Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hali ya
vurugu zinazoendelea Mtwara katika sakata la mradi Gesi asilia kuja
Dar es Salaam.PICHA NA VENANCE NESTORY
Na Neville
Meena, Mwananchi
Dodoma: Wabunge Wawili Maarufu wa Chadema,
Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wameingia katika
vita ya maneno ambayo chanzo chake ni kauli ya Lema aliyotoa katika kikao cha
wabunge (briefing) kilichofanyika mjini Dodoma Jumanne wiki hii.
Lema akizungumza katika kikao hicho,
anadaiwa kutoa maneno ambayo yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa yalikuwa
yakimlenga Zitto kuhusu hatua yake ya kukataa posho na kumtuhumu kwamba ana
ukwasi ambao unapaswa kuhojiwa.
Gazeti hili lilimtafuta Lema
likirejea taarifa iliyotolewa na Zitto akilalamika kwamba Lema alimshambulia
katika kikao hicho cha wabunge wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.
Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia
suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama
kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha
nilichokisema”.
Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa
msimamo wa Lema ulikuwa unapingana na wabunge wengine wa Chadema, ambao
waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe,
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, posho za
vikao na ndiye mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011,”
aliongeza Zitto, ambaye anahudhuria mkutano unaozungumzia uendeshaji wa
Serikali kwa uwazi huko London, Uingereza.
Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka
sasa ni makubwa sana ukilinganisha na hali ya wananchi wakati Serikali ikishindwa
kulipa vizuri walimu na wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza
kulilia posho, wakati wananchi wetu hawana maji, hatuwezi kulilia posho. Mbunge
anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza kuwakilisha
watu waendelee,” alisema Zitto.
Lema, hata hivyo, alisema kwamba
katika mkutano huo aliweka bayana kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza
kuwa wabunge wanapaswa kuwa na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu wa
kuwatetea watumishi wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja
kupewa maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni
haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi
wengine,” alisema Lema na kuongeza:
“Kwahiyo nikasisitiza kwamba
nawashangaa wale ambao wanakataa posho ya Sh80,000 na ukienda kuchunguza
wanakatwa fedha zote kutokana na mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu
kama Arusha wanalala kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za Marekani
150 na 600”.
Alisema katika mazingira hayo
kunakuwapo maswali mengi yasiyokuwa na majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo
alitakiwa anapokuwa katika mji wowote nchini aishi katika hoteli yenye thamani
kati ya Sh20,000, 30,000 na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya
Sh80,000 halafu unalala chumba cha Dola 600 hustahili kupata credibility (sifa)
stahili, ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema Lema.
Alisisitiza kwamba wabunge wa
Tanzania hawalipwi ipasavyo na kwamba kudai malipo ya ziada hakuwaondolei
wajibu wao wa kuwatetea watumishi wengine wa umma ambao pia malipo yao ni
kidogo.
“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000
au Sh200,000 ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa Sh50,000
basi maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata
Sh10,000,”alisema
Chanzo:
Mwananchi
No comments:
Post a Comment