Kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23
Bertrand Bisimwa.
Waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo kwenye eneo la vurugu mashariki mwa nchi hiyo wametangaza kukomesha
uasi wao wa miezi 18 baada ya kushindwa na vikosi vya serikali vikisaidiwa na
vile vya Umoja wa Mataifa.
Taarifa ya kundi la M23 ilitolewa
hapo Jumanne kwamba itamaliza uasi wake na badala yake itapigania malengo yake
kwa njia za kisiasa inakuja baada ya takriban waasi 200 waliokuwa wamejichimbia
milimani kutimuliwa na mashambulizi ya vikosi vya serikali ya Congo.
Wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa,
Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya wamelikaribisha tangazo hilo na kusisitiza
katika taarifa ya pamoja kwamba hiyo ni hatua moja katika kuushughulikia mzozo
ulioichagiza Congo na ukosefu wa utulivu nchini humo pamoja na kukomesha
umwagaji damu unaofanywa na makundi yote ya wapiganaji yasio halali nchini
humo.
Balozi wa Marekani nchini Congo Russ
Feingold ameita hatua hiyo kuwa muhimu na ya kusisimua inayoelekea kwenye
mwelekeo sahihi.
Kundi la M23 ladhoofika
Kundi la M23 linadaiwa kuwa lilikuwa
likipatiwa msaada wa kijeshi na wa kifedha kutoka Rwanda nchi ambayo rais wake
ni Mtutsi.Serikali ya Rwanda imekanusha madai hayo licha ya ushahidi uliotolewa
katika repoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa.Hata hivyo uungaji mkono wao huo
umeonekana kupunguwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ongezeko la
shinikizo la kimataifa kuitaka nchi hiyo kuacha kuchochea mizozo ya Congo kwa
kuunga mkono waasi.
Rais wa kundi la M23 Betrand Bisimwa
amesema katika taarifa hapo Jumanne kwamba anawaamuru makamanda wa waasi
kuviandaa vikosi vyake kwa ajili ya mchakato wa kusalimisha silaha,kuvunjwa kwa
kundi hilo na kujumuishwa katika jamii chini ya masharti ya yatakayofikiwa katika
makubaliano ya amani na serikali ya Congo.
FDLR kuandamwa
Katika mji mkuu wa Kinshasa msemaji
wa serikali ya Congo Lambert Membe ameapa kwamba jeshi la nchi hiyo hivi sasa
litaelekeza juhudi zake katika kuwaadama wapiganaji wa Kihutu kutoka kundi la
FDLR ambalo alinaongozwa na Wanyarwanda waliosaidia kufanya mauaji ya kimbari
nchini humo hapo mwaka 1994.
Takriban wapiganaji 100 wa kundi la
M23 wametekwa na vikosi vya serikali na kiongozi wa kundi hilo Sultani Makenga
na maafisa wengine waandamizi inaaminika wamekimbilia katika nchi jirani ya
Rwanda au Uganda.
Kuvunjwa kwa kundi la M23 kunatowa
ushindi wa wazio na mkubwa kabisa kwa serikali ya Congo tokea kwa uasi wa
kutaka kujitenga wa mwaka 1963 katika jimbo la kusini la Katanga.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment