikosi Kazi cha Serikali kutekeleza Azimio hilo la
Bunge kinatarajia kuwasilisha taarifa yake katika Mkutano wa Kumi na Sita wa
Bunge. Siku ya Jumatatu tarehe 21 Oktoba Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa
Uswiss na maafisa wa mabenki na asasi zisizo za kiserikali zilizopo jijini
Geneva.
Pia Zitto atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa
katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za kimataifa ili kuzuia unyonyaji wa
nchi za Kiafrika unaofanywa na Makampuni makubwa ya Kimataifa.
Baada
ya Geneva Zitto atatembelea nchi za Luxembourg na Brussels kabla ya kwenda
Norway ambapo atamalizia ziara yake kwa Jopo la Wataalamu wa masuala ya kodi na
Maendeleo kuandika taarifa maalumu yenye mapendekezo kuhusu kuzuia utoroshaji
wa fedha kutoka Afrika.
Zitto
atakwenda jijini London kutoa mada kuhusu masuala ya kodi za kimataifa katika
mkutano wa Uwazi (Open Government Partnership). Mwenyekiti wa PAC Tanzania
atafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa PAC Uingereza Bi Margaret Eve Hodge, Lady
Hodge MBE, PC, MP kuhusu masuala
mbalimbali ya ushirikiano wa mabunge mawili na kuendeleza wito wake kwa
makampuni ya kimataifa kulipa kodi zao barani Afrika na kuacha tabia ya kutumia
‘Tax Havens’ kukwepa kodi na kufukarisha nchi za Kiafrika.
Chanzo:
http://www.matukiodaima.com
No comments:
Post a Comment