Taarifa
zilizolifikia Mwananchi Jumapili na kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza
kuwa Eurodad ambao ni mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi
19 za Ulaya, yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi
zinazoendelea, kwa muda sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
Picha na Maktaba
Na Fidelis
Butahe, Mwananchi
Kwa ufupi
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo
hadi Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya
uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Dar es Salaam. Wakati ikisubiriwa
ripoti ya uchunguzi wa Tume Maalumu iliyoundwa kwa Azimio la Bunge kuchunguza
kashfa ya vigogo walioficha Sh323.4 bilioni katika benki nchini Uswisi, Shirika
la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), leo linaanza
kuwachunguza walioficha mabilioni hayo ya fedha nchini humo.
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo
hadi Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya
uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Uchunguzi huo utafanywa na jopo la
wataalamu waliobobea katika masuala ya kodi na maendeleo na wataongozwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye pia ni
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa
bungeni kwa hoja binafsi ya Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha
kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Kufuatia hoja hiyo, Bunge chini ya
Spika Anne Makinda liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia
Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo
bungeni.
Ripoti ya Tume hiyo iliyoundwa na
Serikali kwa Azimio la Bunge ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana, ikiongozwa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, mpaka sasa tayari
imewahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Muda wa tume hiyo kufanya uchunguzi
unakamilika mwezi huu na inatarajiwa katika mkutano ujao wa Bunge unaoanza
Oktoba 29 mjini Dodoma, itawasilisha ripoti hiyo.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi
Jumapili na kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza kuwa Eurodad ambao ni
mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya,
yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea, kwa muda
sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
“Mashirika haya yamekuwa kwenye
kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na
mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kesho
Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswisi na maofisa wa benki mbalimbali na
asasi za kiserikali zilizopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Geneva.
“Zitto pia atahudhuria mkutano wa
Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za
kimataifa ili kuzuia unyonywaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na kampuni kubwa
za kimataifa,” inaeleza taarifa hiyo.
Juzi 21 mwaka huu, Werema alizungumza
na Mwananchi Jumapili na kuthibitisha kuhojiwa kwa vigogo hao 200, lakini
akasita kuwataja kwa majina kwa maelezo kuwa asingeweza kuwataja kwa kuwa
uchunguzi bado ulikuwa unaendelea.
“Uchunguzi huo unaendelea,” alisema
Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema
kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,”
alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika
tu.”
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya
Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) kutoa taarifa Juni,
2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi
ya Watanzania wenye akaunti zenye fedha zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni
sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la
‘The Indian Ocean Newsletter’ toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema
uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa
na viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa
Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa
Sheria wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na Ofisi ya
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la
kimataifa, miongoni mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu
wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya Dola133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa
Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika
wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki zilizoko
nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa mara kwa miaka
mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka
kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje ya
nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Akiwa mkoani Tabora wiki moja
iliyopita katika mikutano ya kuimarisha chama, Zitto alisema tayari
amemwandikia barua Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe
katika mkutano ujao.
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment